Jini Mweusi-43

Alijijengea heshima kubwa nchini Tanzania kutokana na utendaji kazi wake mkubwa aliokuwa akiufanya katika jeshi la polisi. Kutokana na umahiri wake, akapandishwa vyeo na mwisho wa siku akajikuta akiwa Kamanda Mkuu Kanda ya Dar es Salaam, DCP.

Heshima yake inakuwa kubwa, kila anayemuona anamheshimu. Pamoja na heshima aliyopewa, mwanaume huyu aliyeitwa Dickson alikuwa mtu mwenye sura mbaya ambapo huko shuleni kipindi cha nyuma aliitwa kwa jina la Zinjathropus, yaani binadamu wa zamani.

Hakuwa na mchumba, hakuwa na mpenzi, alichokifanya ni kuanza kununua machangudoa. Alifanikiwa sana, alilala na wengi. Alipofika Dar es Salaam, akaendelea kulala nao ila kwa kila ambaye alimuona sura yake na kumgundua, alimuua, alitaka suala la kununua machangudoa liwe siri maisha yake yote.

Upande wa pili kuna mwanamke mrembo aitwaye Pamela, msichana huyu mwenye umbo matata amefika jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kufanya kazi ya uchangudoa. Anapofika huko, kutokana na uzuri wake, anawapata wanaume wengi, anamtetemesha kila mtu, si wanaume tu, hata wanawake wenzake.

SONGA NAYO…

Polisi walikuwa kazini, hawakutaka kuona wakishindwa kwani kwa kile kilichokuwa kikiendelea hakikukubalika hata kidogo. Walipokea taarifa juu ya muuaji aliyekuwa akiwaua wanawake, hasa machangudoa waliokuwa wakijiuza mitaani.

Taarifa zile ziliwachanganya mno, hawakutaka kuona wakishindwa kirahisi namna ile, walichoamua kwa wakati huo ni kuanza kumtafuta muuaji kimyakimya, hawakutaka mtu yeyote afahamu ndiyo maana taarifa hizo hazikutakiwa kutoka nje ya makao makuu.

Walikwenda sehemu mbalimbali, tena pasipo taarifa na wakati mwingine nao wakijifanya wanunuaji wa machangudoa hao ili lengo lao la kumpata muuaji liweze kukamilika. Walijitahidi kupoteza muda wao lakini hawakuweza kufanikiwa kitu kilichowashangaza hata wao wenyewe.

Tetesi zile kwamba kulikuwa na mtu aliyekuwa akifanya mauaji zikaanza kusambaa kila kona, wanawake wakaogopa lakini kwa machangudoa hawakutaka kuacha kufanya kazi yao ya kujiuza kwani pasipo kufanya hivyo ilimaanisha kwamba hakuna kula.

Walijitolea, kama kufa, walikuwa tayari kufia kazini, hawakutaka kuacha hata mara moja. Polisi na watu wengine wa usalama waliwatahadharisha lakini hakukuwa na aliyewaelewa, kila siku ilikuwa ni lazima kwenda barabarani na kufanya biashara yao hiyo.

“Hivi hawa wanawake wanaelewa?” aliuliza polisi mmoja, alikuwa ndani ya gari na wenzake wawili, nje, kulikuwa na kundi kubwa la machangudoa waliokuwa mawindoni.

“Hawaelewi. Nahisi tunatakiwa kufanya jambo la ziada, vinginevyo huyo muuaji ataendelea kuwaua kila siku,” alisema polisi mwingine.

Hawakutaka kubaki mahali hapo, walichokifanya ni kuondoka huku wakiwa na mipango madhubuti kuhakikisha kwamba hakuna mwanamke mwingine atakayeuawa na muuaji huyo ambaye mpaka katika kipindi hicho hawakujua kama alikuwa mkuu wao wa kazi.

Vichwa vyao viliumwa, usiku na mchana walikuwa na kazi kubwa ya kumtafuta muuaji lakini hawakufanikiwa na hakukuwa na mtu aliyehisi kwamba muuaji huyo aliyekuwa akiwaua wanawake wengi alikuwa Kamanda Mkuu Kanda ya Dar es Salaam, Dickson.

