The House of Favourite Newspapers

Jini Mweusi – 66

0

Hali ya sintofahamu inazuka jijini Dar es Salaam, machangudoa wengi wanaanza kuuawa katika mazingira ya kutatanisha. Hakuna anayemjua muuaji, kila changudoa anayenunuliwa na mwanaume aliyekuwa kwenye gari aina ya Volkswagen nyeusi, anauawa kikatili.

Kila mmoja anaogopa, machangudoa wengine wanaacha kujiuza, wanajifungia vyumbani mwao ila kwa wengine ambao hawakuweza kuishi bila kufanya biashara hiyo, wanakwenda huko, bado wengine wanaendelea kuuawa.

Nyuma ya kila kitu, kuna mwanaume mmoja mwenye sura mbaya, tena akiwa ni Kamanda Mkuu wa Jeshi la Polisi Kanda ya Dar es Salaam, (DCP) Dickson ndiye ambaye anafanya mauaji hayo pasipo kugundulika. Kazi yake ni kununua machangudoa na yeyote atakayemgundua, humuua kikatili na kuondoka zake. Polisi wanachanganyikiwa, wanamtafuta muuaji, wanamkosa kwani anaonekana makini hasa kwenye kufuta alama za vidole vyake.

Hali ya hofu inaendelea kutanda jijini Dar es Salaam.

Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Haloo… naongea na Peter Msigwama?” aliuliza Kamanda Dickson.

“Ndiyo! Wewe nani? Mbona usiku-usiku?” aliuliza Peter.

“Unazungumza na Kamanda Dickson…”

“Kumbe ni wewe mkuu! Samahani sana..”

“Usijali. Upo wapi?”

“Nyumbani…”

“Nielekeze, nataka kuja mara moja kuonana nawe…” alisema Dickson.

Kamanda Dickson alikuwa akizungumza na mtu aliyejulikana kwa jina la Peter Msigwama. Huyu alikuwa kijana mwenye uwezo mkubwa wa kuchezea kompyuta na kufanya wizi katika benki mbalimbali nchini Tanzania.

Mwaka mmoja uliopita, zaidi ya shilingi bilioni tano ziliibwa kwa njia ya kitaalamu katika Benki ya Watu iliyokuwa jijini Dar es Salaam, mkurugenzi wa benki hiyo alichanganyikiwa, hakuamini kilichotokea hali iliyomfanya kuwaambia vijana wake wa kitengo cha IT (Information Technology) waliokuwa wakihusika na mambo ya kompyuta kuhakikisha wanajua akaunti fedha hizo zilipohamishiwa.

Haikuwa kazi ndogo, ilikuwa kazi kubwa ambayo usiku na mchana watu wa kitengo hicho cha IT walikesha lakini hawakuweza kujua mahali fedha zilipohamishiwa, mtu aliyezihamisha alionekana kuwa mtaalamu wa kucheza na system.

“Vipi?” aliuliza mkurugenzi huku akionekana kuchanganyikiwa.

“Bado hatujajua ni nani,” alijibu jamaa mmoja huku akionekana kuwa bize na kompyuta yake.

Mkurugenzi hakutaka kusubiri, kiasi cha fedha kilichoibwa kilikuwa kikubwa mno akawaita wataalamu wengine kwa ajili ya kumfanyia kazi hiyo lakini majibu yalikuwa yaleyale, hawakuweza kutambua fedha hizo zilikwenda wapi.

Mtu aliyekuwa ameiba fedha hizo alikuwa Peter, aliziiba akiwa chumbani kwake huku kompyuta ya mapajani ikiwa mbele yake. Uso wake ulikuwa kwenye tabasamu pana, baada ya kusoma IT, Mississippi nchini Marekani, alirudi Tanzania na zoezi lake la kwanza kabisa ili kuona kama aliiva ilikuwa ni kuiba fedha hizo.

