The House of Favourite Newspapers

JINI MTU-12

0

“Hey,. Hey,. Hey..wee vipi mbona walala namna hiyo weye? kumekucha  haya amka upesi, haupo kwenu hapa”

Nilistushwa katika usingizi mzito, nafsi yangu ilikuwa imerejea katika mwili wake muda mfupi tu kabla ya kuamshwa, sikupata nafasi ya kupumzika kabisa, usiku wote nilimalizia huko mitaani niliko zua heka heka usiku ule huko mtaani.

“Saa ngapi sasa hivi shekh?” nilimuuliza yule shekh ambaye ndiye aliye niamsha.

“Saa kumi na moja na nusu, muda wa ibada sasa”

“Aagh! sasa mimi huwa siswali vipi uniamshe saa hizi?” nililalama,macho yakiwa na usingizi mzito.watu wachache katika bweni walikuwa wameamka kwa ajili ya kuswali huku wengine walikuwa wakikoroma kuumalizia usingizi wa asubuhi.

Eeh!. Kwakuwa Mungu mjomba wako? Hujamshwa ili uswali japo unaweza kuswali pia kwani siyo jambo baya,.swala inakufanya uwe karibu na muumba wako ndungu yangu,.any way nilitaka kukusanya vitabu vyote ambavyo jana vilichukuliwa kwa kusoma” alisema shekh.

Na hapo nikakumbuka jana nilichukua Riwaya ya Katalambula kwa kusoma, japo sikusoma hata kidogo pia hata kile kitabu sikurejesha kwa mtunza vitabu ambaye ndiye yule shekh.

Nilichukua kile kitabu nikamkabidhi yule shekh kisha nikaendelea kuuchapa usingizi, kuimalizia asubuhi ya siku mpya.******

Saa sita mchana kupitia runinga iliyo kuwa mule gerezani niliweza kuona  taarifa za kifo cha Hakimu Cymon Mlwilo {mzee Zakora} na famila yake.

Habari ile ilichukua hisia za wafungwa wengi mule gerezani kutokana na namna hakimu huyo alivyo kuwa akihusika na usikilizaji na hukumu wa kesi za wafungwa wengi mule gerezani.

Taarifa ile ya kifo cha kupigwa risasi kwa hakimu yule, ilpokewa kwa hisia mbili tofauti mule gerezani, wafungwa wengi walio pata hukumu kutoka kwa hakimu yule walifurahia kifo chake, huku wafungwa wengine wakipata majonzi na hofu ya kuchelewa kwa kesi zao ambazo zitalazimika kukabidhiwa hakimu mwingine ambaye atakuwa na kazi ya ziada ya kufautilia majalada mengi ya kesi ambazo ziliachwa na hayati Cymon Mlwilo au mzee Zakaora.

Kiasi cha masaa mawili nilifatwa na nyampala na kutakiwa kwenda katika ofisi za maafande mule gerezani.

Nikajua sasa mambo yameiva..nikajua lazma huyo atakuwa afande Mwita.{lafudhi ya kishashi}

Niliingia katika ofisi, macho yangu yakakutana ana kwa ana na afande mwita akiwa na yule afande mingine mwenye kujua kuzibua makofi.

Eeeeh! Kumekucha,. Niliwaza huku tukio la kule hospitalini la jana usiku likijirudia katika akili yangu, nikajua moja kwa moja nini kilicho waleta wale maafande mule gerezani.

Kabla sijazungumza lolote wale maafande walikuwa wamevaa sikilizio vya masikioni, sikujali mwonekano wao japo ulinishangaza kidogo, kilicho kuwa akilini mwangu ni vipi nitakabiliana na maswali kutoka kwa wale jamaa hasa afande Mwita ambaye alikuwa ni moja kati ya askari mwenye akili za ziada katika kazi yake.

“Vipi wewe Vegasi?” alinisalimu afande Mwita akinitizama usoni.

“Safi afande”. Nilijibu, na hapo walinitaka niketi chini kwa ajili ya mazungumzo muhimu na mimi.

