The House of Favourite Newspapers

Jini Mauti-7

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
Hakulala usiku kucha, alikuwa mtu wa kulia tu. Sauti za paka zilikuwa zikisikika kila kona, aliogopa sana na sauti hizo ndizo zilizomfanya kutokulala kabisa. Hakukuwa na siku ambayo aliishi kwa hofu kubwa kama siku hiyo.
ENDELEA NAYO…

Mpaka inafika asubuhi, alikuwa macho, akainuka na kuanza kuondoka mahali hapo. Lengo lake siku hiyo lilikuwa ni kwenda Dar, hakutaka kuendelea kubaki Lushoto kwa kuamini kwamba kadiri ambavyo angeendelea kubaki huko basi bado angeendelea kufuatwafuatwa na bibi.

Mtihani mkubwa aliokutana nao asubuhi ya siku hiyo ulikuwa ni nauli tu, hakujua ni kwa jinsi gani angeweza kupata nauli na hatimaye kufika jijini Dar. Alitaka kuondoka kabisa Tanga, hakutaka hata kubaki kwani aliona ni lazima angeendelea kupata matatizo zaidi.

Alijua alikuwa mzuri, wanaume walivutiwa naye hivyo akaona hiyo ndiyo njia ya kuweza kupata nauli ya kuelekea jijini Dar. Bado wanaume waliendelea kumwangalia kwa matamanio, walimpenda sana kutokana na uzuri aliokuwa nao na hata mimba ile aliyokuwa nayo haikuwa ikionekana.

“Mambo mrembo!” Alimsalimia mwanaume mmoja.
“Salama! Shikamoo!’

“Aaghh! Unaninyima nini bwana! Unaitwa nani mrembo?”
“Naitwa Stellah!”
“Ni mkazi wa hapa Lushoto?”
“Ndiyo!”

“Safi sana! U mzuri mno, ningependa tukae sehemu tuzungumze.”
“Na nani?”
“Wewe!”
“Hapana! Nipo nasubiri basi.”
“Kwenda wapi?”

“Dar!”
“Kumbe tupo wote! Hata mimi naelekea hukohuko! Unaishi wapi huko?” aliuliza mwanaume huyo.

Mama akabaki kimya, alilisikia vilivyo swali aliloulizwa ila hakujua ajibu nini. Tangu amezaliwa mpaka kufikisha umri huo wa miaka kumi na saba hakuwahi kufika jijini Dar, alikuwa akisikia tu kwamba ilikuwa hivi na vile lakini maisha yake mpaka katika kipindi hicho hakuwa amefika huko.
“Mbona kimya?”

“Sijawahi kufika huko.”
“Duuh! Kwa hiyo hujui unaelekea wapi?”
“Sijui!”
“Basi nataka nikupeleke, naweza kuwa msaada mkubwa kwako,” alisema mwanaume huyo.

“Ila sina nauli!’
“Usijali, nitalipia mimi mwenyewe.”
“Nitashukuru!”

Si kwamba hakujua lengo la huyo mwanaume, alilifahamu vilivyo kwani hata macho aliyotumia kumwangalia, yalionesha wazi kwamba alikuwa akimpenda.
Mama akashukuru Mungu huku akijua wazi kwamba huko mbeleni alitakiwa kutoa shukrani, hakutaka kujali sana, alichokuwa akikitaka ni kuingia jijini Dar tu.

Asubuhi ya siku hiyo wakaanza safari, mwanaume yule alionekana kuwa mchangamfu mno, kila wakati alikuwa akizungumza yeye, kila kitu alichokuwa akikitaka mama, alimnunulia.

Walichukua saa kadhaa ndipo walipofika jijini Dar ambapo wakateremka na mama kubaki akizubaazubaa tu.
“Ulisema hauna ndugu?”
“Ndiyo!”

“Nitakutafutia chumba, upo tayari?”
“Nipo tayari!”
Mzee yule akaingia gharama, alimpenda sana mama, kwake alikuwa msichana mrembo, aliyempenda kwa mapenzi ya dhati. Hakutaka kuona akiondoka mikononi mwake, alichokifanya siku hiyo ni kumchukua na kumpeleka katika gesti moja iliyokuwa Mwananyamala.

Walipofika huko, mzee yule akaanza kumsabahi mama kitandani lakini akaonekana kuwa mkali kwa kuamini kwamba kama angekubali kulala naye, basi ndiyo ungekuwa mwisho wa mzee huyo kumsaidia.

“Siwezi kuacha kukusaidia, wewe nipe tu, nitakusaidia,” alisema mzee huyo.
“Siwezi! Mpaka unisaidie kwanza.”
“Haina noma.”

Mzee yule hakuwa na haraka, aliamini kwamba mama alikuwa wake hivyo muda wowote ule angelala naye.
Alichokifanya siku hiyo ni kumuachia kiasi fulani cha fedha kisha kuondoka zake.
Siku hiyo mama alikuwa na mawazo mno, hakuamini kama tayari alikuwa amefika jijini Dar, sehemu aliyoipenda mno.

Usiku ulipoingia, mama hakutaka kulala, aliogopa sana kwa kuwa alitishwa na uchawi aliokuwa nao bibi.

Leave A Reply