JINI MTU-2
“Hii nyumba ya mzee Ramadhani Nswima,. ni nyumba au mti wa mwembe huu!.nyumba gani mvua kidogo inavuja kama tuko nje!.nyumba gani bati lina matundu kibao kama tenga, nyumba wakati wa masika, roho zinakuwa juu juu, anajua kudai kodi tu ila ukarabati wa nyumba hajui..tutahama hapa aagh!..”
“Ta ta ta ta ta” matone ya mvua yalizidi kunidondokea hali iliyozidisha wahka ndani ya roho yangu.. ‘nyumba gani hii sasa!Ona hadi nashindwa kulala aagh”
“Ta ta ta ta” matone ya mvua yaliendelea kunilowanisha.
Sikuweza kuendelea kufumba macho. Kivivu nilifumbua macho yangu hapo maumivu makali kutokea kichwani yalinitambaa mwili wote na ndani ya nusu dakika baada ya kufumbua macho yangu niliona sikuwa chumbani mwangu nilikuwa chini ya kolongo nikiwa nimebanwa na vyuma vya gari lililopolomokea huko chini bondeni.
Mvua kubwa ya mawe na upepo ikiwa inanyesha kwa nguvu.
Hapo kumbukumbu zangu zikarejea upesi kila kitu kilichotokea dakika kadhaa kilipita kichwani mwangu, sasa hii siyo ndoto kama nilivyokuwa nikiota, huu ni ukweli halisi unaoendelea kutokea.
Nilijivuta kwa tabu nikijaribu kujinasua katika vyuma nilivyokuwa nimenasa mule ndani ya gari, maumivu ya kichwa yalizidi kunipa hali ngumu, kichwa kilikuwa kizito kama nimebeba gunia la mchanga.
Lakini hata hivyo kwa tabu nilijtahidi nikajinasua katika uvungu ule wa siti nilipokua nimenasa, gari likiwa limepinduka kimabavu, nikawa natambaa kwa shida kutafuta uwazi wa kutokea nje ya gari.
Katika hangaika ya huku na kule, mara nikapata kuona, tofauti ya kitu ambacho kabla sikuwa nimekifikilia.. ndani ya gari nilikuwa peke yangu, wenzangu hawakuwepo, hata mtu mmoja sikumwona mule garini.
“Weye mpemba weee!” niliita kwa tabu lakini sauti haikufika popote
“Mko wapi ninyi watu” niliendela kuhaha
Kimya.
“Omariii..” niliita tena kwa sauti ya juu kidogo.
Kimya kingine..
Sikujibiwa na sauti yoyote zaidi ya matone ya mvua yaliyokuwa yakidondoka na mkoromo hafifu wa gari.
Kwa bahati nikafanikiwa kupata uwazi mdogo wa dirisha lililokuwa limepasuka, hapo nikapenya na kutoka nje ya gari.
Bado maumivu mwilini mwangu yalizidi kunitambaa mwili wote na kunipa wakati mgumu mno.
Nilizunguka gari lote pale kolongoni lakini sikuona miili ya wenzangu.
Labda kuna msaada fulani ulipatikana kwa wenzangu wakati mimi nikiwa nimepoteza fahamu chini ya uvungu wa siti ya gari! Lakini ndio wapate msaada waniche peke yangu kule bondeni.
Niliwaza jambo hilo kichwani japo upande wa pili kiudadisi zaidi lilinipa mashaka kidogo, lakini nililazimika kuamini hivyo, yakuwa wenzangu walipata msaada fulani ndiyo maana hakuna ninaemwona eneo lile la tukio
Sasa nikawa nafanya jitihada za kupandisha kule chini ya lile kolongo ambapo nitatokea juu ya barabara huku nikiamini nitapata msaada japo ilikuwa ni usiku mwingi.
Mvua ilizidi kunyesha..
Ulikuwa ni usiku mbaya mno, giza lilikuwa limetanda, macho yangu yaliweza kuona mbele pale mwanga wa radi ulipomweka ngurumo kali za radi zilizidi kuufanya usiku huo uwe wa kuogopesha zaidi, kwa mujibu wa saa yangu ya mkononi ilikuwa ni saa tisa na nusu za usiku.
Sasa nikiwa kule chini ya kolongo nikawa napanda kuelekea juu kwa kushikilia mawe yaliyokuwa pembezoni mwa ukuta, kwa bahati mbaya sikuweza kufanikiwa kufika juu kwani mawe yalikuwa yamelowa na hayakuwa imara kila jiwe nililokuwa nikishika lilikuwa likimomonyoka.
