Jini Mauti-5

ILIPOISHIA
Wakati akiwa amesimama tu, ghafla ngoma zikaachwa kupigwa, watu waliokuwa wakicheza wakaacha. Kwa mbali mbele yake akaonekana mwanamke mnene, alikuwa akitembea huku mkononi ameshika usingaENDELEA NAYO

Japokuwa alikuwa mbali lakini alipomwangalia vizuri alimgundua mwanamke yule, alikuwa bibi yangu, yaani mama yake, bi Mwamtumu. Kwanza mama hakuamini macho yake, alimwangalia vizuri mwanamke yule, alitaka kupata uhakika juu ya kile alichokuwa amekiona, hakuwa amemfananisha, alikuwa mama yake kweli.

“Mama!” alijikuta akisema huku akionekana kutokuamini.
Alimfahamu mama yake, alikuwa mtu wa dini, aliyeheshimika sana, kila wakati alikuwa mtu wa kutembea na Biblia huku akiimba nyimbo za dini, sasa ilikuwaje awe mahali pale, tena usiku kama ule? Kila alichojiuliza akakosa jibu.

“Yaani mama yangu mchawi? Haiwezekani,” alisema mama huku akitetemeka mno kwani sehemu ile haikuwa na amani kabisa.

Bibi akanyoosha mikono juu, wachawi wote wakainamisha vichwa vyao, walionekana kufurahia sana uwepo wao mahali pale, walimheshimu bibi na hapo ndipo mama alipogundua kwamba bibi alikuwa mkubwa wa wachawi.

“Leo ni siku ya kipekee, ni siku ambayo nitamkabidhi mtoto wangu huu mkoba wa kichawi ambao nilikabidhiwa na mama yangu,” alisema bibi, aliongea kwa sauti ndogo lakini cha kushangaza ilisikika mahali pale pote.

Akamwangalia mama, alibaki akitetemeka mno, aliogopa, alitamani kukimbia lakini akashindwa kufanya hivyo, mahali pale alipokuwepo hakukuonekana kama kulikuwa na njia yoyote ya kumfanya kukimbia.

“Njoo binti yangu! Leo ni siku ya maana sana kwangu na kwako pia,” alisema bibi.
Mama hakutaka kusogea kule alipoitwa, aligoma lakini kitu kilichoshangaza alijikuta akianza kwenda. Alikuwa kama mtu aliyevutwa kwenda kule alipokuwa bibi ambapo alitaka kumkabidhi mkoba wa kichawi.

“Siwezi, sitaki kuwa mchawi,” alisema mama kwa sauti, sauti iliyosikika sehemu yote mahali hapo, wachawi wote wakashtuka.
“Unasemaje?”

“Sitaki kuwa mchawi, siwezi kuwa mchawi, mimi siyo mchawiii,” alipiga kelele mama.
Uchawi ule wa kule Lushoto haukuweza kukabidhiwa hata kama haukuutaka, ilikuwa ni lazima wewe mwenyewe uukubali, uuchukue kwa mikono yako. Wachawi walishtuka, bibi akakunja sura, alionekana kuwa mwingi wa hasira, kile kilichokuwa kikitokea, hakukitegemea kabisa, hakutarajia kama mama angekataa kuchukua mkoba ule.

“Stella! Ni lazima uchukue mkoba huu! Wewe ndiye malkia mpya wa kuliongoza kundi hili,” alisema bibi yangu huku akimwangalia mama kwa hasira.
“Sitakiii…” alisema mama kwa sauti kubwa.
“Pumbavuuu….” alisema mama kwa hasira, hapohapo akaanza kutokwa na damu sehemu za siri kitu kilichomshangaza sana.
*****
Mama akashtuka kutoka usingizini, ilikuwa usiku mwingi, akaanza kutetemeka kwa woga uliochanganyikana na hofu aliyokuwa nayo. Kile kilichokuwa kimetokea, alijua kwamba ilikuwa ndoto mbaya na bibi hakuwa mchawi kama alivyokuwa ameona.

Kitu kilichomshtua ni kwamba alihisi kuwa na unyevuunyevu chini ya kitovu chake, hapohapo akaamua kuangalia kuona alikuwa na tatizo gani kwani mara ya kwanza alihisi alijikojolea, alivyojiangalia, hakuamini, aliona amelowa damu.
“Damu!” alisema kwa mshtuko.

Hali hiyo ilimshangaza sana, kile kilichokuwa kimetokea kilimfanya kuwa na hofu kubwa, alichokuwa akikikumbuka ni kwamba alikuwa akiota ndoto mbaya, ndoto kuhusu wachawi huku mama yake ambaye kila siku alimuona kuwa mtu wa dini akiwa kiongozi wa wachawi.

Kila kitu kilichotokea aliamini kwamba ilikuwa ndoto, sasa kwa nini damu ilimtoka kwenye ndoto ile ilimtoka katika maisha halisi? Kila alipojiuliza, alikosa jibu.

Alichokifanya ni kusimama na kuchukua kipande cha boksi kilichokuwa pembeni na kuanza kujifuta, ni kweli hakutakiwa kufanya hivyo kwa kuwa kile kipande cha boksi kilikuwa kichafu lakini kutokana na maisha ya shida aliyokuwa nayo, hakuwa na jinsi.

Damu haikukata, iliendelea kutoka, hakuwa akisikia maumivu lakini damu ilitoka mfululizo hali iliyoonekana kumuongezea hofu kubwa.

Loading...

Toa comment