The House of Favourite Newspapers
gunners X

Jini Mauti-18

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
Nilikasirika mno, sikuweza kuvumilia, kweli nilikuwa mchawi lakini sikutaka mtu aniambie kwamba mimi ni mchawi hivyo nikaanza kumfuata. Alijua kwamba namfuata yeye, alichokifanya ni kusimama kibabe na kuanza kuniangalia…

“Agape sipendi ugomvi na yeyote yule, nani mchawi?” nilimuuliza, nilionekana kuwa na hasira mno.
“Wewe hapo,” alinijibu kijeuri.

“Una uhakika mimi mchawi? Umewahi kuniona nikikuroga?” nilimuuliza.
“Kwani nani asiyejua kwamba wewe mchawi? Hebu acha kuwaroga watu, mtoto mdogo unakuwa mchawi,” aliniambia Agape.

Nilikasirika sana lakini sikuwa na jinsi, nilichokifanya ni kugeuka nyuma na kuanza kuondoka mahali hapo huku nikilia. Moyoni niliumia mno, ni kweli nilikuwa mchawi lakini hakutakiwa mtu yeyote kuniita mimi mchawi.

Nikawa na hasira na Agape, sikutaka kumpenda hata mara moja, kila nilipomuona, moyo wangu uliwaka kwa hasira. Nilirudi nyumbani huku nikiwa kwenye hali ya hasira, hata kula sikula vizuri, nilichokifanya ni kwenda kulala.

Usiku niliamshwa na bibi, alikuja kunichukua kama kawaida yake. Nikajiandaa, nikachukua ungo wangu kisha kuondoka chumbani humo. Tulipofika kwenye uwanja wa kukutania, tayari siku hiyo kuliwekwa kiti kikubwa ambacho bibi alinitaka niende kukikalia, yaani ningeanza kazi kama malkia wa wachawi.

Nilipokikalia kiti kile, nikaanza kusikia nguvu za ajabu mwilini mwangu, kiti kile kilinipa nguvu ambazo sikuwahi kuzipata hapo kabla. Watu wote wakainamisha vichwa vyao chini kama kunipa heshima.

Kwa kuwa nilifahamu ratiba nzima, nikaanza kuwapa ratiba nzima juu ya mahali wapotakiwa kwenda kufanya kazi kwa usiku wa siku hiyo. Baada ya kuwaambia, wakaondoka na kwenda kwenye majukumu yao huku nikibaki peke yangu ambapo nilipanda kwenye ungo na kuanza kuelekea katika nyumba aliyokuwa akiishi Agape.

Sikuchukua muda mrefu, nikafika katika nyumba hiyo isiyokuwa na kinga yoyote ile, nikaanza kuelekea ndani mpaka katika chumba alichokuwa akilala. Nikaingia ndani kupitia pembe ya nyumba ile huku nikiwa mtupu kabisa.

Nilimuona Agape akiwa kitandani, alikuwa kwenye usingizi mzito, nilichokifanya ni kumfuata kisha kumuinua, nikamuweka kwenye ungo na kuondoka naye.

Sehemu ya kwanza kabisa kwenda naye ilikuwa Morogoro, kule kulikuwa na shamba kubwa la mchawi mwenzetu kikongwe, shamba la hekari kumi ambapo kila siku watu walikuwa wakichukuliwa kisha kulimishwa huko.

Nilipomfikisha Agape, kitu cha kwanza kabisa akapewa jembe hivyo kuanza kazi ya kulima shambani hapo huku akiwa na wenzake. Agape aliniona lakini hakunifahamu kabisa, alilima kwa takriban saa moja, tena kwa umbali mkubwa, alipomaliza, nikamchukua na kumrudisha nyumbani kwao.

Asubuhi nilipofika shuleni nilitaka kusikia kuhusu Agape, alikuwa akijisikiaje. Taarifa ambazo zilisambaa kwa rafiki zake wa darasa lake ni kwamba asingeweza kufika shule kwani alihisi viungo vyote kuuma huku akihisi kama kutaka kuumwa.
“Na ndiyo akome sasa,” nilijisemea.

Mudi, yule mvulana aliyekuwa akinitaka hakukata tamaa, kila siku ilikuwa ni lazima kuniambia kwamba alikuwa akinipenda sana na kutaka kuwa mpenzi wake. Sikumpenda lakini kutokana na ung’ang’anizi wake, nikajikuta nikianza kuvutiwa na mvulana huyo.

Maneno yake matamu, ahadi zake za kuvutia ikiwepo ya kunitunza na kunijali, nikajikuta nikiingia mikononi mwake. Kwa kipindi hicho sikukumbuka chochote kuhusu Thomas, nilimsahau kabisa.

“Nataka tukutane usiku,” aliniambia Mudi.
“Wapi?”
“Utaweza kuja kwenye ile Baa ya Mawele?”
“Ipi? Ile ya Sinza?”
“Ndiyo!”

“Mmmh!”
“Nini tena?”
“Wanafunzi na baa wapi na wapi?”
Itaendelea wiki ijayo.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/

Leave A Reply