Lakini pia haikuwa kazi rahisi kwani giza nalo lilinipa hali ngumu zaidi, sikuweza kuona wapi nishike na nipite wapi, vilevile si hilo tu hali dhaifu niliyokuwa nayo maumivu yaliyokuwa mwili mzima pia yalinidhoofisha sana.
Sasa nikawa natembea kurudi nyuma kule mwanzo wa maji yanapochuruzikia ni umbali wa mita kama arobaini ndipo kolongo linapoanzia.
Niliamini nikifika mwanzo wa kolongo itakuwa rahisi kutoka kule chini na kupata msaada, kwani kule mwinuko ni wa kawaida na pia eneo lile ni karibu na benki ambapo kwa majira yale, niliamini lazima nitapata msaada hata kutoka kwa walinzi wanaolinda maeneo yale nyakati zile.
Nianza kutembea kwa mwendo wa taratibu na tahadhari kubwa. Mvua iliendelea kunyesha kwa nguvu huku wingu jeusi likiwa limefunika anga na kufanya giza kubwa.
Ilikuwa ni mwendo wa mita kama ishirini na ushee hivi mwanga wa radi ukamulika, kwa sekunde za kuhesabu ikiwa ni kama vile mwanga wa kamera {flash light} mita kama tatu mbele yangu macho yangu yakapata kuona kitu..
Alikuwa ni mtu amelala kifudifudi..lakini sikuwa na uhakika moja kwa moja kama ni mtu.
Radi ikamulika tena, macho yangu yakawa makini zaidi pale mbele, hapo sikupata shaka tena kuelewa ni kitu gani macho yangu yaliona. Alikuwa ni mtu!
Akili yangu ilipata mawenge ghafla, kwani hisia thabiti nilizokuwa nazo kuwa ni lazima yule mtu pale ni miongoni mwa wezangu niliokuwa nao katika basi, sasa vipi tena awe eneo hili, mbali kabisa na eneo la ajali ilipotokea..!
Hii inakuwaje hii..
Hapa lile wazo langu la awali kuwa inawezekana mimi nilisahaulika kuokolewa katika ile ajali na hata kujikuta nipo peke yangu likajirudia kichwani mwangu na nikalifutilia mbali, kwani sikuona mantiki ya fikra hizo kwa sababu mbele yangu kuna mwili wa mtu, ambaye bila shaka ni miongoni mwa wahanga wa ajali ile, japo sikuwa na uhakika wa asilimia zote kuhusu hali yake, nilizipiga hatua kusogea pale ule mwili ulipo.
“Oyaaaa! Ma boy komredi” niliita kwa sauti ya juu kidogo majina ambayo wachezaji wote wa cklabu yetu huwa tunaitana hivyo.
Kimya..
Jamaa alibaki akiwa amelala chali hatikisiki wala hajibu
“Komredi vipi inakuwaje hii..washkaji wengine wapi af…” kabla sijamaliza sentesi yangu.. mwanga wa radi ukaangaza tena…”mamaaaaaaa!!.” nilipiga makelele kwa nguvu.
Nilitishika vibaya mno sijawahi kuona kile nilichokiona kabla, kwa zile sekunde tatu za mwanga wa radi zilitosha kunionyesha tukio baya mno, oooh! nilitetemeka, nguvu miguuni zikinitoka, nikajikuta naparamia mawe na kujikwaa kisha nikadondoka chini, midomo ikiwa wazi macho yamenitoka pima, niliogopa mno.
Ulikuwa ni mwili usiyo kuwa na uhai, pili alikuwa ni jamaa yangu Mpemba, rafiki mchezaji, tatu ambalo ndio kubwa ni namna kile nilichokiona kwake kilivyonipa kimuhemuhe, Mpemba alikuwa amepasuka kifua na tumbo huku mapafu, bandama na utumbo vikiwa vinaninging’inia..
Mwili wake ulikuwa umechanwachanwa na kitu chenye ncha kali na kutengeneza majeraha kama ya samaki wa kubanikwa wanavyotayarishwa, usoni alionekana ni mtu aliyekuwa katika taabu ya maumivu makali kabla ya kufa.
Nilijiburuza pale chini macho yangu yakiwa yanakodoa hovyo nahema kwa pupa huku sauti ya kilio nikiifinya kwa chini. nikijitenga mbali na mwili ule wa Mpemba. Hofu kuu ikiwa kifuani mwangu ikanambia, “hii si ajali hii..haya ni mauwaji,.na muuwaji hayuko mbali,” nilipagawa nikiweweseka na kihangaika kugeuka huku na kule.
