The House of Favourite Newspapers

Jini Mauti-23

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
Tulipofika katika eneo la nyumba yake, hatukukuta nyumba yoyote ile zaidi ya bahari iliyokuwa ikipiga mawimbi makubwa. Endelea…

Tulishangaa sana, tulihisi labda tulikuwa tumekosea njia, tuliondoka na kurudi tena usiku huohuo, tena kwa kuangalia vizuri njia, tulichokiona mara ya kwanza ndicho tulichokiona tena, bahari kubwa iliyokuwa ikipiga mawimbi makubwa.

Haikuwa hivyo tu, wakati mwingine tulipokuwa tukija, hatukukuta kitu chochote zaidi ya jangwa kubwa lililokuwa na mchanga wa moto. Matukio hayo yalitushangaza mno hivyo tukaachana na mambo ya kumfuatilia mchungaji huyo.

Sikutaka kuona mtu mwingine akifa tena kwa ajili yangu na ndiyo maana kila mwanaume aliyeniambia ukweli hakuweza kunipata. Hemed ndiye aliyeonekana kuwa msumbufu sana kwangu, kila nilipotoka shule ilikuwa ni lazima kunifuata na pikipiki yake, akinichukua na kunirudisha nyumbani, aliponifikisha, hakuwa akiondoka, alikuwa akizungumza na mimi kwanza ndiyo aondoke.

Alinisumbua sana. Simu yangu ya kwanza kutumia nilinunuliwa na yeye. Sikutaka kuichukua kwa mara ya kwanza lakini baada ya kunibembeleza sana, nikajikuta nikiichukua. Tulikuwa tukizungumza usiku, kuchati kama kawaida na aliendelea kuniambia kwamba alinipenda sana.

“Ninakupenda Davina,” aliniambia mara kwa mara simuni.
“Lakini bado nasoma.”
“Hakuna tatizo. Kwani nitakatisha masomo yako?”
“Hapana. Ila naogopa mimba.”

“Kwani si kuna kinga jamani, kuwa wangu Davina,” aliniambia kwa sauti ya kubembeleza.

“Hemedi.”
“Naam.”
“Najua unanipenda lakini naomba unipe muda jamani,” nilimwambia.
Hapo ndipo nilipoamini kwamba mwanaume anapoamua kumtafuta mwanamke huamua kwa nguvu zote. Sikupumua vizuri, Hemedi anapiga, sikutulia vizuri, Hemedi anatuma meseji, yaani alifanya mambo yote kuonyesha kwamba alikuwa akinipenda mno. Pamoja na hayo yote, wasiwasi wangu ulikuwa mmoja tu kwamba sikutaka kufanya naye mapenzi kwa kuwa sikutaka kuona akifariki dunia.
“Hemedi…”

“Naaam!”
“Sitaki ufe…”
“Hutaki nife?”

“Ndiyo! Nataka uishi mpaka kifo cha kawaida kitakapokukuta.”
“Unamaanisha nini?”
“Ukifanya mapenzi na mimi, utakufa.”
“Hahaha! Davina acha kunipiga saundi, au ndiyo unaninyima kijanja?” aliniuliza Hemedi huku akicheka kwenye simu.

“Hemedi! Sitaki ufe, naomba unielewe.”
“Na kama nikitaka kufa kwa ajili yako, kuna tatizo kwani?”
“Hemedi! Mbona wewe mwanaume unakuwa mbishi?”
“Nakuwa mbishi kwa sababu nakupenda. Davina, kwanza hebu naomba tukutane sehemu tuongee,” aliniambia.

“Wapi?”
“Popote pale.”
“Sema wewe.”
“Tukutane Sinza.”

“Sinza gani?”
“White Inn kwenye Bar ya Shika More.”
“Sawa.”
Kilichofuata ni kupanga mikakati ya kuonana. Tulipanga kuonana majira ya saa kumi na moja. Nilikuwa na mawazo mengi, nilijitahidi kwa nguvu zote kumkataa Hemedi lakini hakutaka kunielewa kabisa, kila wakati alikuwa akinisumbua.

Nilimwambia kwamba endapo angefanya mapenzi na mimi ilikuwa ni lazima afariki dunia lakini hakutaka kusikia kabisa na ndiyo kwanza aliniambia maneno mengi ya kimahaba kwamba alikuwa tayari kufa kwa ajili yangu.

Siku hiyo nilikubali kuonana naye lakini sikutaka kufanya naye mapenzi kabisa, yaani ilikuwa ni kukutana, kupiga stori kisha kila mtu kuondoka zake. Nilipofika katika Baa ya Shika More, nilimuona akiwa ametulia kwenye meza moja iliyokusanya viti vinne, aliponiona, akaanza kutoa tabasamu pana.

“Karibu mrembo,” alinikaribisha na kutulia kitini.

Itaendelea wiki ijayo.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/

Leave A Reply