The House of Favourite Newspapers

Jini Mtu-04

Nikiwa pale katika kile chumba pweke nimeegemea ukuta fikra zilinipeleka nyumbani, namwona mama yangu akiwa ni mwenye tabasamu pana siku alipopata matokeo yangu ya kidato cha nne,  ananipokea kwa bashasha kubwa, huku nikiwa nimechinjiwa jogoo kama pongezi kwangu, machozi ya furaha yanamtoka, mama yangu ananisogelea na kunishika mashavu yangu kwa viganja viwili vya mikono yake huku akinitizama kwa mapenzi makubwa anasema, umenitoa kimasomaso baba yangu, mungu akulinde na hila za shetwani ufike mbali zaidi ya hapa.

Sauti yake inakuwa na mwangwi kama kwamba yupo eneo kubwa lililo tupu.

   Nimetia tia ahadi nafsini ya kutokomeza umasikini humu ndani, siku moja utakuwa ni miongoni mwa wazazi wenye heshima  kubwa katika huu mji wa Kigoma, namjibu ilihali sauti ikiwa na mwangwi, moyoni nikiwa na ari ya kufanya vizuri zaidi katika masomo yangu,

   Natoka mama

   Unatoka?

   Ndio

  Wapi unaenda ilihali unajua leo ni siku yako,siku ya ushindi wa kufauru masomo yako baba?”

  Ni kweli mama”

  Sasa?..

  Naenda kwa Nasra nasema huku nikiwa na aibu machoni, naeguza uso pembeni, simtazami moja kwa moja, ila namwona pale alipo simama anashusha pumzi ndefu na kunitizama kwa kina huku tabasamu la kutia moyo likijitengeneza katika kinywa chake, kabla ya kupanda cheo na kuwa kicheko kidogo, anagundua mwanae nazidiwa na nguvu ya mapenzi.

   Ni nyakati nzuri kabisa katika maisha ya binadamu ndizo zinazobadilika na kuwa nyakati mbaya kabisa bila ya kutarajia.

  Kwanini unasema hivyo mama?  nilihoji mshangao ukiwa machoni mwangu na kutengeneza mikunjo mithili ya mkeka wa kinyamwezi katika paji la uso wangu.

 Ni kwamba kama mtu akiwa katika maisha mabovu hakuna kibovu zaidi kitakachomkuta zaidi ya hicho, lakini akiwa kwenye maisha mazuri ndio ataona mabadiliko pale hali hiyo itakapotoweka na kwa kawaida maisha mazuri huwa hayadumu.

Kabla sijahoji zaidi, ghafla  nilistuka kutoka katika njozi hiyo.

Nilistushwa na  yowe kubwa la mtu anae gumia maumivu ya kiwango cha juu, kutokea huko nje ambako kulikwa na wale wapishi wa kibinadamu,. “aaaagh mama nakaufaaaa!.uwiiii.!”  nilistuka mno baada ya kusikia ile sauti kali, na zaidi ilikuwa ni sauti ya mtu ninae mfahamu.!

Nilisimama huku nikitetemeka, mate mepesi yakijaa kinywani nikasogea pale dirishani. nikatupa jicho nje “ooooh! mungu wangu! nini hii yaillah!!.” nilijikuta nikipayuka kwa kile nilicho kiona tena dhidi ya mtu ninae mfahamu kabisa..

Alikuwa ni Amri Bakari mchezaji namba nane, kiungo mchezeshaji mwenye uwezo mkubwa wa kumiliki mpira awapo uwanjani, mwenyeji wa huko viunga vya mji wa Ujiji kilometa kadhaa kutoka mjini Kigoma.

Alikuwa amelazwa katika moja ya meza kubwa zilizo tumiwa na wale wapishi  watu, alikuwa hana nguo hata moja katika mwili wake.alikuwa amefungwa ya chuma katika kila mguu na mkono iliyo unganishwa na nondo zilizo kuwa pembeni mwa ukuta.