Yaliyo mkuta mpemba kwa hakika hayakuwa ni matokeo ya ajali bali ni mauwaji ya kukusudia, tena inawezekana muuuwaji alidhamilia kabisa kufanya kitendo kile, na kama hofu yangu ilivyo nambia muuwaji hakuwa mbali eneo lile kwani majeraha yake yalikuwa bado mabichi kabisa.
Vilevile majeraha yale yalinionyesha namna muuwaji alivyo na roho ya kikatili.
Nikawa umbali fulani kutokea pale katika maiti ya mpemba, pembeni kabisa ya ukuta wa jabali, nikawa nimejikunyata kitako miguu nimeivuta sambamba na kifua changu, kamasi jembamba likinitoka huku jasho pia likiwa jingi mwilini mwangu ilihali mvua kubwa ya upepo ilikuwa ikinyesha
“Paaaaa” Sauti kali kama ya bomu ilisikika na kufanya mtikisiko eneo lote..”uwiiiii” nilipiga kelele za hofu huku nikijiziba uso wangu. sasa zamu yangu ya kupasuliwa tumbo na kifua na muuwaji imewadia…
Lakini kumbe ilikuwa ni ngurumo tu ya radi..ilifuatiwa na miale mikali kama umeme na matone ya mvua yakiongeza kasi.. lazma niondoke eneo hili upesi nikatoe taarifa.. nilijiambia moyoni nikajikaza kiume na kusimama wima sasa nikazipiga hatua za kasi huku nikipepesuka kama mlevi lakini ilikuwa ni hatua nne tu ndizo nilizo fanikiwa kuzipiga.
Wakati napiga hatua ya tano ndipo hapo nilipo hisi kuguswa na kitu kama kiganja cha mkono begani mwangu..”ayiiii” nilitoa sauti ya mshtuko nikiruka hatua moja mbele kisha nikageuka nyuma upesi.
Macho kwa macho na kiumbe wa ajabu.
Uwiiiiii,.nakufaaaaa, nilipiga makele punde macho yangu yalipo ona umbo la kiumbe yule.
Alikuwa ni kiumbe nisiye pata kumwona katika huu ulimwengu popo si popo, binadamu si binadamu wala nyani si nyani, lilikuwa ni jitu la miraba minne, lenye kiwili wili kama cha binadamu huku nyuma ya mgongo wake kukiwa na mabawa kama ya popo, kichwa na uso wake ulikuwa kama sokwe mzee, huku mwili mzima ukiwa na manyoya lukuki, hakuwa na nguo isipo kuwa mwili wake wote ulizingilwa na manyoya..’JINI’ ndio sifa pekee iliyo penyeza kichwani mwangu kwani ni majini ndio nimewahi kusikia na kusoma katika baaadhi ya vitabu kuwa ni viumbe wa kuogopesha kama huyu alioko mbele yangu.
“Toka..toka..toka” nilinong’ona kiwazimu, kana kwamba nafukuza ngedele shambani!. nikawa narudi nyuma hovyo, yule kiumbe alinitizama kwa macho yake mabaya yenye kufanana kabisa na mnyama aina ya kingkong niliye pata kumwona katika sinema, alinitizama kwa aina fulani ya mshangao! mimi pia nilishangaa mtazamo ule, labda aliona kitu kutoka kwangu ambacho hakutegemea.
Mkono wake ulio kuwa na nguvu aliunyoosha, na kwa maajabu mengine ule mkono ukawa unarefuka kama mpira kisha ukanikamata shingo kwa nguvu na kunivutia karibu yake.. “mamaaaaaa.maaaaaa nakufaaaa msaadaaa JINIIIIII!” nilipayuka hovyo, ila makelele yangu hayakufika umbali japo wa sentimita sitini,.
Nilikabwa kwa nguvu shingoni na yule kiumbe hadi nikawa sihemi..”ooh Yarabi niokoe mja wako mie” macho yalianza kuona giza dalili za kufa kwa kukabwa shingoni zikajidhihirisha, nikatepeta,. nguvu zikaniishia, yule kiumbe akaendelea kunikaba huku akishindilia kwenye shingo yangu vidole vyake vyenye makucha yaliyo komaa, hapo nikalegea nguvu zikanitoweka giza likafunika macho yangu*****
Je, nini kitaendelea?
Tukutane Jumamosi hapahapa
Comments are closed.