The House of Favourite Newspapers

Jini Mauti-9

0

wpid-arabic_girl_by_shonefluoartd5a442i1ILIPOISHIA
Mama alikuwa msiri, hakutaka kumwambia mzee yule kilichotokea, alikubali kubembelezeka na mwisho wa siku kuanza kuongea mambo mengine kabisa. Mzee yule aliyejitambulisha kwa jina la Abdallah alimwambia mama ukweli kwamba alimpenda mno na alitaka kuwa naye kimapenzi.

ENDELEA NAYO“Una mke?”
“Ndiyo! Ila ninakupenda, nipo tayari kwa lolote,” alijibu mzee Abdallah huku akionekana kumaanisha.
“Sawa! Nipangishie chumba na unifungulie biashara,” alisema mama.
“Hakuna tatizo.”

Mapenzi ni mapenzi tu, mzee Abdallah alitekwa sana na mama, akajikuta akifanya kama alivyoambiwa, baada ya siku tatu, mama akahamia katika chumba kimoja kilichokuwa Tandale kwa Mtogole huku akimfungulia biashara ya kuuza madera.

Mama alifurahi mno, katika kipindi chote hicho hakuwa amemwambia kama alikuwa mjamzito na hicho ndicho kitu kilichomuumiza sana kichwa chake. Alihisi kwamba kama angemwambia basi huo ndiyo ungekuwa mwisho wao.

Kitu kilichokuja akilini mwake ni kuitoa mimba ile. Hakutaka kujifikiria, akajipanga vilivyo, akapanga siku ya kwenda katika maabara ndogo kwa ajili ya kufanya kazi hiyo, siku hiyo ilipofika, akaelekea huko.

“Mimba haiwezi kutolewa hii,” alisema daktari.
“Kwa nini?”
“Imekaa ndivyo sivyo, kama nikisema niitoe, utakufa.”
“Unasemaje?”
“Huo ndiyo ukweli.”

Mama hakukaa sana mahali hapo, akaondoka na kuelekea katika maabara nyingine ambayo aliambiwa ilitumika sana kutoa mimba kwa wasichana, alipofika huko akaambiwa maneno yaleyale kwamba mimba isingeweza kutoka kutokana na namna ilivyokuwa tumboni, akakata tamaa, hakuwa na la kufanya, alichokifanya ni kuamua kumwambia mzee Abdallah.

“Hilo si tatizo, hata ungekuwa na watoto kumi, nimekupenda wewe, nalipenda boga, acha nipende na ua lake,” alisema mzee Abdallah.

Mama hakuamini, akamkumbatia mzee Abdallah na siku hiyo akampa mahaba motomoto. Huo ndiyo ukawa mwanzo wa uhusiano wao wa kimapenzi.

Tumbo la mama likaanza kuonekana, katika kipindi hicho ndiyo alikuwa na wakati mgumu, mauzauza yaliendelea huku kila siku bibi akimtokea na kumwambia ni lazima achukue mkoba wake wa uchawi kama yeye alivyouchukua kwa mama yake.

Mama aliendelea kukataa, kuna kipindi alikuwa radhi apate tatizo lolote lile, yaani hata kama kufa afe lakini si kukubali kuwa mchawi kama bibi alivyotaka awe.
Baada ya miezi tisa, mama akajifungua katika Hospitali ya Mwananyamala. Siku hiyo alipojisikia uchungu na kwenda hospitali, kulikuwa na paka mmoja aliyependa sana kwenda hospitali hapo.

Mama aliniambia kwamba kulikuwa na magazeti yaliandika kuhusu paka hao kwamba walikuwa wengi mno katika kipindi kile, acha niseme wazi kwamba hao walikuwa wachawi, yaani bibi alifika hospitali hapo na wenzake katika umbo la paka na kuanza kumfuatilia mama.

Mpaka mama anajifungua, paka wale waliendelea kuwepo. Si mama peke yake ambaye hakujua kama wale paka walikuwa wachawi bali hata watu wengine nao hawakulijua hilo kwani kwa kuwaangalia, walikuwa paka kwa asilimia mia moja.

Madaktari hawakuweza kugundua kitu chochote kile, kwao, walipowaangalia, waliwaona kuwa paka wa kawaida kabisa. Mama hakulala usiku, macho yake yalikuwa wazi na kama kulala, alilala mchana tu.

Alikaa kwa siku tatu hospitalini ndipo aliporuhusiwa na kurudi nyumbani. Mzee Abdallah alifurahia sana, maishani mwake, japokuwa alikuwa ameoa lakini mama alikuwa chaguo la moyo wake.

Hakutaka kurudi nyumbani kwake, mama alimpenda kwa mapenzi ya dhati. Wakati mwingine mzee Abdallah aligombana na mkewe baada ya kugundua kwamba alikuwa na mwanamke wa nje, mzee huyo hakujali, alimwambia mkewe kwamba ndiyo alikuwa na mwanamke na kamwe asingeweza kumuacha.

Mara kwa mara bibi alimtokea mama, aliendelea kumsisitiza kwamba ilikuwa ni lazima awe mchawi lakini mama aliendelea kuwa na msisitizo wake kwamba iwe isiwe hakutaka kuwa mchawi kabisa.

“Kama hautaki kuwa mchawi, binti yako atachukua hii mikoba,” alisema bibi huku akionekana kumaanisha alichomwambia mama.
“Hawezi kuwa mchawi, Davina hawezi kuwa mchawi.”
“Tutaona.”

Leave A Reply