“Vegasi ungehitaji ushindani nasi leo? Ilihali unajua tuko hapa kwa ajili ya kujua kile ulicho kifanya jana usiku kule hospitalini na kule nyumbani kwa mzee Cymoni Mlwilo?”

Ebwana wee!.

Ilikuwa ni kauli niliyo itegemea lakini ilinitisha vibaya mno, kilicho niogopesha zaidi hata maungo yangu kupata jasho, ni kauli ya afande Mwita kusema kuhusu uwepo wangu kwa hakimu Cymon Mlwilo ama mzee Zakora.

  Kajuaje huyu binadamu,.niliwaza  nikifikilia namna ya kumjibu yule mtu, lilikuwa ni tendo la haraka mno kabla sijajibu tayari afande Mwita akazidi kuikaanga nafsi yangu katika karai la mafuta ya moto

“Unajiuliza nimejuaje haya? Hilo siyo muhimu kwa sasa ila elewa kuwa tayari nisha jua na unahitaji utoe majibu.”

Ebwana wee!. Kweli jamaa walijipanga.leo afande mwita anaweza kusoma mawazo yangu.!

Kwa hakika mungu kumfanya binadamu kuwa kiongozi katika ulimwengu hakukosea, binadamu ni kiumbe mwenye akili na uwezo mkubwa mno kama akizitumia akili zao kwa utulivu, uwezo mzuri wa kufikili, na utekelezaji yakinifu.

“Sijui unacho ongea afande,”

“Siyo tabia nzuri kusema uongo ilihali unae mdanganya anajua kuwa unamdanganya hata wewe unajua kama mimi najua kuwa unanidanganya nimesomeka hapo Veagasi?”

  Huyu afande naye ni miongoni mwa jamii hii nini, Anajuaje ninacho kiwaza!. Wazo lilipita kichwani mwangu, na vile nilivyo kuwa nikifikilia hilo afande Mwita alikuwa akiweka vizuri visikilizio vya masikioni, na papo hapo akayajibu mawazo yangu.

“Inawezekana nikawa miongoni mwa jamii yako ndio maana najua nyendo zako na kile unacho kifikilia thus way niko hapa nipate ukweli kutoka kwao,”

Ujanja wote uliniingia mfukoni.

“Mimi sijui lolote wakuu aagh” nilijibu kwa fadhaa.

Wewe hukwenda hospitali jana?”

Hospitali kwa nani na kufanya nini,.na vipi niweze kufanya hilo ilihali niko gerezani?”

Nilisema kwa ukali macho nimeyatoa, niliona jamaa wakinywea kama mboga ya majani iliyo chemshwa, jamaa aliye kuwa akinipiga piga makofi leo hakudhubutu hata kidogo, kila mtu aliona mimi sikuwa binadamu wa kawida.

Na hapa niliona tulikuwa tunaogopana mimi, nilikuwa nikiwaogopa wale jamaa wasaa ule kwa kuweza kujua kile ninacho kiwaza, lakini hata wao walikuwa wakiniogopa mimi kwa kuona siyo binadamu wa kawaida kabisa.

“Hukumuibukia yule binti anaitwa Nasra kule hospitali wewe?” afande Mwita aliniuliza kwa upole huku macho yake yakiwa sawia na yangu.

“Ninacho jua Nasra amekufa, hayo mengine unayo sema ni mapya kwangu.”

“Unacheza na akili zetu wewe, huwezi kukwepa shutuma hizi Vegasi,watu wote wamekuona pale Wodini, haijatosha umemuibukia hakimu Cymoni  nyumbani kwake..

Alisema akionekana kupagawa  yule askari mwingine alimeza funda la mate macho yakiwa ya hofu kidogo.

“Unafikili unacho kizungumza kina sense katika fikra za watu makini afande?., ningekuwa mimi ndio wewe ningeacha kabisa kufutilia vitu ambavyo havina maana yoyote katika akili za watu makini”

Afande Mwita alichoka, kauli yangu ilizidi kukata maini, ni kauli hii niliyo isema kwake siku hii na ndiyo kauli hii hii aliyo wahi kuitamka kwa Nasra.

