Jini Mauti-12
ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
“Thomas,” nilimuita mvulana huyo, alikuwa akiondoka kuelekea kwao, aliposikia nimemuita, akasimama na kugeuka nyuma, akaniangalia usoni.
“Davina…” alilitamka jina langu, nikashtuka kuona kumbe alikuwa akinifahamu.
SASA ENDELEA…
Nikamsogelea pale aliposimama, mapigo yangu ya moyo yakaanza kudunda kwa nguvu, kwa mbali kijasho chembamba kikaanza kunitoka, mwili wangu ulisisimka kupita kawaida. Thomas akaachia tabasamu pana, tabasamu lililouburuza vilivyo moyo wangu, nikajiona kama nimekutana na malaika.
Nilimwangalia Thomas usoni, sikuamini kama siku hiyo mvulana huyo alisimama mbele ya macho yangu, alionekana kuwa mzuri wa sura, alitoa tabasamu ambalo kwa hakika liliongeza uzuri wake wa sura na kunipagawisha mno.
Nilisimama naye karibu sana na hata kama ungekuwa unapita karibu yetu ungegundua kwamba wawili sisi tulikuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi. Nilimwangalia kwa macho yaliyoelezea hisia zangu, hisia za mapenzi ya dhati kutoka moyoni mwangu.
Sikuwa na cha kuongea, niliona kama maneno yote niliyotakiwa kuongea yalikwisha na hivyo kubaki kama bubu tu. Thomas alikuwa akinisikilizia, alitaka kusikia kile nilichotaka kumwambia mara baada ya kumuita.
“Davina….” aliniita huku akinishangaa, sauti yake ikanitoa kwenye lindi la mawazo.
“Abeee…”
“Unasemaje?” aliniuliza.
“Nani? Mimi? Hapana! Sina la kusema, nilitaka kukusalimia tu,” nilimwambia huku nikitetemeka.
Haikuwa kweli, nilikuwa na mengi ya kumwambia lakini niliogopa, sikujua angenichukuliaje, nilionekana msichana mdogo lakini nami nilikuwa mrembo kiasi fulani kutokana na wanaume wengi kunisifia, tena hasa nilivyokuwa nimejazia kwa nyuma.
Nilipomwambia hivyo, akashukuru kisha akaondoka, nyuma nilibaki nikimwangalia, nilijuta kwa nini sikumwambia kwamba ninampenda. Nakumbuka siku hiyo nilikuwa na mawazo mengi, kila nilipokaa, mawazo juu ya Thomas yaliutawala mtima wa moyo wangu.
Mama aliligundua hilo, alijaribu kunidadisi lakini alishindwa kujua niliwaza nini na aliponiuliza, sikumwambia ukweli, nilimdanganya tu kwa kumwambia kwamba nilikuwa sawa.
Ilipofika usiku, kama kawaida yangu nikachukua ungo wangu, nikajipaka unga maalum kwa ajili ya kuwangia kisha kupotea chumbani, tulikutana katika uwanja wetu wa kukutania kisha kuanza kupanga ni kitu gani tulitakiwa kufanya.
Nilikuwa malkia wa wachawi lakini kwa kipindi hicho sikutakiwa kuuchukua huo uongozi kwani bado sikuwa nimekomaa, niliendelea kufundishwa zaidi. Tulipopewa majukumu na bibi, tukatakiwa kuyafanyia kazi.
Kabla sijafanya kitu chochote kile, ilikuwa ni lazima nimfuate Thomas chumbani kwake, nimwangalie kwa muda ndipo niendelee na kazi nyingine. Wakati nafanya hivyo kila siku, kumbe bibi alikuwa akinifuatilia tu.
Hakuniambia kitu ila alijua kwamba nilikuwa kwenye mapenzi ya dhati na kijana huyo mwenye sura nzuri, alichokifanya kama kunisaidia ni kumchukua Thomas kila siku na kuniletea, nilimwangalia, niliporidhika, alimrudisha kwao.
“Ninataka uwe na furaha maisha yako yote,” aliniambia bibi.
“Nitashukuru sana.”
“Ila naomba uwe makini.”
“Kivipi bibi?”
“Kuna kitu tunakuwekea mwilini mwako.”
“Kitu gani?”
“Hutakiwi kukifahamu kwa sasa, ila hutakiwi kufanya mapenzi na mwanaume yeyote yule,” aliniambia bibi.
“Kwa nini?”
“Hakuna sababu. Usifanye mapenzi na mwanaume yeyote mpaka utakapoolewa,” aliniambia, tena kwa sauti ya kunisisitiza hasa.
“Sawa bibi,” nilimuitikia, sikujua alitaka kunipa kitu gani.
Baada ya siku kadhaa, bibi alinifuata na kunipa maji fulani, yalikuwa kama na mchanganyiko wa damu, akaniambia niyanywe kwani hayo ndiyo yalikuwa na kitu kile alichotaka kunipa, nikafanya hivyo.
Je, nini kitaendelea? Usikose wiki ijayo.