The House of Favourite Newspapers
gunners X

Jeuri ya Harmo Yafichuka, Mtu mzito Nyuma ya Pazia Atajwa

0

AGOSTI 22, mwaka huu (Jumapili iliyopita), staa wa Bongo Fleva, Rajab Abdul almaarufu Harmonize au Konde Boy Mjeshi alitimiza miaka mitatu tangu alipojitoa kwenye lebo iliyomkuza kimuziki ya Wasafi Classic Baby (WCB) iliyo chini ya staa mwingine wa muziki huo, Nasibu Abdul au Diamond Platnumz.

 


Watu mbalimbali
wamezungumzia miaka mitatu ya Harmonize au Harmo nje ya Wasafi ambapo wamesema kuwa, msanii huyo ni miongoni mwa wasanii waliofanikiwa pakubwa katika Ukanda wa Afrika Mashariki huku mwenyewe akifichua jeuri ya mafanikio yake.

 


HARMONIZE NA IJUMAA

Katika mazungumzo na Gazeti
la IJUMAA hivi karibuni, Harmo au Tembo aliwataka vijana kukabiliana na changamoto wanazopitia kwa lengo la kufikia mafanikio waliyojiwekea.“Kila kitu kinachotokea katika maisha kichukue kama changamoto, ni muhimu kukabiliana nacho na kuwathibtishia watu kwamba unaweza kupambana nacho,” anasema Harmonize.

Harmonize anasema kuwa, wimbo wake wa Never Give Up unaelezea kila kitu kuhusu maisha na mtu kutokata tamaa.Mjeshi huyo anasema kuwa, kila kitu kilichopo katika wimbo huo ni cha ukweli juu ya maisha yake binafsi .Harmo anasema kuwa, lengo la kuanzisha lebo yake ya Konde Gang Music Worldwide ni kutaka kujisimamia mwenyewe kimuziki, lakini kubwa zaidi ilikuwa ni ndoto yake kumiliki lebo.


MAFANIKIO NJE YA WASAFI

Wimbo uliomtoa Harmo
kimuziki ni Aiyola ulitoka Agosti 25, 2015 ukitayarishwa ndani ya studio za Kazi Kwanza Record chini ya Prodyuza Maxmaizer.Video ya wimbo huo ilifanyika jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini na kutoka Novemba 6, 2015 ikiwa imeongozwa na Director Nick Roux.

 

Kipaji cha Harmo kilionekana kikubwa na ndiyo sababu Lebo ya Wasafi haikuona taabu kutoa pesa kwa ajili ya kufanya video hiyo inayotajwa kuwa ya gharama kubwa.Wimbo huo wa Aiyola ukawa mkubwa kwa kiasi chake na kuvutia wengi ndani na nje ya nchi na haikuwa ajabu pale msanii wa Nigeria, Kiss Daniel alipoonesha kuukubali.Huo unatajwa kuwa mwanzo wa kupata maisha mazuri kupitia muziki kutoka maisha ya kubangaiza katika Mitaa ya Kariakoo jijini Dar hadi kuwa staa mkubwa.Mafanikio mengine ya Harmo ni kushinda Tuzo za African Muzik Magazine Awards (AFRIMMA) zilizotolewa Dallas

Texas nchini Marekani kama Msanii Bora Chipukizi 2016.Hata kabla ya kusepa Wasafi, Harmo alikuwa amefanya kolabo na wasanii kutoka nchi mbalimbali barani Afrika kama Marina (Rwanda), Yemi Alade (Nigeria), Eddy Kenzo (Uganda), Emma Nyra (Nigeria), Willy Paul (Kenya), IYO (Nigeria), OmoAkin (Nigeria), Korede Bello (Nigeria), Sarkodie (Ghana) na wengine wakali.


MAFANIKIO NJE YA WASAFI

Kuelekea mwishoni mwa
mwaka 2019, Harmo aliondoka Wasafi akiwa ni msanii wa pili kufanya hivyo baada ya Rich Mavoko.Kwa mujibu wa Harmo, kuondoka Wasafi haikuwa kazi rahisi kwani ili kuvunja mkataba wake na lebo hiyo ilimlazimu kulipa shilingi milioni 500 kwa kuuza nyumba zake tatu alizokuwa amepata ndani ya miaka mitatu kutokana na muziki.