Utaalamu alioutumia ulikuwa ni wa hali ya juu. Mkurugenzi na uongozi mzima wa Benki ya Watu ulichanganyikiwa, hawakujua nini cha kufanya, japokuwa walitoa taarifa polisi lakini hilo halikufanikiwa kugundua fedha hizo zilitolewa na kuwekwa kwenye akaunti ipi.

“Yaani hamjajua fedha zimewekwa kwenye akaunti ipi?” aliuliza polisi mmoja.

“Hatujajua mkuu! Tumesumbuka kwa siku tatu mfululizo, hatukupata kitu,” alijibu jamaa mmoja wa kitengo cha IT.

Simu ikapigwa nchini Afrika Kusini, wataalamu wengine wanne wakashuka na kupelekwa katika benki hiyo lakini bado hali ilikuwa tete. Baada ya wiki kupita, Peter akaamua kuzirudisha fedha hizo katika benki hiyo, mkurugenzi akashusha pumzi, hakuamini kilichotokea.

Polisi hawakutulia, vichwa vyao vilisumbuka, watu wakatumwa kwa ajili ya kufanya upelelezi kugundua ni nani aliyekuwa akihusika katika wizi huo, japokuwa fedha zilirudishwa lakini bado walitaka kumfahamu mtu huyo.

Baada ya siku kumi, wakafanikiwa kumkamata Peter ambaye aliwaambia marafiki zake mchezo aliocheza ambao walimsaliti kwa kutoa taarifa polisi kisiri. Polisi walipomuona Peter hawakuamini, alikuwa kijana mdogo mno lakini kichwa chake kilikuwa na mambo makubwa.

Kama serikali, haikutaka kumpoteza kijana kama Peter, walichokifanya ni kumchukua kwa ajili ya kuisaidia serikali huku akipewa sehemu muhimu kwa ajili ya kufanyia mambo yake tofauti na wizi.

Katika kipindi alichopelekwa katika kituo cha polisi ndipo alipokutana na Kamanda Dickson, hakuamini alipomuona Peter, alipoambiwa kwamba huyo ndiye aliyehusika katika wizi wa mabilioni ya fedha kwa kutumia kompyuta yake, alibaki akishangaa. Kwa kuwa namba ya kijana huyo iliachwa ofisini kwake akaamua kuichukua.

“Huyu atanisaidia…” alisema Dickson baada ya kumkumbuka Peter.

Alipompigia simu na kuzungumza naye, akaamua kumfuata Mikocheni alipokuwa akiishi. Japokuwa ilikuwa ni usiku sana lakini hakutaka kujali, ilikuwa ni lazima kuonana naye ili aweze kuzihamisha fedha zake na kuziweka katika akaunti yake ya siri.

“Unataka nikusaidie nini mkuu?” aliuliza Peter huku akitetemeka, alimuogopa sana kamanda huyo, hakuwa mtu mzuri hata mara moja.

“Nataka kuhamisha fedha zangu zote, kutoka kwenye akaunti hii, kwenda kwenye hii,” alisema Dickson huku akimuonesha akaunti zake.

“Hakuna tatizo…”

Peter hakutaka kuuliza maswali, alichokijua ni kwamba bado mtu huyo alikuwa kiongozi wa jeshi la polisi lakini ukweli ni kwamba aliamua kutoroka na kuacha kila kitu. Peter akaingia kazini, akachukua kompyuta yake ya mapajani na kuanza kufanya kazi hiyo. Japokuwa ilikuwa ni usiku sana, hakuchoka, hakusinzia, alitaka kuhakikisha fedha zinahamishwa, kweli baada ya dakika thelathini, kiasi chote cha shilingi milioni mia mbili kikahamishwa kwenda kwenye akaunti nyingine ya siri ya Dickson. Kamanda Dickson akakenua, sasa kilichobaki ni safari ya kuelekea katika Kisiwa cha Ukerewe kujificha.

Je, nini kitafuatia? Usikose riwaya hii ya kusisimua Alhamisi ijayo kwenye gazeti hilihili.

Leave A Reply