The House of Favourite Newspapers

Jini Mweusi – 67

2

Hali ya sintofahamu inazuka jijini Dar es Salaam, machangudoa wengi wanaanza kuuawa katika mazingira ya kutatanisha. Hakuna anayemjua muuaji, kila changudoa anayenunuliwa na mwanaume aliyekuwa kwenye gari aina ya Volkswagen nyeusi, anauawa kikatili.

Kila mmoja anaogopa, machangudoa wengine wanaacha kujiuza, wanajifungia vyumbani mwao, ila kwa wengine ambao hawakuweza kuishi bila kufanya biashara hiyo, wanakwenda huko, bado wengine wanaendelea kuuawa.

Aliyekuwa akiua wanawake hao ni Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda ya Dar es Salaam, Dickson. Aliwaua kwa siri lakini baada ya kipindi fulani kupita, akagundulika na hivyo kuanza kutafutwa.

Kwa amehamishiwa fedha zake zote katika akaunti yake ya siri, hakuna aliyejua fedha zimehamishwaje kwani aliyefanya kazi hiyo ni mtaalamu sana katika mambo ya kompyuta, anachokifanya ni kuanza safari ya kuelekea Mwanza.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Usiku ambao taarifa zilitolewa kwamba Kamanda Dickson ndiye aliyekuwa akifanya mauaji na hivyo ilitakiwa atafutwe mpaka apatikane, polisi hawakutaka kuchelewa, walichokifanya kilikuwa ni kuimarisha ulinzi katika kila kona kuhakikisha kwamba mtu huyo havuki kwenda nje ya Jiji la Dar es Salaam.

Walichokifanya ni kuimarisha ulinzi mkali katika bandari zote kuhakikisha mtu huyo haondoki kuelekea Zanzibar au katika kisiwa chochote kile. Ulinzi wao haukuishia huko tu, pia wakahakikisha wanaimarisha ulinzi Kibamba ambapo walijua fika kwamba mtu huyo anaweza kutoroka na kuelekea katika mkoa wowote.

Ulinzi uliwekwa kila sehemu, hawakutaka kusikia mtu huyo akiondoka jijini Dar es Salaam kwenda sehemu yoyote ile kwani hata viwanja vya ndege, kote huku walihakikisha ulinzi unakuwa mkubwa, polisi wengi waliokuwa na bunduki na mbwa mikononi mwao walisimama imara wakimsubiri.

Wakati hao wakiwa wameweka ulinzi kila kona, Kamanda Dickson ndiyo kwanza alikuwa akitoka nyumbani kwa Peter ambapo tayari alikamilisha suala zima la uhamishaji fedha alilokuwa amelitaka lifanyike haraka iwezekanavyo.

Hakutaka kurudi nyumbani kwake, mpango wake mzima ulikuwa ni kutoroka na kuelekea katika Kisiwa cha Ukerewe ambapo aliamini kwamba angeishi kwa raha mustarehe huku akila maisha mpaka hapo atakapokufa. Akaondoka na kuelekea barabarani, kofia kubwa ilikuwa kichwani mwake kama kawaida, alipoiona Bajaj moja ikija kule alipokuwa, akaisimamisha.

“Hapa mpaka Kimara elfu ishirini…” alisema dereva Bajaj.
“Sawa! Twende…”
Safari ya kuelekea Kimara ikaanza mara moja. Njiani, alikuwa na mawazo mengi lakini hakutaka kujali sana, wakati huo haukuwa wa majuto tena, ulikuwa ni muda wa kufanya mambo mengine na kuangalia maisha yake ya mbele.

Kutoka hapo Mikocheni B mpaka Kimara walichukua dakika ishirini tu kufika, akamlipa dereva kiasi cha fedha alichokihitaji kisha kukaa pembezoni mwa barabara akisubiri magari makubwa ya mizigo.

Muda ulikuwa umekwenda sana, ilikuwa ni saa nane kasoro usiku, kulikuwa na baridi kali, lakini hakutaka kujali, kitu pekee alichokuwa akikihitaji ni kulikimbia Jiji la Dar es Salaam ambalo lilionekana kuwa la hatari katika maisha yake kipindi hicho.

Mawazo juu ya msichana Pamella yakaanza kurudi tena kichwani mwake, alimkumbuka msichana huyo mrembo, alijitahidi kumuonesha mapenzi ya dhati lakini kitu kilichotokea hakujua msichana huyo angelichukuliaje suala lake la kutafutwa baada ya kuwaua wanawake wengi.

“Hivi akijua itakuwaje?” alijiuliza lakini hakupata jibu lolote lile.
Wakati akiwaza hayo, akakumbuka kwamba alikuwa na namba yake ya simu hivyo alichokifanya ni kuichukua simu yake na kuanza kulitafuta jina la Pamella. Alichokuwa akikitaka ni kuzungumza naye, kumjulia hali na pia kumuomba msamaha kwa mabaya yote aliyoyafanya.