MAFANIKIO YA ALIBAM YA
AFRO EAST
Nje ya Wasafi, mwaka
jana, Harmo aliachia albam iliyokwenda kwa jina la Afro East akiwashirikisha wasanii wengi ndani na nje ya Bongo kama Burna Boy, Mr Blue, Lady Jaydee, Morgan Heritage, Khaligraph Jones, Phyno, Skales, Yemi Alade, Mr Eazi, Falz na wengineo.Albam hiyo bado inaendelea kufanya vizuri na kuweka rekodi mbalimbali kwenye mitandao ya kusikiliza, kutazama, kuuza na kununua muziki na kupiga mkwanja mrefu akitajwa kama msanii wa pili Bongo anayeingiza pesa nyingi kwenye mitandao hiyo.


ALBAM YA PILI

Katika mazungumzo na Gazeti
la IJUMAA, Harmo anasema kuwa, anatarajia kuachia albam yake ya pili iitwayo High School ambayo tayari imekamilika kila kitu, anachosubiri ni kuona ratiba za wasanii wenzake kwenye lebo yake kisha ataidondosha.


MAFANIKIO YA LEBO YA
KONDE GANG
Ibraah ndiye alikuwa msanii wa
kwanza kusainiwa Konde Gang na hadi sasa ina wasanii wengi kuliko Wasafi ambao ni Harmo mwenyewe, Ibraah, Anjella, Skales, Country Wizzy, Cheed na Killy ambao jumla yao ni saba.


UTAJIRI WA HARMO

Mtandao unaodili na kujua
thamani za wasanii Afrika Mashariki wa shoutmeceleb.com unamtaja Harmo mwenye umri wa miaka 30 kuwa na utajiri unaokadiriwa kufikia Dola za Kimarekani milioni moja (zaidi ya shilingi bilioni 2.3 za Kitanzania).Utajiri huo ni jumla ya mali zote alizonazo kuanzia mapato anayoyapata kupitia lebo yake ya muziki ya Konde Gang kutokana na shoo na mauzo ya muziki kwenye mitandao, umiliki wa kampuni ya kushuti video, gharama za kukodi nyumba na ofisi, ubalozi wa makampuni, matangazo, viwanja na magari anayomiliki kama Toyota Land Cruiser V8, Mercedes Benz na Audi.


ANAYEMPA JEURI

Kutokana na mafanikio
aliyopata Harmo nje ya Wasafi, kumekuwa na maneno mengi kuwa huwenda kuna mtu mzito anayempa jeuri.Hata hivyo, Uchunguzi wa Gazeti la IJUMAA umebaini kwamba, mbali na mameneja wake ambao ni Beauty Mmary almaarufu Mjerumani na Rajab Mchopa, mtu anayetajwa kumpa jeuri ni Dk Sebastian Ndege almaarufu Jembe ni Jembe.Katika uchunguzi huo, Jembe ni Jembe anatajwa kuwa ndiye ‘master mind architecture’ wa Harmo na mafanikio makubwa aliyoyapata.

 

Mtandao mmoja nchini Kenya, unamtaja Jembe ni Jembe kuwa ni bilionea anayemiliki kituo cha redio jijini Mwanza kinachoitwa Jembe FM, klabu ya usiku ya Jembe ni Jembe na Jembe Beach Resort (ufukwe wa kula bata) zote za jijini Mwanza. Pia wakati f’lani, Jembe ni Jembe alitajwa kuwa C.E.O wa Kampuni ya Bima ya Ndege Insurance na mmiliki wa Bendi ya Skylight na ni mtu anayependa maendeleo ya sanaa ya muziki.

 

Kabla ya hapo, alikuwa Mtangazaji wa Kipindi cha Njia Panda cha Clouds FM na kitaaluma ni daktari wa magonjwa ya binadamu.Katika moja ya intavyu zake, Jembe ni Jembe anasema; “Watanzania tujifunze kufurahia mafanikio ya wengine. Pale mwingine anapofanya jambo la kupiga hatua mbele kwenye mafanikio, tunatakiwa kumpongeza, kumtia moyo, kumfariji na kumuonesha kwamba inawezekana.“Siyo kutafuta kasoro ziko wapi na kumsemea jinsi atakavyofeli na maneno mengi ya kukatisha tamaa.”

STORI: WAANDISHI WETU, DAR | GPL

Leave A Reply