*   *   *   *   *

Magreth hakuelewa kitu kilichotokea mpaka mtu aliyemzoea, mteja wake mkubwa, Dickson kutoonekana katika eneo alilokuwa akifanyia biashara yake, Sinza Mori. Alichanganyikiwa, alijaribu kumtafuta katika simu lakini mtu huyo hakuwa akipatikana na katika kipindi ambacho simu ilipatikana, hakuwa akipokea.

Magreth alichanganyikiwa mno, mteja wake huyo alikuwa kila kitu kwake, kila alipokuwa akienda kulala naye, alipata kiasi kikubwa cha fedha kuliko wateja wengine ambao walikuja na kuondoka, ambao hawakuwa wa kudumu kama alivyokuwa Dickson ambaye mpaka kipindi hicho hakujua kama mtu huyo alikuwa yule mkuu wa polisi mwenye sura mbaya.

“Wiki hii nitatembelea katika viwanja vyote, nitamfuma tu sehemu,” alijisemea Magreth, hakutaka kuchelewa, alichokifanya ni kuanza kutembea huku na kule, kwa siku hiyo ya kwanza, alitaka kwenda Ambiance, aliamini kwamba angeweza kumkuta huko, hivyo akaanza kutembea kutoka Mori mpaka Afrikasana.

*   *   *   *   *

Kwa kuwa tangu garini alimwambia Pamela kwamba hakupenda kufanya mapenzi katika sehemu yenye mwanga mkali, hata walipoingia ndani na Dickson kukataa kuwasha taa, Pamela hakushangaa kwani tayari alipewa taarifa kwamba mteja wake huyo hakuwa tayari kufanya mapenzi kwenye mwanga, alichokuwa akikitaka ni kuwa ndani ya chumba kilichokuwa na mwanga hafifu.

Kilichoendelea chumbani ni kushikana hapa na pale kisha kulala kitandani, kilichoendelea chumbani humo ni sauti za mahaba na kitanda kusikika. Walichukua muda wa masaa mawili ndipo Dickson alipoamua kujilaza pembeni, usingizi ukaanza kumnyemelea kwani alichoka mno, dakika tatu baadaye, usingizi mzito ukamchukua.

Alikuja kushtuka usingizini baada ya saa moja na nusu, mwanga mkali ulimpiga usoni, alipoiangalia saa yake, aligundua kwamba tayari ilikuwa ni saa nane usiku. Alishtuka, akajishika kichwani kuona kama alikuwa na kofia, hakuwa na kitu chochote kile hali iliyomfanya kuchanganyikiwa.

“Atakuwa ameniona?” alijiuliza Dickson huku akiwa amechanganyikiwa.

Akasikia maji yakimwagika kutoka bafuni, akajua kwamba Pamela alikwenda bafuni kuoga, alichokifanya ni kuchukua mkanda wake, akajiweka kitandani, alitaka kumuua msichana huyo kwa kumnyonga na mkanda ule kwani bado aliendelea kujisisitizia kwamba kila kitu kilichokuwa kikiendelea katika maisha yake hasa ya nyakati za usiku kiendelee kuwa siri.

Wala hazikupita dakika nyingi, mlango wa bafuni ukafunguliwa na Pamela kutoka huku akiwa kajifunga taulo tu na kulifanya umbo lake lililonona kuonekana vizuri machoni mwa Dickson.

Alipomuona mwanaume huyo, hakumshangaa wala hakushtuka, akamsogelea kitandani pale na kutulia, akamwangalia usoni Dickson, akamsogelea na kumpiga busu shavuni mwake.

“Umeamka saa ngapi?” aliuliza Pamela huku tabasamu kubwa likiwa usoni mwake.

“Nani? Mimi? Muda si mrefu. Mbona hushtuki?” aliuliza Dickson.

“Nishtuke kwa lipi?”

“Kuniona!”

“Kwani wewe hutaki kuonwa?”

“Nataka, lakini mbona hujashtuka?”

“Eehh! Nishtuke kwa lipi mpenzi?”

Dickson akashusha pumzi nzito, ule mkanda aliokuwa ameushikilia akauweka pembeni na kubaki akimwangalia msichana huyo.

Je, nini kitafuatia? Usikose riwaya hii ya kusisimua Alhamisi ijayo kwenye gazeti hilihili.

 

Toa comment