“laa! sasa nimepata jibu.,wewe ni muhusika wa matukio yote haya, ni wewe pia unae husika hata na kupotea kwa maiti ya Nasra kule hospitali” alisema afande Mwita kwa makini, jasho likimtoka katika maungo yake.

“Nalazimika kukushanga afande,vipi sasa unaweza kuamini hiki kizungumkuti kinacho endelea, hata ushindwe kuamini makosa na  ushindwe kumkamata huyu mkuuu wa wiliya anae jiita Hashim Aziz ama Saumya Kohil kama mtu niliye kwambia anahusika na baadhi ya matukio?”Nilisema.

Kauli yangu ilimbabaisha kiasi na ukweli fulani ulipenya katika akili yake, japo hakutaka kunionyesha lakini maneno yangu yalimwingia sawasawa.

“Vegasi wewe unajua siyo kiumbe wa kawida, usitake kuleta uchonganishi kwa maslahi yako binafsi” alisema afande Mwita kwa fadhaa. Sikumjibu nilibaki nikimtizama tu mtu yule mbishi.

Ukimya wa sekunde sita saba ukapita, kila mtu akiwaza kwa namna yake na katika ukimya ule  niliona jamaa kama akilekebisha kifaa chake cha masikioni, huku sura yake ikionekana kupata mstuko wa ghafla na akawa ni mtu aliye pata mfadhaiko kwa kiwango kikubwa.

Hatimae nikavunja ukimya.

“Wewe ni unajua awali nilivyo kuwa sielewi kile kinacho tokea katika maisha, umefanya mahojiano na mimi mengi unajua hilo afande, vipi mwanzo sikuweza kumjua huyu mtu na sasa niko humu ndani nimeweza kumjua huyu mtu, hujiulizi hilo afande?..Ushauri wangu ni rahisi sana..nitoe humu ndani mimi sihusiki na lolote…lakini kama utaendelea kunifuatilia..megi yatatokea yatakayo kufanya uwe tahila wa akili..maana utayachunguza na hauto jua lolote zaidi ya kukuchanganya tu akili”

“Kwa hiyo unakili kuhusika na sekeseke la jana huko nje Vegasi..na hata hili linalo tokea wasaa huu unahusika nalo pia wewe?”

“Wewe unaonaje Afande?” nilimrudishia swali katika hali ya majivuno.

Aliuma meno kwa hasira kisha akanirukia ngumi kali ya mdomo iliyo pasua mdomo wangu na kunifanya damu zilizo changanyika na udenda mwepesi unitoke, nikahisi uso wote unanifukuta kwa maumivu makali.

“Sheetwaini unaleta mikwara hapa.. na kwa taarifa yako yote uliyo yazungumza yapo katika kifaa hiki,” alisema akitoa kifaa cha kunasia sauti na kunionyesha kisha akakirejesha katika mfuko wa shati lake kisha akaendelea.

“Na huu utakuwa ushahidi wa kwanza kukutia hatiani kwa makosa unayo fanya huko mtani..mchawi wewe”

“Nilifikili naongea na watu makini wenye kisomo chake kumbe naongea na watu wenye elimu ya ngumbalu” nilisema  nikiwa najipangusa damu katika mdomo wangu, hasira zikiwa juu.

Kibao.

Uso ulizidi kuwaka moto huku nikiona maluwe luwe mbele yangu.

“Unafikili mimi ntakuogopa hata kama wewe u mwanga Vegasi?” alisema afande Mwita akiwa amenikwida shati na kunisogeza sentimita chache na uso wake.

“Siku..moja… hii..damu inayo mwagika hapa chini italipwa” nilisema huku nikikohoa na kohozi zito lililo tapakaa damu likinitoka mdomoni,na kumrukia usoni Afande Mwita.

