The House of Favourite Newspapers

Jini Mweusi-73

0

Hali ya sintofahamu inazuka jijini Dar es Salaam, machangudoa wengi wanaanza kuuawa katika mazingira ya kutatanisha. Hakuna anayemjua muuaji, kila changudoa anayenunuliwa na mwanaume aliyekuwa kwenye gari aina ya Volkswagen nyeusi, anauawa kikatili.

Kila mmoja anaogopa, machangudoa wengine wanaacha kujiuza, wanajifungia vyumbani mwao, ila kwa wengine ambao hawakuweza kuishi bila kufanya biashara hiyo, wanakwenda huko, bado wengine wanaendelea kuuawa.
Aliyekuwa akiwaua wanawake hao ni Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda ya Dar es Salaam, Dickson. Aliwaua kwa siri lakini baada ya kipindi fulani kupita, akagundulika na hivyo kuanza kutafutwa.
Kwa sasa yupo Mlandizi, baada ya kuona msako umekuwa mkubwa barabarani anaamua kwenda Mwanza kwa miguu kupitia Mlandizi. Anapofika porini, anaamua kujipumzisha huku polisi wenye mbwa wakiendelea kusogea kule alipokuwa.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Ilikuwa ni lazima kupambana na watu hao. Aliwahesabu, aliangalia silaha walizokuwa nazo, hazikuwa na uwezo wa kumfanya kutofanikiwa kufanya kile alichotaka kufanya.
Mtu wa kwanza kabisa ambaye aliona kama angeweza kumkabili na kuwashinda wengine, alikuwa Iddi. Huku mwanaume huyo akiwa amemsogelea kwa ajili ya kumfunga kamba, alichokifanya Dickson ni kukunja ngumi yake nzito na kumpiga Iddi ngumi ya shingo iliyomfanya kupiga uyowe mara moja tu, akaanguka chini.
Wale wengine walipoona hivyo, hawakutaka kukubali, hicho ndicho alichokitaka Dickson, wa kwanza alipomsogelea, akamdaka kwa mkono mmoja, akampiga kichwa kimoja kitakatifu usoni, jamaa akaanza kuona mawenge, hata alipoachwa na kutaka kukimbia, akapepesuka akashindwa, kuendelea mbele, akalala chini na kuanza kupiga kelele.
Walibaki wawili, wakabaki wakiangaliana tu, mapigo mawili aliyowapiga wenzao yaliwachanganya hata wao wenyewe. Hawakujua kama huyo mtu alikuwa wa kawaida au mzimu, hawakutaka kubaki mahali hapo, waliogopa, hawakutaka kufa, waliyapenda maisha, kilichofuata ni kukimbia.
Dickson alitisha, mapigo aliyowapiga watu wale yalikuwa mawili, kila mmoja moja lakini yalikuwa ya maana yaliyoonesha kwamba kama angewapiga kwa mapigo matatu au zaidi, wangeweza kufa.
Ndani ya sekunde chache, Dickson akabaki peke yake, hakutaka kubaki mahali hapo, bado alikuwa na safari ndefu na ilikuwa ni lazima kusonga mbele kwani asingeweza kurudi nyuma. Akaondoka zake.
Mpaka alfajiri inaingia, bado Dickson alikuwa akielekea mbele, hakujua mahali alipokuwa akielekea palikuwa wapi, kitu pekee kilichomjia kichwani mwake ni kwamba alikuwa akikimbia kuepuka mkono wa sheria.
Alikimbia mpaka alipofika sehemu iliyokuwa na mto mdogo ambao maji yake yalikuwa yametulia. Hakutaka kuvuka, kitu cha kwanza kabisa akasimama pembeni na kuanza kunawa uso wake.
Njaa kali ilianza kumuuma, alikuwa na fedha za kutosha mifukoni mwake lakini hazikuwa na thamani kipindi hicho, hakuwa na pa kuzitumia, alibaki nazo mifukoni kama mtu aliyekuwa na makaratasi yasiyokuwa na umuhimu wowote ule.
