The House of Favourite Newspapers

JINSI MWANAMKE ANAVYOWEZA KUPOTEZA UWEZO WA KUSHIKA MIMBA

KUTOPATA ujauzito ni miongoni mwa matatizo makubwa yanayowaumiza wanawake wengi kisaikolojia. Mwanamke kutokupata mimba kunaweza kusababishwa na matatizo yake mwenyewe ya uzazi au matatizo ya uzazi ya mume wake. Matatizo ya mwanaume katika mfumo wa uzazi yamegawanyika katika makundi mawili. Kwanza, ni kutokuwa na nguvu za kufanya tendo la ndoa na pili, ni kutokuwa na uwezo wa kuzalisha mbegu za uzazi zenye ubora.

Kutokuwa na nguvu za kufanya tendo la ndoa kwa mwanaume lipo kwa kiasi kidogo kulinganisha na tatizo la kutozalisha mbegu za kiume. Siyo kila mwanaume mwenye uwezo mzuri wa kufanya tendo la ndoa anatoa mbegu zenye ubora wa kumpa mwanamke mimba.

Tunaposema mwanamke hapati ujauzito ni kwamba, endapo hana historia ya kupata ujauzito hapo awali na ameishi na mwanaume kwa mwaka mmoja na tendo la ndoa linafanyika kikamilifu, lakini hakuna mimba, basi tunasema kuna tatizo. Vilevile endapo mwanamke ana historia ya kuwahi kupata mimba awe na watoto au la na anaishi na mumewe ndani ya miezi sita wakitafuta mimba, lakini kipindi chote hicho hakuna, basi tunasema kuna tatizo.

Tunaposema tendo la ndoa linafanyika kikamilifu ni pale uume unapoingia ukeni na tendo lenyewe linafanyika katika siku zile za kupata mimba. Siku za kupata mimba wengine huziita ni siku za hatari ambapo mwanamke anakuwa katika upevushaji mayai au ovulation.

Mwanamke aliye katika kipindi cha upevushaji mayai hupata dalili kuu za ute wa uzazi. Ute huu umegawanyika katika sehemu kuu tatu ambazo ni ute mwepesi, ute wa kuvutika na ute mzito. Ute mwepesi huchukua siku mbili, ute wa kuvutika siku moja, tena ni saa zisizozidi kumi na mbili na ute mzito siku mbili hadi tatu.

Dalili nyingine ni kuongezeka kwa hamu ya tendo la ndoa kipindi hicho cha ute wa uzazi, maumivu kidogo ya chini ya tumbo, maumivu ya matiti na joto la mwili hupanda kidogo. Kipindi cha ute wa uzazi ndipo mayai yanapotoka.

Kila mwanamke anapaswa kuwa hivi na pia ni lazima mwanamke apate ujauzito pale anapohitaji. Endapo hafanikiwi, basi tunasema kuna tatizo ambalo linahitaji uchunguzi wa kina na tiba. Matatizo ya uzazi tunayagundua kwanza kwa kufuatilia historia ya uzazi kwa mume na mke na vipindi ambavyo tayari wameshakaa pamoja.

JINSI TATIZO LINAVYOTOKEA

Tatizo la kutoshika mimba kwa mwanamke limegawanyika katika sehemu kuu mbili. Matatizo haya yapo kwa asilimia hamsini kila moja. Kwanza ni tatizo katika viungo vyake vya uzazi, pili ni tatizo katika mfumo wa vichocheo au homoni. Viungo vya uzazi vya mwanamke ni uke, mlango wa kizazi au cervix, kizazi, mirija ya uzazi na vifuko vya mayai.

Matatizo yoyote katika sehemu hizi huleta athari kubwa kwa uzazi, tatizo linaweza kukwamisha kupata ujauzito au hata kuharibika kwa mimba. Vichocheo au homoni kwa mwanamke ni nyingi ambazo zipo zinazosaidia mzunguko wa hedhi, za upevushaji wa mayai na zinazoleta changamoto na mabadiliko mbalimbali mwilini.

Baadhi ya homoni hizi ni kama Progesterone, Estrogen, Prolactin, LH, TSH, FSH na nyinginezo ambazo huwa kwa kiwango maalum na vipindi maalum mwilini. Upungufu katika mojawapo ya vichocheo hivi huleta athari kwenye mfumo wa uzazi. Huweza kusababisha kutopata ujauzito au mimba kutoka zenyewe.