Alinitwisha ndoo ya kichwa huku akinisindikiza na ngumi nyingine ya shingo kali ziadi. nilihisi shingo imeteguka, na giza liliingia machoni mwangu.

******

Huwa ni pale tu ninapo kuwa  sina ufahamu wa duniani basi hali hiyo inatosha kabisa kunisafirisha katika ulimwengu wa pili.******

 

Ulikuwa ni mchana unaelekea ukingoni kabla ya alasiri kuingia, nilikuwa mbele ya hospitali ya Lubengera nikiwa namung’unya kidonge ambacho kinanifanya nisiweze kunekana kwa macho ya kawaida, nilipiga hatua kuingia katika geti la kuingilia ndani bila kuonekana na walinzi.

Nilienda moja kwa moja hadi katika wodi aliyo kuwa amelazwa Nasra, ajabu sikumkuta, nikamsaka katika wodi zote mule ndani lakini wapi..

Hakuwepo.

Nilijaribu kutuliza akili yangu ili walau nifatilie pale yalipo mawazo yake.

Lakini wapi..palikuwa patupu.

Mmh! Atakuwa katika matatizo huyu!.

Nilifumba macho, nikanuia maneno ya kuwa mbele ya  Nasra.

Nilipo fumbua macho nilijikuta nipo katika mazingira ambayo sikuyategemea hata kidogo, moyo wangu ulilipuka kwa hofu, mate mepesi yalinijaa mdomoni, nilikuwa nyuma ya watu wengi, katika eneo la makabuli ya Nazareti.

  Nini kimemkuta Nasra

Nilijiwazia huku nikiwa siko tayari wala kutegemea kusikia kuwa kuna jambo baya limetokea kwa Nasra, kilicho nifanya niogope zaidi, watu wote pale walikuwa ni wanaume, sasa Nasra ni mwanamke vipi awe eneo lile ambalo liloneka kuna mazishi ya kislamu yanendelea pale!.

Nilipenya katikati  ya watu bila kuonekana, hadi eneo la mbele.

Moyo wangu ulipiga mkumbo, pale nilipo ona jeneza ndani yake kukiwa na maiti aliyo fugwa kama kifuko cha pipi, tayari kwa kufukiwa katika kabuli.

Nasra sikumwona!.

Shekh alikuwa akiombea dua maiti kwa ajili ya mazishi na watu wote walikuwa kimya, haikuchukua zaidi ya dakika moja kujua kuwa aliyekuwa amekufa ni  NASRA!.

Tumbo lilinichemaka, miguu iliniisha nguvu,nilibaki nimeganda kama sanamu la askari wa  posta, mate mepesi mdomoni yalinijaa, huku donge zito likinikaba kooni, hatimae nikajikuta naangua kilio kikubwa mno.

Nilikuwa nalia kwa sauti kubwa na uchungu wa hali ya juu, ila siyo miongoni mwa watu waliokuwa pale walio weza kusikia kilio changu.

Mwanamke aliye kuja katika maisha yangu kama malaika wa ukombozi, ndio alikuwa akiingizwa katika mwanandani tayari kwa kufukiwa na lundo kubwa la kifusi cha mchanga.

Niliona dunia nzima inafinyangwa finyangwa huku mimi nikiwa ndani yake, nilipata maumivu makali moyoni yasiyo mithilika, nilijitahidi kupigania masha ya Nasra kwa kiasi kikubwa, lakini binadamu wenzangu wamenikwamisha, hili liliniumiza mno.

Hatimae mwili wa mwanamke mrembo Nasra, ulitengenezewa vizuri mwana ndani, kisha watu wenye makoleo wakanza kuufukia mwili wake ndani ya nyumba yake ya milele.

Dakika kumi badae taswira ya tuta la kaburi ilitengenezwa, kisha viongozi wa dini waliomba dua na kutoa mawaidha mafupi kisha watu wakasambaa katika pilika zao za kila siku.

Maisha ya Nasra katika dunia yaliishia pale.

