Jini Mauti-22

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
Japokuwa mama alionekana kunitetea sana lakini alikuwa na wasiwasi mno, kila nilipomuona akiwa peke yake, mawazo yalimsonga na alionekana kufikiria mambo mengi sana. Ukweli ni kwamba mama alikuwa na wasiwasi mwingi, kila kitu kilichokuwa kikitokea kilimfanya kuwa na mawazo mno. Endelea…

“Davina…” aliniita.
“Abee mama.”
“Hebu niambie ukweli, wewe ni mchawi?” aliniuliza, alinikazia macho.
“Mimi?”

“Si ndiyo naongea nawe.”
“Hapana mama! Mimi si mchawi.”
“Kweli?”
“Ndiyo mama!”

“Na mbona kila unayefanya naye mapenzi anakufa?” aliniuliza.
“Mama! Mimi sijui.”
“Hapana! Lazima kuna kitu. Utakuwa umepewa mkoba wa uchawi ni lazima nikupeleke kanisani kuombewa,” aliniambia.
“Kwenda kanisani?”

“Ndiyo!”
“Sitaki, siwezi kwenda kanisani.”
“Kwa nini?”
“Basi tu.”

Sikutaka kwenda kanisani, nilikuwa na hofu kubwa kwani nilijua mambo ya kanisani yalikuwa vipi. Nilimkatalia mama, sikuwa radhi kuona nikienda kanisani kwani maisha yangu hayakuwa mazuri hata kidogo.

Sikwenda tena shule, nilimuomba baba anichukulie uhamisho na kweli akafanya hivyo, nikahamia katika Shule ya Sekondari ya Mbezi. Shule hiyo ilikuwa tofauti na Manzese, pale Manzese ilikuwa ni shule ya serikali lakini hii ilikuwa ya mtu binafsi.

Hapo kulikuwa na wasichana warembo walioonekana kuwa na maisha mazuri. Kuna wengine waliokuwa wakijiita majina mazuri ya Kizungu ilimradi kuwaonesha watu ni jinsi gani walikuwa warembo.
Mimi sikuwa msichana mrembo ila Mungu alinibariki kwa kunipa umbo zuri kwa nyuma, nilikuwa nimeumbika na kila nilipopita mbele ya wanaume ilikuwa ni lazima kunitazama kwa nyuma na kama ukinitazama ilikuwa ni lazima unitamani.

Nilipoingia shuleni hapo ilikuwa gumzo, wanaume wengi walinizungumzia, wengine wakawaambia wasichana wawaunganishie kwangu lakini sikuweza kukubaliana nao.

Bado nilikumbuka kilichotokea kwa Thomas na Mudi, sikutaka kitokee kwa mtu mwingine. Wanaume wengi walikuwa wakinifuata kila siku lakini sikutaka kukubaliana nao. Kidogo hapo Mbezi nilionekana kuwa na amani, hakukuwa na mtu aliyenisimanga kwa kuwa nilikuwa mchawi.

Kati ya wanaume wote waliokuwa wakinifuata, kulikuwa na watatu ambao walionesha uhitaji mkubwa wa kuwa nami, wa kwanza aliitwa Michael, huyu alikuwa mwanafunzi wa kidato cha nne, wa pili alikuwa Sifael, mwanafunzi wa kidato cha tatu kama mimi na mwingine alikuwa dereva bodaboda ambaye alikuwa akiegesha pikipiki yake katika eneo ambalo halikuwa mbali na shuleni hapo, huyo aliitwa Hemed.

Kama msichana nilionesha msimamo wangu, halikuwa jambo jepesi kunilaghai, mbali na hiyo nilikuwa na wasiwasi kwamba kama ningemkubali mwanaume yeyote basi ingekuwa ni lazima afe wakati wa kufanya mapenzi.

Kuroga sikuacha, bado niliendelea kama kawaida. Tulisafiri usiku na ungo, tulikwenda sehemu mbalimbali huku nikisimama kama kiongozi. Nilipata nafasi ya kula nyama za watu na kunywa damu zao na mambo mengine ya kishirikina.

Katika maisha yangu yote ya uchawi nilikuwa naogopa kwenda kwa watu wa makanisani ambao walisimama imara na Mungu. Wakati mwingine nilitoa hofu na kwenda kuwaroga watu hao majumbani mwao.

Huko, tulikuwa tukikutana na mambo ya ajabu mno ambayo yalitushangaza. Nakumbuka kuna siku tulipanga kwenda kumroga mchungaji wa kanisa moja la Praise And Worship la pale Mwenge, tulitaka tumpe uchovu wa kufika kanisani kwake kwani alikuwa akitusumbua sana.

Tulipofika katika eneo la nyumba yake, hatukukuta nyumba yoyote ile zaidi ya bahari iliyokuwa ikipiga mawimbi makubwa.

Itaendelea wiki ijayo.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/

 

Loading...

Toa comment