The House of Favourite Newspapers

Jide: Miaka 20 Kwenye Gemu Haikuwa Shughuli ya Kitoto!

0

JIDE amesikika kwenye ngoma za masikio ya wapenda Burudani Bongo yapata miaka 20 sasa.

Muziki huu wa Bongo Fleva umemfanya kupewa majina mengimengi kama Jide, Lady Jaydee, Binti Machozi, Binti Komando, Anakonda na mengine mengi, lakini jina lake kwenye kitambulisho cha Nida ni Judith Wambura Mbibo.

 

Kwa kipindi hicho chote tangu mwaka 2000, Jide amesikika na anasikika kwenye ngoma nyingi kubwa kama Machozi, Siri Yangu, Siwema, Usiusemee Moyo, Siku Hazigandi, Natamani Kuwa Malaika, Understand, Wanaume Kama Mabinti, Historia, Joto Hasira, Yahaya na nyingine kibao.

 

Anatajwa kuwa miongoni mwa wanamuziki wa kike waliofanya kolabo nyingi zaidi ndani na nje ya Bongo huku akitwaa tuzo kibao.

 

Kwa kutambua kazi kubwa aliyofanya Jide katika kutengeneza platform ya Bongo Fleva, ambayo sasa inaajiri maelfu ya watu, IJUMAA SHOWBIZ imepiga stori nyingi na Jide katika mahojiano maalum (exclusive) ili kujua amewezaje kudumu kwenye gemu kwa kipindi hicho chote;

IJUMAA SHOWBIZ: Kwanza Jide hongera kwa kutimiza miaka 20 kwenye gemu, safari ilikuwa ngumu kiasi gani na nini siri ya mafanikio?

 

JIDE: Kiukweli haikuwa shughuli ya kitoto! Changamoto kubwa ilikuwa ni namna nilivyopambana mwenyewe kujulikana sehemu tofautitofauti. Lakini naweza kusema ilinisaidia mno na kunifanya niwe jasiri nisiogope kupambana, hadi nikafikia mafanikio.

IJUMAA SHOWBIZ: Mastaa wengi tumewaona wakichora tatuu kwenye miili yao, je, wewe umechora na kama hujachora ni kwa nini?

 

JIDE: Kiukweli mimi mwili wangu sijawahi kuuchora tatuu na sitachora, kwani bila kuchora huwezi kuwa msanii? Sioni umuhimu wake ndiyo maana sijataka kufanya hivyo.

IJUMAA SHOWBIZ: Unatajwa kuwa miongoni mwa waasisi wa muziki huu wa Bongo Fleva ambao mmeweka ramani kwa wasanii, nini mtazamo wako?

 

JIDE: Nashukuru sana kwa sababu kuna wasanii wengi ambao waliniangalia mimi na kutamani wawe kama mimi kisha wakaingia kwenye muziki na hatimaye malengo yao yametimia. Kwa hiyo, ninajivunia sana kuwa mfano kwa wasanii wengine hasa wa kike baada ya kuniona nilichokifanya. Niliingia kwenye muziki nikiwa mtoto mdogo wa kike na nikafanikiwa.

 

Ninachoweza kuwaambia ni kwamba, waendelee kupigana kwa kuwa nilishaweka msingi mzuri wa mtoto wa kike na hatimaye na wao wanaaminiwa kama wasanii wazuri. Wapo wengi kama Vanessa Mdee (V-Money) na wengine.

 

IJUMAA SHOWBIZ: Umefanya kolabo kibao na wasanii wengi na zote zimefanya poa, ni nini siri ya mafanikio?

 

JIDE: Nimekuwa nikishirikiana nao na kazi inatoka vizuri. Hii ndiyo maana hata wao wananiamini, wanajua wakifanya kazi na mimi, lazima hiyo kazi itapokelewa vizuri na mashabiki wa muziki.

IJUMAA SHOWBIZ: Kwa nini wasanii wa kike kwenye muziki ni wachache?

 

JIDE: Huwenda ni kuogopa au kutokujiamini, lakini mimi ninawaambia wasiogope kwa sababu kile ambacho wanamuziki wa kiume wanachokifanya, hata wao wanaweza kukifanya. Kwa hiyo, kama kuna wanamuziki wa kike ambao walikuwa wanasita au kuogopa kuingia kwenye muziki, ninawashauri waingie na wapambane, hakuna kitu ambacho kimeumbwa kwa ajili ya watu fulani.

 

IJUMAA SHOWBIZ: Umewezaje kudumu kileleni mpaka leo na bado unafanya vizuri?

 

JIDE: Sibweteki eti kwa sababu mimi tayari nimekuwa maarufu, hivyo inatosha. Huwa mara nyingi ninakuwa mbunifu na ninawaza nifanye kitu gani ambacho kwa sasa kitaniweka karibu na mashabiki wangu.

 

Nikifanya hivyo, ninaendelea kuwapa kile ambacho mashabiki wanavutiwa nacho; yaani iko hivi, mtu unapofanya vizuri, usitosheke, endelea kufanya vizuri zaidi na zaidi, isifike mahali ukasema hapa sasa basi.

IJUMAA SHOWBIZ: Kwa wasanii wa kike Bongo, ni yupi ambaye unatamani awe kama Jide?

 

JIDE: Wasanii wapo wengi, kwa hiyo siwezi kumtaja mmoja wakati wanafanya vizuri na wameupeleka muziki wetu nje ya Bongo na ndiyo ndoto yangu ambayo nilikuwa nayo, ndiyo maana nilitoka na kwenda nchi mbalimbali kuimba hata kwa lugha yao wakati mwingine ili tuweze kutambulika.

 

Kuna baadhi ya nyimbo niliimba na wasanii wa Afrika Kusini, Rwanda na kwingineko ili kupeleka ujumbe kule kuwa, Tanzania nako kuna wasanii wanaofanya vizuri. Kusema msanii awe kama mimi, siwezi kwa sababu kila msanii ana vionjo vyake ambavyo mashabiki wake wanavikubali ndiyo maana wakaamua kumshabikia yeye.

 

IJUMAA SHOWBIZ: Mwaka 2020 una mpango wa kufanya na wanamuziki wa kimataifa na kama upo ni mwanamuziki gani?

JIDE: Ikifika

muda huo nitalizungumzia hilo.

 

IJUMAA SHOWBIZ: Malkia Karen ni mtoto ambaye amekuwa akiwa mikononi mwako, je, huwa unamsapoti na unamuona atafika wapi?

JIDE: Amekua akikiona kile ambacho nilikuwa ninakifanya, akakipenda na akaona kitamnufaisha, ndiyo maana na yeye akaamua kuwa mwanamuziki. Nasapoti sana kile anachokifanya na anajitahidi, ninamuona mbali sana na huwa namwambia ajitahidi sana kubuni vitu ambavyo mashabiki wanavi-hitaji.

Leave A Reply