Nilibaki pale makabulini, mbele ya tuta la kabuli la Nasra nikiwa katika maumivu makali mno ya moyo nikiwa sijajua ni kitu gani kilitokea hadi Nasra apatwe na mauti ghafla vile, hii haikuwa siku yake ya kufa.

Sasa nini tena kimetokea?

Sikupata jibu.

Nilibaki pale kwa masaa mengi hadi giza likaingia, koo langu likiwa limekauka kwa kilio, bado sikujisikia kuondoka.

Wingu zito na jeusi la mvua lilitanda katika anga upepo ukisukuma takataka hovyo, giza likiwa kubwa, ngurumo kali za radi zilifoka kwa hasira, yapata saa mbili usiku, bado nilikuwa mbele ya kabuli la Nasra.

Kwa mtu wa kawaida isinge kuwa rahisi majira yale kuwa eneo lile la makabuli ambalo linasifikia kwa mambo ya kichawi na mizimu hatari.

Kiasi cha dakika za kuhesabu mvua kubwa ya upepo alianza kunyesha kwa nguvu,  huku giza likiwa zito vibaya mno, vichaka vilivyo kuwa katika eneo lile la makabuli vingeweza kukuogopesha, ila mimi sikuwa na hofu na kitu chochote.

Nilisimama nikazipiga hatua kuondoka eneo lile.

Nilichukua uelekeo wa Katubuka manguruweni ambako alikokuwa akiishi Nasra.

Giza liliendelea kuwa kubwa na mvua ilikuwa ikinyesha, hatua kama kumi nilihisi mwili ukinisisimka na miguu ikipata ganzi hata nikashindwa kupiga hatua nyingine niligeuza shingo yangu kutizama nyuma ya kabuli la Nasra., lahaula lakwataa!!!.

Nilipigwa na mshangao, huku nikivutwa na hisia kali ya hofu.

Watu wawawili walikuwa wakifukua kabuli la Nasra, kutokana na giza sikuweza kuona kwa uzuri nyuso.

Niliduwa kwa nukta kadhaa kisha nikasogea.

Hawakuweza kuniona.

Alikuwa ni mzee mtu mzima aliye onekana kama mganga wa kienyeji, huku mtu wa pili alikuwa ni binti wa miaka kati ya kumi na tisa.

Walikuwa kimya huku kila mmoja akikazana kufukua kabuli lile kwa makoleo, walifanya haraka haraka mno, nilibaki nikiwatizama kwa mshangao nisijue dhamila ya watu wale wawili.

Yule baba mzee mganga kila alivyo kuwa akichimba mchanga kwa koleo alikuwa akiimba nyimbo zake za kiganga, huku yule binti alionekan ni mwenye mashaka makubwa mno japo alikuwa akishiriki katika tendo lile.

Nilimtizama yule mganga katika macho yake, nikaingiza ufahamu wangu katika kichwa chake ili walau nipate kujua kile anacho kiwaza, nilisikia sauti kali na ngurumo za kutisha katika kichwa cha yule mzee mganga wa kienyeji, nilipo kuwa bado nipo ndani ya kichwa chake mara alisitisha kuchimba akanikazia macho pale nilipo simama, ikawa ni kama mwenye hisia ya kuwepo na kitu chenye uwezo mkubwa mbele yake.

Lakini hakuweza kuniona.

Aliongea vitu fulani vya kichawi, ambavyo vingeweza kunidhiru..

Lakini wapi.

Nguvu zile alizo zitumia zilikuwa ni nguvu dhaifu mno hakuna kilicho weza kunidhuru.

Alikuwa ni mtu aliye kuwa amepandwa na majini kichwani mwake.

Na majini yale yaliyo kuwa kichwani mwa yule mganga wa kienyeji yalikuwa ni majini yenye uwezo mdogo mno ukilinganisha na mimi.

Nilirejea katika ufahamu wake, bado wale majini waliendelea kunitolea ngurumo za vitisho, na wakati hayo yanaendelea ndani ya kichwa cha yule mganga..  alisitishwa kufukua mchanga wa kabuli, na alikuwa amekazia macho eneo nililo kuwa nimesimama bila kuniona, hakuwa yeye aliye kuwa akifanya yale bali na mashetani yake mule kichwani mwake.

