Jeshi la Polisi Lafanikiwa Kusuluhisha Mgogoro wa Kugombania Mifugo, Mara
POLISI kata wa kata ya Isenye Wilaya ya Serengeti mkoani Mara Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Method Kagina, amefanya jitihada za kusuluhisha mgogoro wa kugombania mifugo kati ya mjane Shoma Maduhu mkazi wa kijiji cha Nyiberekera na ndugu wa marehemu mumewe. alikumbana na changamoto baada ya ndugu wa marehemu kumnyang’anya mifugo iliyokuwa mali ya mumewe.
Katika hatua za kushughulikia mgogoro huo, Kagina alikutana na pande zote mbili ili kuweza kuelewa chanzo cha mgogoro huo na kuwakumbusha wajibu wao kisheria.
Kwa kupitia mazungumzo na elimu ya kisheria, ndugu wa marehemu walieleweshwa kuhusu haki za mjane na umuhimu wa kumsaidia katika kipindi hiki kigumu.
Na mara baada ya pande zote mbili kuelimishwa kisheria Septemba 29,2024, mifugo hiyo ilikabidhiwa rasmi kwa Shoma Maduhu, hatua ambayo inadhihirisha umuhimu wa ushirikiano kati ya jamii na vyombo vya sheria katika kutatua migogoro Kagina aliweka msisitizo kwamba utatuzi wa amani wa matatizo ya kijamii ni muhimu katika kujenga jamii imara na yenye umoja.