Kulikuuwa na watu wengine wa ajabu takribani kumi walio kuwa wameizunguka  ile meza,vichwani mwa wale watu walikuwa ni minywele  mingi iliyo jisokota sokota na kukaa hovyo kwa kukosa matunzo, huku katika nyuso zao juu kidogo ya kope za macho yao kulikuwa na michoro ya ajabu ajabu iliyo pinda pinda na kufanya sura zao ziwe ni zakutisha, walikuwa na makucha marefu!.  katika viganja vya mikono yao walikamata visu vikali.

Sikupata kusikia lugha waliyo kuwa wakizungumza wale watu wa ajabu.

Kweli leo nipo ushetanini,

Macho yangu yalishuhudia mtu akishika pande kubwa la nyama katika paja la kushoto  kisha akakata pande lile nyama halafu akalitia mdomoni na kulitafuna kama kwamba anakula sambusa.

Wakati huo huo bwana Amri Bakari alitoa sauti nyingne kali ya maumivu,  damu nyingi ziliruka kama mbuzi aliye katwa kichwa, hapo hapo watu wakasogeza midomo yao katika lile jeraha linalo vuja damu kwa kasi kisha wakawa wanakunywa ile damu!. Jamaaa alizidi kupiga makelele makali ya maumivu yasiyo mithilika.

Mtu analiwa akiwa hai!

Midomo na sura zao zilitapakaa  damu, ukijumlisha na yale masinzi yaliyo kuwa katika nyuso zao, basi walitisha vibaya mno.

Zoezi la kunyonya damu ya bakari halikuzidi dakika tano kwani waliweza kunywa kiasi cha damu ambacho kili lidhisha  nafsi zao.

Walikamata visu vyao kisha wale watu  wakiwa wamemzunguka Amri Bakari ambaye sasa, hakuwa na nguvu za kutosha kutokana na kutokwa na kiasi kingi cha damu, sasa walikata vipande vya nyama katika mwili wa Amri Bakari kisha wakawa wanatafuna hiyo minofu.

Amri alikuwa akipiga ukelele hafifu kila walipo kuwa wakinyofoa pande la nyama katika mwili wake, alikuwa akijisukasuka mkono na miguu yake katika minyororo iliyozidi kumbana na kumchuna kwa kumbana hadi ikawa anatokwa na damu.

“Ina…umaaaa..aiiiiii..mamaaa…maaa..munguuuu….weeeee.! Amri alilalama kwa tabu akiwa hana nguvu kabisa, alikuwa akipata maumivu makali mno.

Wale watu waliendelea kumnyofoa kwa pupa,walionekana kupenda minofu  ile kwani walimshambulia kwa pupa, damu zilitapakaa vibaya mno eneo lile.

Nilijikuta kwa mara nyingine nikijikojolea, mwili wangu ukitetemeka vibaya mno, nilitishaka kwa kiwango kikubwa sana, haya mambo nilizoe kuyaona katika zile filamu za wrong turn Sasa leo nilikuwa nikitokewa na maswahibu yale.

Hii ni mbaya zaidi, hawa viumbe wanakula watu!.yanii mtu anakula mtu mwenzie!. khaaaa hili ni tukio baya mno.

Katika watu walio wahi kufa kifo kibaya, kifo cha maumivu makali, basi Amri Bakari aliingia katika orodha hiyo, mwili wake ulibaki mifupa yenye damu nyingi, mtu mmoja alishika kisu kisha akashika korodani ambazo zilikuwa bado zinaningi’nia kisha akazikata kwa mara moja, akazitia katika chungu kilicho kuwa kinatokota mafuta yenye harufu kama mafuta ya kondoo ikawa anazikaanga kabla ya kuzitoa na kumkabidhi mama wa makamo ambaye alikuwa na mashavu makubwa yaliyo nenepeana kwa kutafuna nyama mbichi za binadamu wenzake, alizishambulia zile korodani kwa uchu mkubwa kwakweli!

Harufu ya damu iliingia ndani kabisa ya ubongo wangu na kunivuruga nilijikuta nikijitapikia  pale nilipo kuwepo hadi nikahisi utumbo unachomoka.

Nikiwa nimeinama pale chini najitapikia hovyo, mara  tena, nikasikia vitu vinakatwa  katwa nikajizoa na kusimama katika dirisha tena, sasa ile misukule ilikuwa ikimalizia kukatakata miguu ya Marehemu Bakari na kupasuapausa kabisa kichwa chake,  kisha vipande vikawa vinawekwa katika masifuria tayari kwa kuchemshwa supu!.