Ilikuwa ni lazima avuke kuelekea upande wa pili wa mto ule, hakujua angevuka vipi lakini ilikuwa ni lazima afanye hivyo. Mtoni, hakukuwa na mtumbwi wowote ule, kuna kipindi alifikiria kuogelea mpaka upande wa pili lakini wakati mwingine akahisi kufanya hivyo si vizuri kwani hakujua ndani ya mto ule kulikuwa na nini.
Alichokifanya ni kwenda pembeni na kupumzika. Hapo ndipo mawazo yake yalipoanza kurudi nyuma, tangu siku ya kwanza alipoanza kufanya kazi ya upolisi, alipokutana na msichana Pamela mpaka siku hiyo. Kwenye kila kitu alichokuwa akikifikiria, kilimuumiza, hakuamini kwamba yeye huyohuyo, leo hii ndiye angekuwa akitafutwa Tanzania nzima.
Pale alipojipumzisha, akajikuta akipitiwa na usingizi na baada ya dakika kadhaa, akaamshwa na sauti za watu waliokuwa mtoni.
Haraka akasimama, akayatupia macho yake mtoni, wavuvi waliokuwa na mtumbwi walikuwa wakipiga kasia.
Huo ndiyo ulikuwa msaada wake mkubwa wa kumvusha mahali hapo, alichokifanya ni kuanza kuwaita kwa kuwapigia mluzi. Wale wavuvi waliposikia, wakageuza mtumbwi wao na kuanza kumfuata.
“Mbona upo hapa?” aliuliza mvuvi mmoja.
“Nilikuwa nasubiri msaada wa kunivusha kule ng’ambo,” alijibu Dickson.
“Haujakutana na kitu chochote kibaya?”
“Hapana! Kwani kuna nini?” aliuliza Dickson, kauli za mzee yule zikamfanya kuhisi kitu.
“Basi tu.”
Hakutaka kuuliza swali jingine, alichokihitaji ni msaada tu na wavuvi wale wakaanza kufanya kama alivyoomba. Muda wote macho yao yalikuwa kwenye maji, Dickson hakujua walikuwa wakitafuta nini, akaona bora aulize.
“Kuna mamba wengi sana, huwa wanatumaliza sana wanakijiji,” alijibu mvuvi mmoja baada ya kumuuliza kuhusu utazamaji wao wa makini mtoni.
“Kuna mamba? Mto huu una mamba?” aliuliza Dickson.
“Ndiyo! Tena mamba hatari sana. Umeshawahi kusikia kuhusu Malupupu?” aliuliza mvuvi mmoja.
“Hapana! Ndiyo nini?”
“Ni aina ya mamba wanaopatikana katika mto huu ni hatari sana,” alijibu mvuvi mwingine.
Walibaki wakizungumza mpaka walipofika ng’ambo ambapo Dickson akateremka na kutaka kuwalipa lakini wazee wale walikataa katakataka kwa kumwambia kwamba walimsaidia tu,
Hakutaka kujali, alichokifanya ni kusonga mbele zaidi. Baada ya dakika kadhaa, akafika katika kijiji kimoja kikubwa, kilichokuwa na nyumba nyingi za nyasi, kijiji hiki kiliitwa Mzenga, Kusini mwa Mkoa wa Morogoro ambapo kulikuwa na kanisa kubwa lililojengwa na Wamishenari miaka ya nyuma.
Wanakijiji waliomuona Dickson, wengi wakaanza kukimbia. Walimuogopa, Dickson hakujua kitu gani kilikuwa kimesababisha mpaka watu hao kuanza kumkimbia. Wakati akijiuliza hilo, mara mbele yake akasimama kijana mmoja aliyeonekana kuwa mtanashati.
Alikuwa tofauti na wanakijiji wengine, kwa jinsi alivyovaa wala isingekupa wakati mgumu kugundua kwamba mtu huyo alitoka mjini siku za hivi karibuni. Wakabaki wakiangaliana tu.
“Kwa nini umekuja katika kijiji chetu?” aliuliza jamaa huyo, alionekana kumfahamu Dickson kwa sura, hata alipomwangalia, sura ya mwanaume huyo haikuwa ngeni kabisa, alimfahamu.
Wakati Dickson akibaki na maswali mengi, hapo ndipo alipogundua kwamba kijana yule aliyesimama alikuwa na karatasi yenye picha, alipoiangalia vizuri karatasi ile, akaiona ikiwa na picha yake, moyo wake ukapiga paaaaa.
Je, nini kitaendelea? Usikose Alhamisi ijayo.

Leave A Reply