MATATIZO KATIKA MFUMO WA VIUNGO VYA UZAZI

Kama tulivyoona aina ya viungo vya uzazi vya mwanamke, tutaanza kuzungumzia kiungo kimojakimoja, tukianzia ukeni hadi kwenye vifuko vya mayai. Matatizo ya ukeni yanayoweza kuleta athari katika uzazi ni maambukizi sugu ukeni. Kwa kawaida mwanamke mwenye afya nzuri ukeni kwake huwa na hali ya tindikali inayoletwa na bakteria waitwao Lactobacilli ambao wameumbwa hapo na mwenyezi Mungu. Endapo tindikali hiyo itapungua au kupotea ukeni, basi ni rahisi kupata maambukizi.

Maambukizi ya ukeni ni fangasi na maambukizi ya bakteria endapo inaweza kuwa magonjwa ya zinaa na mengineyo. Dalili nyingine ni maumivu wakati wa kujamiiana, kutokwa na harufu mbaya ukeni, kupata vidonda au uvimbe ukeni kama vijipu.

Maambukizi haya husambaa hadi kwenye mlango wa uzazi. Maambukizi katika mlango wa uzazi au cervix ni mengi ambayo ni matokeo au mwendelezo wa maambukizi ya ukeni. Dalili za maambukizi ya mlango wa kizazi ni maumivu wakati wa kujamiiana na kuhisi kama kitu kinasukumwa, kuhisi uvimbe ukeni kama gololi kubwa kwa ndani wakati wa kujisafisha.

Mlango wa kizazi au shingo ya kizazi pia ni rahisi kupata kansa au saratani. Hivyo basi, endapo una tatizo hili kwa muda mrefu, ni vizuri ukawa na tabia ya kufanyiwa uchunguzi mara kwa mara kwa daktari wa magonjwa ya kina mama. Kizazi au uterus kimetengenezwa kwa misuli mororo inayovutika ndiyo maana mama anapokuwa mjamzito, tumbo linakuwa kubwa na baada ya kujifungua linasinyaa.

Kizazi kina tabaka tatu, kwanza ni tabaka la ndani linaitwa endometrium, pili ni tabaka la kati au myometrium na tabaka la nje au perimetrium. Matatizo yanayotokea katika kizazi ni kugeuka kwa tabaka la ndani la kizazi hali iitwayo endometriosis, maambukizi sugu ndani ya kizazi kama vile PID na endometritis, uvimbe kwenye kizazi (fibroids) na uwepo wa usaha ndani ya kizazi.

Matatizo yote haya huambatana na dalili mbalimbali kama maumivu ya mara kwa mara chini ya tumbo, kutokwa na uchafu au majimaji ukeni yenye harufu mbaya, kuhisi uvimbe ukeni, damu kutoka bila mpangilio ukeni, maumivu wakati wa hedhi na hata upungufu wa damu mwilini kutokana na damu kutoka bila mpangilio.

Tatizo lingine katika kizazi lipo kwenye mirija ya uzazi. Mirija ya uzazi ipo miwili kwa mwanamke, mmoja kulia na mwingine kushoto. Kazi ya mirija ya uzazi ni kusafirisha mayai na kutungisha mimba. Mimba inatungwa kwenye mrija halafu inasafirishwa hadi ndani ya kizazi ili ikue.

Mirija ya kizazi ina sehemu kuu tatu, kwanza ni sehemu inayoungana na kizazi ambayo ni nyembamba, halafu sehemu ya kati ambayo ni pana, mwishoni mwa mirija ni vidole vyake vyenye kazi ya kuchukua yai lililokomaa na kuliingiza ndani ya mirija. Yai lisipokutana na mbegu hutoka na damu ya hedhi.

Matatizo kwenye mirija ni maambukizi yatokayo kwenye kizazi na kusambaa huko, mirija kukatwa kwa upasuaji wa kufanga kizazi au mimba kutungia kwenye mirija, ectopic pregnancy. Dalili za maambukizi ya mirija ya uzazi ni maumivu chini ya tumbo yanayosambaa kulia na kushoto, maumivu ya kiuno, maumivu wakati wa kujisidia haja ndogo, maambukizi makali huweza kusababisha mgonjwa awe na homa.

Athari za maambukizi ya mirija ni kuziba kwa mirija. Mirija inaweza kupoteza uwezo wake wa kutungisha mimba kama itakatwa, pia endapo itaharibika kwa maambukizi. Maambukizi ya mirija huweza kusababisha mirija iharibike kwa kujaa maji au hydrosalpinx au kujaa usaha au pyosalpinx. Itaendelea wiki ijayo.

Comments are closed.