The House of Favourite Newspapers

Jini Mauti-10

0

ILIPOISHIA
“Nasikia paka wananiita.”
“Paka?”
“Ndiyo mama.”
“Wapo wapi?”

“Huwasikii hao wanalia?”
“Hapana!”
“Mama! Nawasikia paka wakilia,” nilimwambia mama.
ENDELEA

Mama akasimama na kuelekea katika pembe ya nyuma, nikasikia akisema maneno kwa sauti ya chini kisha kusikia maneno machache aliyoongea kwa sauti kubwa.
“Ole wako umsumbue mwanangu, ama zako ama zangu,” niliyasikia maneno hayo toka kwa mama yangu, aliyaongea huku akiwa na hasira mno, akarudi kitandani na kulala.

Kuanzia kipindi hicho, zile sauti za paka zinakata, sikujua nini kiliendelea lakini kutokana na akili za kitoto, nikashukuru Mungu hivyo kulala. Kilichofuata, ghafla nikajikuta nikiwa kwenye kundi kubwa la watu, walikuwa watupu, nilipowaona, nao wakaniona, nikawa nawaangalia kwa zamu, cha kushangaza, nikamuona yule mwanamke mzee niliyemuona ndotoni, mwanamke aliyetaka kunipa mkoba ambao sikujua wa nini. NIKASHTUKA NA KUOGOPA.
****
Nilibaki nikitetemeka pale nilipokuwa, kila nilipowaangalia watu wale, niliyahofia maisha yangu kwani niliona nikiwa kwenye hatari kubwa. Kumbuka nilikuwa mdogo, miaka saba na nilikuwa nikisoma shule ya msingi darasa la kwanza.

Mwanamke yule mzee ambaye ndiye alikuwa bibi yangu akaanza kunifuata kule niliposimama, nilipoona akipiga hatua kunifuata, niliogopa sana, nilibaki nikitetemeka mno. Alionekana kuwa mwanamke hatari, macho yake yalikuwa makubwa.

Mkononi mwake alishika mkoba mkubwa, alinifuata huku uso wake ukiwa na tabasamu pana. Aliponifikia, akanikazia macho hali iliyonifanya nitetemeke zaidi, akaunyoosha mkono wake na kutaka kunipa mkoba ule.

“Mjukuu wangu! Wewe ndiye mrithi wangu niliyekusubiri kwa kipindi kirefu,” aliniambia bibi huku mkoba ule ukiwa umenifikia.
“Wewe ni nani?’ nilijipa ujasiri wa kuuliza.
“Mimi bibi yako.”
“Huo mkoba wa nini?”
“Wewe chukua.”

Nilikuwa muongeaji sana, tangu nilipokuwa mdogo, nilikuwa kama nilivyokuwa. Sikumuogopa mtu yeyote, nilipotaka kuzungumza jambo fulani, nilizungumza tena kwa haraka sana. Nilipofikishwa hapo, kiukweli niliogopa lakini baada ya kukaa kwa dakika fulani, nikayazoea mazingira ya hapo, hofu ikaanza kunitoka.

“Unakwenda kuwa malkia Pwani yote,” aliniambia bibi.
“Malkia wa nini?”
“Malkia wa uchawi.”

Aliponiambia hivyo tu, kuna hali niliisikia moyoni mwangu, sikujua ilitoka wapi, nilijisikia nikipata nguvu, nikiwa na imani kubwa juu ya kile alichoniambia, hapohapo, pasipo kulazimishwa nikanyoosha mkono wangu na kuuchukua mkoba ule, nikakabidhiwa uchawi na kuwa mrithi wa bibi yangu.

Nikaanza kusikia ngoma zikipigwa kwa shangwe, watu wakaanza kucheza huku wakishangilia, kitendo cha mrithi kupatikana kilimfurahisha kila mtu. Nilibaki nikiuangalia mkoba ule, sikujua ndani kulikuwa na nini lakini ulikuwa mzito.

Baada ya kukaa hapo kwa muda kama wa dakika ishirini, bibi akaniambia kwamba ilinipasa niondoke kurudi nyumbani na kesho angekuja kunichukua na kunileta hapo kwa ajili ya mafunzo, yaani nilitakiwa kufundishwa mambo mengi kuhusu uchawi ili niwe na nguvu.

Nilikubaliana naye na hivyo kuambiwa nifumbe macho, nikaze meno na nibane pumzi, nikafanya hivyo huku mkoba ukiwa mkononi mwangu, baada ya hapo, ghafla nikajikuta nikiwa kitandani, nilishtuka, kijasho kilikuwa kikinitoka, nilihisi joto kali sana.
“Kuna nini?’ aliniuliza mama, alikuwa ameshtuka kutoka usingizini.
“Mama…” nilimuita.

“Unasemaje?”
“Mkoba wangu upo wapi?”
“Nini?”
“Nilikuwa na mkoba, upo wapi?”
“Mkoba gani?”
“Nilipewa mkoba.”

“Na nani?” aliuliza kwa mshtuko.
“Mwanamke mzee! Upo wapi?” nilimuuliza mama.
Mama akaonekana kufahamu kilichotokea, nilipomwambia hivyo tu, akajua kwamba tayari bibi alinipa mkoba baada ya yeye kukataa, sasa mkoba ule aliamua kunipa mjukuu wake.

Kwa mara ya kwanza nikamuona mama yangu akianza kulia, sikujua kilichomliza ila mara kwa mara alikuwa akimtaja bibi kwamba ilikuwa ni lazima amkomeshe.

Leave A Reply