JESHI SUDAN LAKUBALI KUGAWANA UONGOZI NA RAIA

BARAZA tawala la kijeshi na viongozi wa upinzani nchini Sudan, wamesaini makubaliano ya kugawana uongozi baada ya mazungumzo ya usiku kucha kumaliza mzozo nchini humo.

Baada ya makubaliano hayo kumefanyika sherehe katika hoteli ya Corinthia katika mji mkuu wa Khartoum.

Makubaliano hayo yanatazamiwa kuchukua miaka mitatu ya uongozi wa pamoja utakaofuatwa kwa uchaguzi mkuu. Baada ya kusainiwa kwa makubaliano hayo, viongozi wa pande zote wamezungumzia kizazi kipya katika taifa ambalo limeshuhudia ghasia na mauaji ya mamia ya waandamanaji tangu kutimuliwa kwa kiongozi aliyekuwepo,  Omar El Bashir,  mnamo Aprili.

Katika makabiliano na jeshi yaliyogeuka kuwa ghasia zilizosababihsa vifo vya watu, waandamanaji walitaka jeshi likabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia. Utiaji saini wa makubaliano hayo, unaonekana kuthibitisha makubaliano yalioidhinishwa kimsingi mapema mwezi huu.

Makubaliano hayo yanaeleza kwamba jeshi litakuwa uongozini kwa miezi 21 ya kwanza, na baada ya hapo utawala wa kiraia utaidhinishwa katika miezi 18 itakayofuata, na kufuatwa kwa uchaguzi mkuu. Makubaliano ya pili kuhusu masuala ya katiba yanatarajiwa kukamilishwa Ijumaa wiki hii.


Loading...

Toa comment