Nilishikwa na mashaka makubwa kwani picha niliyo iona ni kuwa hata mimi nitakufa kifo cha staili hiyo hiyo, kukatwa katwa viungo vya mwili mwangu ilihali nikiwa hai na kutafunwa nyama yangu kama sambusa, na hilo linatoa maana kuwa hata mabaki ya  mwili wangu hayataonekana asilani katika ulimwengu..

Supu ilichemshwa kwa dakika za kuhesabu,  kisha ikaepuliwa halafu wale viumbe wakaanza kuishambulia supu ile kama kwamba wanakula supu ya mbuzi.!

Machozi yalinibubujika kama maji niliogopa mno, hofu ya mauti ilitanda kifuani mwangu, sikuwa tayari kufa na ndoto zangu kuyeyuka  kirahisi namna ile, tena katika matukio yanayo kuja kama hadidhi za kubuni.

Nilikuwa ni mtu mwenye matarajio makubwa ndoto za kuwa na maisha bora, mchumba mwenye sura nzuri na shepu ya kuvutia nitakae zaa nae watoto wawili  tu wa kwanza ‘mwanamume’ wapili mwanamke.. pamoja na  jamii yangu iliyo jaa upendo sikuwa na sababu ya kukosa matarajio kama haya, lakini vyote hivi vinakuja kutoweka ghafla na kubaki kuwa ndoto tu..

Kimsingi nilitambua kuwa wachezaji wenzangu pia   nao walikuwa wameshikiliwa katika mazingira haya na wapo katika eneo fulani na pengine nao wanakutana na fikra kama zangu..Kitu nilicho kuwa sikijui ni wapi katika eneo hili wapo.

Wale viumbe wala watu, walipo maliza kumtafuna Bakari walianza kutawanyika na kutokomea gizani huku wakitoa sauti za ‘mibenzuko’ ya shibe.

Badae kidogo wakaja wale wapishi wa kibinadamu  wavaa makoti meupe na kofia za duara, wakawa wanafanya usafi katika meza ile iliyo tumika kwa chakula kwa wale viumbe, kusema ule  ukweli ndugu  somaji haya mambo we yasome tu katika hizo mnazo ziita hadithi, ama sijui nini vile Riwaya.. ambazo mnatungiwa na  hao wandishi wenu, ila siyo yakukute, yasikie tu yanasimuliwa kama hivi!.

Punde akili yangu ikiwa bado haijapata uimara dhabiti geti la chumba nilicho fungiwa  likafunguliwa wakaingia wale wapishi idadi yao wakiwa watano. Naaam, hapo nikaelewa muda wa kuchinjwa na nyama yangu kukatwa vipande vidogo vidogo kabla ya  kubanikwa kisha kufanyiwa uchunguzi wa ugonjwa wa anofobia umewadia.

   Siwezi kufa kizembe mimi  nilijiambia moyoni wakati huo mtu mmoja alikuwa amekwisha sogea hatua mbili mbele yangu,  nilimzibua ngumi kali ya taya nikasikia kitu kinafnya ‘kaaa’ akachia ukelele wa maumivu huku mikono yake akiipeleka shavuni mwake meno kadhaa akiwa hana tena, wale wenzake pia walitoa yowe dogo la mstuko huku wakiinama wakiwa wameziba  nyuso zao kwa viganja vyao  hawakutegemea kama ningeweza kutoa shambulio lile kalia kabisa.

Bila kukawiza hapo hapo nikaruka mzima mzima na kutua na kiwiko cha mngongo kwa jamaa wa pili aliye kuwa jirani, pigo lile lilimpeleka hadi chini huku akibweka kwa mstuko uliochanganyikana na maumivu ya ghafla, sikumlazia damu hapo hapo nilimshindilia teke jingine la ubavuni lililomfanya akeme kama amebanwa na uchungu wa  kujifungua,

“Pumbavu ninyi..kumbe mnayajua maumvu sasa vipi muwatafune wenzenu kama samaki ninyi [nikawatukania mama zao} wakati najiweka sawa kukabiliana na yule mtu wa tatu hapo hapo nikakutana na pigo kali kisogoni kwangu lililo nifanya nione nyota  nikajibwaga chini kama lumbesa la  mtumba.

