The House of Favourite Newspapers

Jini Mweusi-52

0

Hali ya sintofahamu inazuka jijini Dar es Salaam kufuatia kupotea mfululizo kwa machangudoa katika mazingira ya kutatanisha. Taharuki kubwa inazuka kwani ndani ya kipindi kifupi tu, zaidi ya machangudoa kumi na moja wanapotea na hakuna anayejua walikopotelea.

Jambo hilo linasababisha jeshi la polisi kuingilia kati. Kinachozidi kuzua utata, wote wanapotea katika mazingira yanayofanana. Mwanaume mmoja asiyejulikana, aliyekuwa anatembelea gari la kifahari aina ya Volkswagen, aliyekuwa akienda eneo hilo usiku wa manane ndiye anayehusishwa na wote wanaopotea.

Upande wa pili, kijana aliyekuwa na mwonekano tofauti na binadamu wa kawaida, Dickson Maduhu au Zinja kama wenzake walivyokuwa wakimtania, amejiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Hisia kali za mapenzi zinasababisha kijana huyo aanze kutoka usiku na kwenda kutafuta machangudoa.  Hivyo baadaye anahamishiwa Dar es Salaam.

Mara baada ya kufanikiwa kuwa DCP, Dickson anajikuta akinogewa na penzi la changudoa mmoja aitwaye Pamela, umbo lake, ngozi vinamchanganya na kujikuta akianza kumganda pasipo kujua kwamba ukaribu wake na msichana huyo ungeweza kubadilisha kila kitu.

Je, nini kitafuatia?

SONGA NAYO…

Dickson hakuwa na hamu ya kufanya mapenzi na Magreth, alichokifikiria ni kumuua msichana huyo tu. Alimwangalia kitandani pale, kwa jinsi alivyojiachia, alijua fika kwamba endapo angeleta mchezo na kumuacha hai msichana huyo ilikuwa ni lazima aumbuke hapo baadaye.

Vitambaa vyake vilikuwa mikononi mwake, Magreth hakuwa na hofu yoyote ile, alijiweka vizuri pale kitandani huku akianza kuchojoa nguo moja baada ya nyingine.

“Come to me big dad…” (Njoo kwangu baba…) alisema Magreth kwa kutumia maneno ya mahaba. Dickson akakifikia kitanda kile na kumsogelea karibu.

Hakuwa na huruma, hiyo haikuwa mara ya kwanza kuua, alikwishawahi kufanya hivyo kabla hivyo hilo halikuwa tatizo kwake, kwa kasi ya ajabu, hapohapo akaviandaa vitambaa vile na kumfunika navyo Magreth puani na mdomoni.

Msichana huyo akaanza kukukuruka kitandani pale, akaanza kurusha mikono yake huku na kule kama mtu aliyekaribia kukata roho. Dickson hakutaka kumuacha, aliendelea kumkandamizia vitambaa vile. Kutokana na nguvu kubwa aliyokuwa nayo, Magreth akashindwa kujitoa mikononi mwa mwanaume huyo, ndani ya dakika mbili tu, nguvu zikaanza kumuisha na baada ya sekunde chache, akatulia kitandani hapo, pumzi ikakata na kufariki dunia.

“Haina jinsi Magreth…” alisema Dickson.

Alipohakikisha kwamba msichana huyo amekufa, akaelekea jikoni akachukua maji na kuyaweka kwenye bakuli kisha kurudi mle chumbani. Akachukua kitambaa na kuanza kuufuta mwili ule katika sehemu zote zilizokuwa na alama za vidole vyake.

Hakutaka kugundulika, alijua fika kwamba kama asingefanya hivyo basi ilikuwa ni lazima kugundulika kwani alama za vidole zingepimwa na uchunguzi kuanza kufanyika.

Alipoona kwamba amezifuta alama zote, akauzungushia shuka kisha kuubeba na kutoka nao nje. Alipofika nje, akaelekea katika eneo la maegesho ya magari yake, akaupakiza mwili ule ndani ya gari kisha kuondoka nao.

Hali ya hewa ilianza kubadilika, mawingu yalijikusanya angani na upepo kuanza kuvuma hali iliyoonesha kipindi kichache kijacho mvua kubwa ingeweza kunyesha.

Dickson akaenda stoo ambapo alichukua koleo na sururu kisha akaelekea ndani ya gari, kilichofuata ni kuanza safari ya kuelekea katika Msitu wa Pande huku lengo lake likiwa ni kwenda kuuzika mwili ule.

Mvua kubwa ikaanza kunyesha, Dickson hakurudi nyuma, alichotaka ni kumalizana na suala la mwili wa Magreth usiku huohuo. Kwa kuwa hakuwa na foleni usiku huo, alitumia dakika kumi tu, akaanza kuukaribia msitu huo.

“Ngoja niingie hapahapa,” alisema Dickson kisha kukata upande wa kushoto na kuingia ndani ya msitu huo.

Aliliendesha gari katika njia iliyokuwa na nyasi ndefu zilizolowanishwa na mvua iliyoendelea kunyesha. Alikwenda mbele zaidi huku taa za gari lake zikiwa full. Aliendesha mpaka alipofika katika sehemu iliyokuwa imezungukwa na miti mingi, akasimamisha gari na kuteremka huku mkononi akiwa na bunduki kwa ajili ya tahadhari.

Hakuutoa mwili kwanza, akachukua vifaa vyake na kuanza kuchimba shimo msituni pale. Hakutaka kujiamini kwamba alikuwa peke yake, muda mwingi aliangalia huku na kule ili kuona kama kulikuwa na mtu mwingine zaidi yake.

Alichukua dakika zaidi ya ishirini, shimo likakamilika, alichokifanya ni kurudi garini, akauchukua mwili wa Magreth na kwenda kuuingiza kwenye shimo lile kisha kuanza kuufukia.

****

“Unasemaje?”

“Tumeletewa taarifa ya mauaji!”

“Kutoka wapi?”

“Mbezi! Kuna taarifa kwamba inasemekana kuna mwili umefukiwa.”

“Wapi?”

“Kwenye msitu wa Pande!”

“Lini hiyo?”

“Jana usiku wakati mvua kubwa ilipokuwa ikinyesha,” ilisikika sauti ya polisi mmoja.

Polisi wa Kituo cha Polisi cha Mbezi walikuwa wakitoa taarifa kwa mkuu wa kituo hicho kwamba siku hiyo waliambiwa kwamba kulikuwa na taarifa zilizodai kwamba kuna mwili wa mtu ulikuwa umefukiwa msituni.

Taarifa hizo zikapokelewa hivyo polisi wanne waliokuwa na bunduki mikononi mwao, wakiwa ndani ya gari lao kuanza safari ya kuelekea huko walipoambiwa kwamba mwili wa mtu ulipozikwa.

Hawakuchukua dakika nyingi, wakafika katika eneo ambalo watu wengi waliingia msituni kwenda kushuhudia kile kilichokuwa kimetokea, nao wakaliingiza gari kuelekea huko.

Mbele, wakakutana na umati mkubwa wa watu ukiwa umekusanyika kwa staili ya kuzunguka kitu, walichokifanya ni kuwasogeza watu hao na kisha kuelekea pale ambapo kulionekana kama kuna kitu kimefukiwa, wakaanza kufukua.

“Kuna nini kwani?” alisikika mwanamke mmoja akiuliza.

“Nasikia kuna mwili umezikwa. Ila ni tetesi, sijui kama ni kweli,” alijibu mwanaume mmoja kwa sauti ya chini. Bado polisi waliendelea kulifukua shimo lile.

Leave A Reply