The House of Favourite Newspapers

Jinsi Mwanamke Anavyoweza Kupata Saratani Ya Matiti-2

WIKI iliyopita nilianza kuzungumzia namna mwanamke anavyoweza kupata saratani ya matiti. Wiki hii nitaimalizia mada hii ili nianze mada nyingine. Iko hivi, saratani ya matiti pia inarithiwa. Endapo katika familia yenu au ndugu mwingine wa karibu sana alipatwa na saratani ya matiti, basi upo uwezekano wa wewe kupata saratani hii. Vinasaba vya saratani vinavyozunguka katika ukoo wenu ambavyo husababisha watu wa kwenu wapate saratani ya matiti, vinasaba vya saratani ya matiti vinaitwa BRCA 1 na BRCA 2.

 

Hali ya maisha pia huchangia mwanamke kupata saratani ya matiti. Wanawake walio katika hali bora ya maisha mfano wale wasomi wenye kipato kizuri au wafanyabiashara na wengine ambao wapo vizuri kiuchumi wapo hatarini kupatwa na tatizo hili. Wengine ni wanawake ambao wanazaa halafu hawanyonyeshi watoto au wanawanyonyesha kwa kipindi kifupi kutokana na sababu Jinsi

 

mbalimbali pia wapo hatarini kupata saratani hii. Mionzi iwe ya Xray au ya viwandani ikielekezwa mara kwa mara kwenye kifua cha mwanamke mwenye umri wa chini ya miaka thelathini basi anaweza kuja kupata saratani ya matiti miaka ijayo. Ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi mfano nyama choma, kitimoto, unywaji wa pombe na hata uvutaji wa sigara kwa mwanamke vinaweza kuleta madhara baadaye na kujikuta unapata tatizo hili.

 

Wengine wanaoathirika na tatizo hili ni wanawake wanene sana. Unene uliopitiliza utaujua kwa kupima uzito kwa kiwango cha BMI au Body Mass Index. Mwanamke mnene ana kiwango kikubwa cha homoni ya Estrojen inayoweza kumletea saratani ya matiti. Mwanamke ambaye tayari alishawahi kutibiwa saratani ya titi moja naye yupo hatarini kuathirika titi la pili. Matumizi holela ya vidonge vya uzazi wa mpango bila ya ushauri wa kitaalamu unaweza kuchochea kutokea kwa tatizo hili la saratani ya matiti.

 

Tatizo hili huanza kuwatokea wanawake kuanzia umri wa miaka ishirini hadi arobaini, hawa ndiyo kundi kubwa na likitokea katika umri wa zaidi ya miaka arobaini hali huwa mbaya zaidi. Kuna baadhi ya tafiti zinaonyesha kwamba, makundi mengine ya wanawake walio hatarini kupatwa na saratani ya matiti ni wale wanaofanya kazi za usiku, endapo watakaa karibu na taa za umeme zenye mwanga mkali kwa kipimo cha 50-60Hz, kutokana na miale yake ya magnetic kuzuia hali ya kawaida ya utoaji wa vichocheo vya melatonin ambavyo hasa hutoka wakati wa usiku mwilini mwa kila mwanamke, vikiwa na kazi maalumu ya kudhibiti utolewaji holela wa vichocheo vya Estrojeni ambavyo vikizidi ndipo saratani hii inatokea.

 

Makundi mengine ni wanawake wasagaji kutokana na tabia yao ya kutozaa au kuja kuzaa katika umri mkubwa wapo hatarini kupatwa na tatizo hili la saratani ya matiti, wafanyakazi wa kwenye ndege, hawa hupata saratani ya matiti.

 

NINI CHA KUFANYA? Saratani ya matiti ni rahisi kuidhibiti. Kuwepo na utaratibu wa mwanamke mmoja mmoja au kwa vikundi kumwona daktari au wataalamu wa afya kwa uchunguzi. Uwepo utaratibu wa maeneo ya kazi kuwafanyia upimaji wakinamama. Saratani ya matiti ikichelewa unaweza kupoteza uhai.

 

Ni vema uwahi hospitali kwa uchunguzi wa kina na tiba. Endapo itathibitika kuna tatizo kwenye titi lako, basi vipimo vya awali ni ultrasound, mamography, X-ray ya kifua na majimaji au kinyama kwenye titi ni muhimu. Endapo utahisi titi linauma, linatoa majimaji wakati hunyonyeshi au ukikamua linatoa damu, basi muone haraka daktari wako. Dalili nyingine ni kuhisi titi gumu au kuna uvimbe kwapani au ndani ya titi, chuchu zimezama ndani au ngozi ya titi inakuwa na makunyanzi kama ganda la chungwa.

DK. CHALE SIMU: +255713350084

Comments are closed.