“Unaleta ushujaa wa kwenye video hapa”  jamaa niliye mpa vitasa vya taya alinidhibiti, nilipokea mkong’oto wa nguvu hadi nikajuta kujitia u-james bond.

Nilifungwa minyororo kwa nguvu miguuni na mkononi kisha  nikabebwa juu juu hadi katika meza ya machinjio, yatari kwa kuchinjwa.

Chuki mbaya kabisa nikiona kwa jamaa niliye mngo’a meno mawili, nilijua  sasa naelekea kufa kifo cha maumivu pengine kuliko alicho kufa Bakari.

Pale katika meza nililazwa chali huku mikono na mguu yangu ikitanuliwa na kufungwa minyororo kwa nguvu hadi nikahisi miguu na mikono inataka  kukatika, damu zilikuwa zikitoka katika mikono na miguu yangu kutokana na kukazwa kwa ile minyororo.

“Mshenzi wewe unanitoa mimi meno..nipo huku huu mwaka wa ishirini na nne sijawahi kupigwa na kitoweo leo hii… ngoja nitakuelekeza namna ambavyo hutakiwi kuwa jeuli”

Jamaa alisema huku akiwa amesimama kando ya meza niliyo lazwa akinitizama kwa macho yake madogo kama kidonge, chuki mbaya ikiwa usoni mwake.

“Najua utanifanya kile ambacho hujawahi kufanya, ila nakusikitikia wewe usiyejua kwanini upo duniani na kwanini ulimwengu upo na katu swali hili huwezi kupata jibu lake kwakuwa unaishi mahala ambako huwezi kufundishwa kitu hiki”

“Kimyaa  we kisonoko wewe..unajua nini kuhusu dunia hayawani wewe” Jamaa alikoroma kwa ukali macho kayatoa mshipa ya kichwa imemsimama.

“Labda nikufundishe jambo  moja ambalo hujawahi kufundishwa au kuwaza  katika maisha yako..wewe ni binadamu tu tena  uliye tokana na tone dhaifu la manii tena lenye kunuka..na siku moja utarejea kwa mola wako ukiwa dhaifu..hiyo pumzi unayo ivuta leo  bure bure  yupo mwenye mamalaka nayo, sasa wewe endelea kukenua mapengo yako uonapo damu za wenzako zinamwagika na  viongo vyao  mnakula.. {nikamtukania mama yake} ipo siku mtalipa damu za wenzenu”

Yule jamaa alinitizama huku akitoa tabasamu baya la kejeli lililoacha mipengo yake nje.

Walinivua nguo zote nikabaki mtupu kabisa, visu vyao vikali vikiwa mikononi mwao tayari kwa kuanza kunikata kata nyama!.

Nilianza kuomba dua kimoyomoyo. oooh! Mola wangu,,nilifanya mengi maovu ya kukuasi katika ulimwengu, sasa tazama leo roho yangu inakuja mbele yako Yarabii!  nipokee kwa mikono ya upendo na unihifadhi katika eneo salama, niepushe na moto, nisamehe dhambi zangu, ni wewe pekee unasthili kuabudiwa na …” kabla sijamaliza toba yangu nilihisi eneo kubwa la kifuani  likikatwa na pande lanyama kumeguliwa. “AAAAAAAH”  nilipiga makelele, maumivu yakitambaa katika mwili wangu..wakati huo huo nikasikia ukelele mwingine wa ghafla  tena ukelele mkali ikitoka kwa yule jamaa bwana Mapengo.

“UUUUUWI!” ukelele ulisikika na eneo lote likatikisika kama vile, tetemeko la ardhi limepita karibu kabisa na eneo lile, hali ilitokea kwa  kwa nusu dakika.

Sikujali ukelele wake wala kile kilicho tokea, kilicho kuwa abongoni mwangu ni yale maumivu ya kukatwa pande la nyama, nililia mno macho nimeyafinya maumivu hayamithiliki.