“Au nitampigia baadaye…” alisema na kuacha.
Wakati akiwa amesimama mahali hapo, kwa mbali akaliona gari kubwa aina ya Scania likija kule alipokuwa. Kwa haraka sana akasimama kutoka pale alipokaa na kusogea barabarani, kilichofuata ni kuanza kulisimamisha gari hilo kwa kupunga mkono juu, dereva akasimamisha gari hilo, hakuwa na hofu ya utekaji kwa kuwa bado alikuwa ndani ya jiji hilo.

“Nikusaidie nini? Mbona usiku sana?” aliuliza dereva huyo aliyeonekana kuwa na miaka sitini au zaidi.
“Nataka kwenda mkoani, nimefiwa rafiki yangu!”
“Umefiwa na nani?”

“Mama yangu! Tena usiku huuhuu. Naomba unisaidie swahiba…”
“Unakwenda wapi?”
“Dodoma..”

“Daah! Una bahati sana, mimi nakwenda Singida…ingia nikusaidie,” alisema dereva yule huku akifungua mlango. Dickson akaingia, kitu alichokutana nacho kwenye ‘dashboard’ ni Biblia ambayo ilimfanya kuamini kwamba mtu aliyempa lifti alikuwa Mkristo mzuri tu.

Safari ikaanza, garini, Kamanda Dickson hakutaka kuwa kimya, alikuwa mzungumzaji sana huku muda wote akijitahidi kubadilisha sauti yake na kusikika kivingine kabisa. Alimwambia dereva yule namna alivyoguswa na msiba wa mama yake kwani jinsi alivyokuwa akimlea tangu alipokuwa mtoto mpaka kipindi hicho, kwa kweli moyo wake ulimuuma sana.

Dereva yule alimwamini kwa kila alichomwambia, alichokifanya ni kumfariji na kumtia moyo kwamba hiyo yote ilikuwa ni mitihani ya dunia hivyo kama mwanaume alitakiwa kupambana mpaka pale atakaposhinda.

Kwa kipindi kifupi tu, wakazoeana, wakaanza kuzungumza kana kwamba walikutana kipindi kirefu kilichopita. Ingawa ilikuwa usiku sana lakini hakukuwa na mtu aliyetamani kulala, walibaki wakizungumza mpaka walipoingia Mbezi Mwisho.

Wakati wanatoka Mbezi Mwisho na kuanza kuelekea Kibamba, kwa mbali mbele wakaanza kuona msururu wa magari makubwa ya mizigo yakiwa yameegeshwa pembeni, hawakuelewa ni kitu gani kilichokuwa kikiendelea, alichokifanya dereva yule ni kusimamisha gari lake karibu na gari jingine, akateremka na kumfuata dereva mwingine ambaye naye alisimamisha gari lake pembeni.

Kamanda Dickson hakujua kitu kilichokuwa kikiendelea, muda wote macho yake yalikuwa katika saa yake, alijiona kuchelewa, alitamani kumwambia dereva yule arudi kwani safari yake ndefu ilitakiwa kufanyika usiku kwa usiku na kama ikifika asubuhi, angekaa hotelini ambapo huko angeshinda siku nzima mpaka usiku ambapo angeendelea na safari yake.

“Kuna nini?” aliuliza Dickson wakati dereva aliporudi.
“Hawa polisi wanazingua sana, eti kuna mtu wanamtafuta…” alijibu dereva yule huku akionekana kukasirika.
“Mtu gani?”“Yule Kamanda Dickson, nasikia kavuruga, nilipata stori yake juu-juu tu usiku huu, ndiyo wanamtafuta kwa kupekua kila gari,” alijibu dereva yule pasipo kufahamu yule mtu aliyekuwa akizungumza naye ndiye aliyekuwa akitafutwa.

Moyo wa Dickson ukapiga paa, damu ikaanza kuzunguka kwa kasi mwilini mwake, hakuamini alichokisikia, hapohapo akajikuta akianza kutokwa na kijasho chembamba na wakati kulikuwa na kibaridi.

Polisi waliokuwa mahali hapo wakayaruhusu magari kusogea kule walipokuwa na gari walilokuwemo nalo likaruhusiwa, likaanza kusogea kule kulipokuwa na idadi kubwa ya polisi. Hakujua afanye nini kuwaepuka, akajikuta akianza kusali tu Mungu amuokoe na avuke salama.

Je, kitaendelea nini? Tukutane wiki ijayo.

2 Comments
  1. Abdyi1 says

    Dah Kamanda Anaelekea Kupotea

  2. Emmanuel says

    Nomaa

Leave A Reply