“Haya upesi semeni mnataka nini katika kabuli hili?” nilisema kwa ukali kwa namna ile ya fikra.

Wale majini baada ya kuona uwezo wangu siyo wa kawida, walitii amri na kunieleza dhumuni lao katika kabuli lile. “Binti anataka kuwa ni mwenye mvuto na bahati, tunataka nyota ya maiti hii iliyo ndani ya kabuli hili  walinijibu kwa utii.

Yule mganga akiwa ameduwaa kama amenaswa na umeme, hata binti aliye kuwa akiendelea kufukua kile kifusi cha mchanga aliogopa zaidi na taratibu alisitisha ufukuaji ikawa anamshangaa yule mganga vile alivyo baki ameganda.

Mvua ilizidi kunyesha na giza lilikuwa kubwa ziaidi.

Niliwaamulu wale majini wasitishe zoezi lile mara moja.

Lakini mara kiiwiliwili cha mganga kilijigawa na kuwa pacha.

Na katika kiwiliwili kile cha pili kilianza kubadilika na kujitengeza  kiumbe kingine cha ajabu alikuwa ni mfano wa chura mkubwa wa miguu miwili, mwenye shingo na kichwa kama cha binadamu, alinitizama kwa jicho baya na akiwa tayari kwa makabiliano na mimi.

Alikuwa ni miongoni mwa majini, walio kuwa mwilini mwa yule mganga, jini mwenye kiburi, Yule kiumbe alizungumza maneno fulani hatari sana, akiwa ananitizama kwa macho yake makali yaliyo ng’aa mithili ya almasi.

Yalikuwa ni maneno ambayo kama huna uwezo wa ziada, punde sauti ile inapo penya masikioni mwako basi unapatwa na pigo kali mithili ya shoti ya umeme mwilini mwako, lakini ilikuwa tofauti kwangu, ile sauti haikuleta athali yoyote kwangu na hapo nilinyoosha mkono wangu na kushika shingo ya yule kiumbe, kisha kwa nguvu kubwa na za ajabu nilikibamiza kichwa chake juu ya kabuli moja  lililojengewa vigae, yule kiumbe alitoa yowe kubwa mithili ya ngurumo ya radi, hapo sauti kali ya mstuko kwa yule binti aliyekuwa na hofu ilimtoka, kwani aliambulia kusikia sauti kubwa na yakutisha pasina kuona ile sauti inapo tokea, na laiti kama engeweza kushuhudia kile kilicho kuwa kinaendelea mbele yake basi angeweza kupoteza fahamu kwa mstuko ambao angeupata.

Nilishika tena shingo ya yule kiumbe na kumnyonga kwa nguvu hadi akafa,.

Sauti kali ya hofu kutoka kwa majini wengine walio kuwa kichwani mwa yule mzee zilisikika.

Majini walikuwa wakitoka katika mwili wa yule mzee na kukimbia hovyo huku wakipiga kelele za mashaka makubwa, kwa hakika walikutana na kiumbe kisicho cha kawaida, waliniogopa vibaya mno, hata wakati wale majini wanatoka kichwani mwa yule mzee huku wakipiga makelele yule binti alishindwa kuvumilia kabisa baada ya kumwona mganga wake akiwa katika mashaka makubwa akisukwasukuwa huku na kule na majini waliokuwa wakitoka kichwani mwake, alitoka kasi eneo lile la makabuli huku akipiga makelele ya kuomba msaada na kutokomea gizani.

Kiasi cha majini takribani hamsini yaliyo kuwa mwilini mwa yule mzee mganga wa kienyeji yaliondoka yote,.

Yule mzee alianguka pale chini akiwa amepoteza fahamu, nilitizama mwili wa yule jini nae ulikuwa umetulia tuli akiwa maiti.

 

Je, nini kitaendelea?
Tukutane Jumamosi.

Leave A Reply