Nilitegemea kupata jeraha jingine mahali popote wakati wowote katika mwili wangu kwa kumeguliwa mipande ya  minofu ya nyama.

Macho yangu yalifumbua  huku midomo yangu ikikosa umoja kabisa, nilitizama juu ambako kulikuwa na ukuta wa  ardhi ya pango..  meno nikiwa nimeyauma na kufanya mishipa ya kichwa kunisimama, kule juu hakuna nilicho ona zaidi ya  tandu nyingi za buibui zilizo vurugwa kutokana na mtikisiko ulio tokea dakika chache zilizo pita.

Mawenge mawenge ya hapa na pale yalinifanya  nisiweza kufikiri vizuri hata kidogo.

Nikaendelea kungoja kukatwa katwa maeneo mengine katika mwili wangu hadi kufa  lakini ajabu kukawa kimya!.

Nikajiweka tayari zaidi kwani akili yangu iliniambia wale jamaa kwakuwa wanachuki na mimi basi wanataka waniue kifo cha taratibu “ninyi misukule  just come and kill me right now {nikawatukania tena mama zao} nilizungumza kwa fadhaa nikiwa natweta vibaya mno.

Kimya.

Hapakuwa hata na chakara chakara yoyote.

“Ninyi mbwaa..agh! hata nikiwaita mbwa ntakuwa nimewakosea mbwa kwani mbwa ni  viumbe wa Mungu ninyi mashetaniii.! njooni mnile nyama upesi {nikawatukania bibi zao} ilikuwa ni kama nime patwa na wazimu..lakini haya niliyafanya ili kuwapandisha hasira wale watu ili kama kufa basi nife upesi kuliko maumivu yale makali kabisa ambayo haya vumiliki.

Lakini kuliendelea kuwa Kimya.

“We mr Mapengo hebu njoo ule nyama  yangu upesi fala wewe au unaniogopa pimbi wewe”

Kimya kwa mara nyingine tena!.

Nilipindisha shingo yangu nikatizama  kulia kwangu ambako alikuwa amesimama mr Mapengo, hapo nikakutani na tukio lillo nichanganya mno akili yangu.

Mbele yangu walikuwa wale wapishi wanne, nyuma yao walikuwa wale viumbe misukule  wakati kule mwisho kabisa walikuwepo wale viumbe wakubwa kabisa wenye kufanana na Sokwe.

Wote kwa pamoja walikuwa wamenisujudia kwa unyenyekevu wa hali ya juu!!.

“Nini hii maana yake sasa? Yaone yalivyo matahila” nilinongo’ona kwa sauti ya ukali, bado lile jeraha baya likizidi kunifanya mwili wangu uwake moto.

“Ooh!. Mungu wangu ndio wakati wa kubanikwa au?  fanya kitu kwa ajili yangu yarabii, niokoe mja wako” nilalama huku nikiwa nimekata tamaa kabisa.

Tendo la hawa viumbe kusujudu mbele yangu pengine ni moja ya taraibu zao hasa kama wanakuwa wanaandaa jambo fulani la kukuteketeza, hilo ndilo lililokaa akilini mwangu kwa wakati ule.

Lakini bado hali ya kusujudu mbele yangu iliendelea bila kuonekena dalili ya zoezi hilo kuisha muda mfupi ujao.

Nilitoa pumzi ndefu huku macho yangu yakirudi angani katika dari lenye tandu za buibui zilizo vurugika.

Lile jereha liliendelea kunipa wakati mgumu mno, minyororo iliyofungwa miguuni mwangu na mikononi, pia ilikuwa ikiniumiza vibaya mno.

“Hey!.niondoeni hapa ninyi viumbe wa ajabu,” sauti ndogo ya fadhaa ilinitoka, nikiwa nimekata tamaa ya kiwango cha mwisho kabisa, nilijua kuna jambo kubwa ambalo linaenda kutokea katika mwili wangu dhidi ya wale viumbe wa ajabu.

Nikiwa nimelala chali machozi mepesi yalinichuruzika kutoea pembeni mwa macho yangu na kuchuruzika hadi katika masikio yangu huku kamasi jepesi likiwa linichungulia katika pua zangu na kurudi  tena ndani.

