Jini Mweusi 50

Hali ya sintofahamu inazuka jijini Dar es Salaam kufuatia kupotea mfululizo kwa machangudoa katika mazingira ya kutatanisha. Taharuki kubwa inazuka kwani ndani ya kipindi kifupi tu, zaidi ya machangudoa kumi na moja wanapotea na hakuna anayejua walikopotelea.

Jambo hilo linasababisha jeshi la polisi kuingilia kati. Kinachozidi kuzua utata, wote wanapotea katika mazingira yanayofanana. Mwanaume mmoja asiyejulikana, aliyekuwa anatembelea gari la kifahari aina ya Volkswagen, aliyekuwa akienda eneo hilo usiku wa manane ndiye anayehusishwa na wote wanaopotea.

Upande wa pili, kijana aliyekuwa na mwonekano tofauti na binadamu wa kawaida, Dickson Maduhu au Zinja kama wenzake walivyokuwa wakimtania, amejiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Hisia kali za mapenzi zinasababisha kijana huyo aanze kutoka usiku na kwenda kutafuta machangudoa.  Hivyo baadaye anahamishiwa Dar es Salaam.

Mara baada ya kufanikiwa kuwa DCP, Dickson anajikuta akinogewa na penzi la changudoa mmoja aitwaye Pamela, umbo lake, ngozi vinamchanganya na kujikuta akianza kumganda pasipo kujua kwamba ukaribu wake na msichana huyo ungeweza kubadilisha kila kitu.

Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Huo ulikuwa mwanzo wa ukaribu baina ya Dickson na changudoa Pamela. Msichana huyo mrembo ambaye alivutia kila alipomwangalia aliliteka penzi la Dickson kiasi kwamba hata alipokuwa ofisini, hakuwa akifikiria kitu chochote kile zaidi ya penzi la msichana huyo mwenye umbo lenye mvuto.

Siku zikaendelea kukatika, hakukuwa na muda wa kutulia, saa mbili ofisini pasipo Pamela zilionekana kuwa nyingi, wakati mwingine alihakikisha anafanya kazi zake haraka iwezekanavyo kisha kurudi nyumbani ambapo alimpigia simu Pamela na kuja nyumbani kwake.

Wivu ukamjaa moyoni, wakati mwingine alimlazimisha msichana huyo alale nyumbani kwake kwani kila alipokuwa naye mbali, alihisi msichana huyo kulala na wanaume wengine kitu kilichouumiza mno moyo wake, kwa jinsi alivyokuwa na mapenzi mazito kwa Pamela, kuna kipindi alisahau kabisa kwamba msichana huyo alikuwa changudoa tu ambaye alilala na mwanaume yeyote aliyekuwa na pesa.

“Vipi tena?” aliuliza Pamela, ilikuwa mchana wa saa saba, alipigiwa simu na Dickson, haikuwa kawaida kitu hicho kutokea.

“Upo wapi?”

“Nipo nyumbani, kuna nini mpenzi?” aliuliza Pamela.

“Unaweza kuja mara moja?”

“Wapi?”

“Nyumbani kwangu.”

“Kwani haupo kazini?”

“Haujanijibu swali langu, unaweza kuja?”

“Naweza. Ila kuna nini?”

“Wewe njoo, wala usiogope,” alisema Dickson na simu kukatwa.

Kichwa chake kilichanganyikiwa mno, alichokitaka mahali hapo ni kumuona msichana huyo tu kwani hakukuwa na kitu alichokuwa akipenda kama kuwa karibu na Pamela.

Hakutaka kuendelea kukaa ofisini, alichokifanya ni kuondoka na kurudi nyumbani haraka ambapo wala hazikupita dakika nyingi, Pamela akafika, moja kwa moja akampeleka chumbani na kulala naye, hata kazi aliamua kuachana nayo kwa siku hiyo kwani penzi la Pamela lilimchanganya.

****

Magreth alibadilisha ratiba yake, kila siku akawa mtu wa kutembea katika viwanja mbalimbali vya machangudoa huku lengo lake likiwa ni kuona kama angefanikiwa kumpata mteja wake aliyemkimbia katika kipindi alichomhitaji sana.

Alizunguka na kuzunguka, tena wiki nzima mpaka alipofanikiwa kupata taarifa ambazo aliamini kwamba mtu aliyekuwa akizungumziwa alikuwa huyohuyo aliyekuwa akimhitaji.

“Umesema ana BMW nyeusi?” aliuliza changudoa mmoja.

“Ndiyo! Unamfahamu?”

“Kwa kweli sijawahi kumuona, ila huyo mteja anafika sana hapa kiwanjani,” alijibu changudoa huyo.

“Nitampata vipi?”

“Kwani ni nani kwako? Mumeo?”

“Hapana! Ila ninataka kuonana naye,” alisema changudoa huyo.

Jibu pekee alilopewa ni kwamba isingewezekana kuonana na mteja huyo kwani siku hizo hakuwa akifika sana kutokana na kulipata penzi la kudumu kutoka kwa msichana mrembo aliyetokea Arusha, Pamela.

Kitu alichokitaka Magreth ni kuonana na huyo Pamela kwa kuamini kwamba angepata taarifa nyingi juu ya mwanaume huyo na hata ikiwezekana kupafahamu kwake kwani hakukuwa na mteja ambaye alimpa fedha nyingi kama mwanaume huyo ambaye mpaka katika kipindi hicho hakujua alikuwa na sura gani.

Alipofanikiwa kuonana na Pamela, akajaribu kutengeneza urafiki naye, akaanza kumzoea, kila siku mchana akawa mtu wa kwenda kumtembelea, kwa kuwa Pamela hakuwa na marafiki wengi na pia hakuwa amelizoea sana jiji, akaupokea urafiki wa Magreth pasipo kujua msichana huyo alihitaji nini.

Mpaka siku ambayo Dickson alimpigia Pamela simu na kumuita nyumbani, Magreth alikuwa pamoja naye chumbani, alichokifanya ni kumuaga kwa lengo la kwenda huko.

“Ndiyo unakwenda kuonana naye?” aliuliza Magreth.

“Ndiyo! Unataka twende wote?” aliuliza Pamela huku akionekana dhahiri kwamba alikuwa akitania.

“Hahah! Kama inawezekana! Kwani hawezi kulala na wanawake wawili?” aliuliza Magreth, naye mwenyewe alionesha kutania.

Pamela hakujibu swali hilo zaidi ya kucheka kisha kuondoka nyumbani hapo. Kwa Magreth alionekana kuwa na uhakika kwamba mwanaume huyo ambaye Pamela alikwenda kuonana naye ndiye yule ambaye alifika sana katika kiwanja chake, Sinza Mori na kumnunua, lakini ghafla akapotea na hakurudi tena.

“Atakuwa ndiye yeye tu, ni lazima nimtafute, nipajue kwake na kumrudisha mikononi mwangu,” alisema Magreth pasipo kujua mtu huyo alikuwa nani.

Je, nini kitafuatia? Usikose riwaya hii ya kusisimua Alhamisi ijayo kwenye gazeti hilihili.

Loading...

Toa comment