“Kwachaaa”

Nilisikia kitu kina fyatuka katika minyororo na mara nikahisi uhuru katika mikono na miguu yangu iliyo kuwa imebanwa na minyororo,  nikaunyanyuka mkono taratibu kweli nikaona nilikuwa huru katika minyororo, nikageuza shingo yangu kwa wale viumbe nikaona bado wamesujudu mbele yangu katika hali ile ile ya utii!.

Nikapata mshangao kiasi, bado akili yangu ikawa tayari kupokea shambulio lolote kutoka kwa wale viumbe wenye nguvu kubwa ya kichawi.

Sikuwa na imani na hawa viumbe hata kidogo, kama inaweza kuachiwa ukakimbia na kijitenga nao umbali mrefu lakini akasimama na kunyoosha mkono wake na ukarefuka kama mpira kisha akakukamata na kukurudisha katika himaya yake vipi niwe na imani na viumbe hawa.

Nililitambua hilo lakini hata hivyo akili nyingine iliniambia kutokubali kufa kikondoo, niliamka nikaketi kitako  maumivu makali katika jeraha yakinitambaa, damu ilikuwa ikinichurizika vibaya mno.

Mara wale watu wakiwa katika hali ileile ya kusujudu wakaanza kutamka maneno ambayo sikuwahi kusikia lugha ile katika huu ulimwengu.  Ndio nalogwa hivyo mie niliwaza hofu ikiwa imetanda usoni mwangu macho yakiwa na mshangao mkubwa.

Nilijinyanyua pale mezani na kusimama chini huku bado nikiwa  sijajua nifanye nini nikawa narudi kinyume nyume mkono wangu wa kulia ukiwa katika jeraha kubwa la kisu lililokuwa livujisha damu kama bomba, hofu ikiwa kubwa mno.

Wale watu waliendelea kutamka yale maneno ya kichawi kwa muda kiasi na mara kukasikika  sauti nyingi zaidi ya  zile za wale watu waliokuwapo mahala pale sauti hizo pia zilikuwa zikitamka maneno kama haya waliokuwa wakiyatamka wale viumbe kwa pamoja.

Aisee!. niliogopa mno.

Nilizidi kurudi kinyume nyume nikjitenga na wale watu sauti nyingi  ziadi tena za maelfu ya watu ziliendelea kuzungumza yale maneno yasiyo eleweka na kadri nilivyo zidi kurudi nyuma na kujitenga na wale viumbe ndivyo zile sauti zilivyo zidi kupaza zaidi.

Hofu yangu ikazidi kuwa kuu zaidi nikageuka kwa ghafla na kutimua mbio mkono wangu ukiwa katika jeraha la tumboni nakimbia huku nikichechemea.

Hatua ya kwanza..yapili..ya tatu..ya nne.. ile nanyanyua mguu napiga hatua ya tano mara nikajikuta mguu wangu haufiki chini na hapo hapo nikajikuta mwili mzima unafuata mvuto wa mguu wangu, lilikuwa ni shimo, tena siyo shimo tu bali ni shimo kubwa na  refu kwenda chini..

Napolopomoka katika shimo refu kwenda chini. “Aaaaagh” nilipiga ukelele wa mshituko. “Vuuuuuuu” mvumo wa kuanguka ulivuma masikioni mwangu,  nilienda kasi chini pasina kufika chini,  akili yangu ikawa haielewi  jingine zaidi ya kutegemea kujibamiza ardhini na kupasuka vipande vipande, niliendelea kwenda chini kwa kasi ya ajabu kabisa.

Mara nilijikuta nikijipigiza  katika vitu vigumu mno katika lile shimo, bila shaka ilikuwa ni visiki na mawe ya pembeni mwa kuta za shimo.

“Pwaaaaaaaaaaaa” nilijibamiza chini, kishindo kikubwa kikasikika na mara hiyo hiyo nikahisi ubaridi ukitambaa mwilini mwangu na kisha unyevunyevu ukitawala kila sehemu nilijitahidi kufumbua macho na kuzirejesha fahamu lakini  ilikuwa vigumu sana.              

 

Je, nini kitaendelea?
Tukutane Alhamisi hapahapa.

Comments are closed.