JINSI YA KUEPUKA MIMBA ZISIZOTARAJIWA-2

WIKI iliyopita nilianza kuelezea vipengele kadhaa kuhusiana na makala haya na wiki hii nitamalizia.

DALILI ZA KUPEVUKA YAI NI ZIPI?

MWANAMKE anaweza kuona dalili za yai kupevuka kwa karibu siku tano kabla.

Dalili kuu na viashiria vya yai kupevuka ni pamoja na mabadiliko ya ute kwenye mlango wa uzazi na kuongezeka joto la mwili. Dalili nyingine ni maumivu ya tumbo, kujaa maziwa na kupata maumivu kwenye maziwa. Mwanamke pia anaweza kuwa na dalili ya kuumwa kiuno, mgongo na baadhi hutokwa chunusi usoni au uso kutakata isivyo kawaida.

Halikadhalika kuna wanaoumwa tumbo na hata kuharisha na kuwa na hamu ya kushiriki tendo la ndoa kuliko kawaida. Ute wa mlango wa uzazi ni uteute anaouona mwanamke kwenye nguo ya ndani au kwenye karatasi laini (tissue) anapokwenda kujisaidia haja ndogo.

Mabadiliko ya ute wa mlango wa uzazi ni alama ya kuwa mwanamke yupo kwenye dirisha la kuweza kupata mimba. Baada ya hedhi kuisha ute wa mlango wa kizazi huongezeka kwa ujazo na hubadilika pia hali yake. Mabadiliko haya yanaendana na kuongezeka kwa kiwango cha homoni ya oestrogen mwilini.

Mwanamke atakuwa zaidi kwenye uwezo wa kupata mimba kama uteute unakuwa hauna rangi, unateleza sana na unavutika. Ute huo hufanana na sehemu nyeupe ya yai ukilivunja. Kazi ya uteute huu ni kusaidia mbegu kuwa na spidi zaidi wakati zinaogelea kuelekea kwenye mfuko wa kizazi. Halikadhlika huilisha na kuilinda mbegu inapokuwa inasafiri kuelekea kwenye mirija ya uzazi

Mwanamke mmoja kati ya watano huwa anasikia kitu kinaendelea kwenye mifuko yao ya mayai (ovaries) wakati wa kipindi cha upevushaji. Haya ni pamoja na maumivu madogomadogo au yanayovuta na kuachia. Mwanamke akizihisi dalili hizi katika kipindi kilekile kila mwezi, aangalie uteute wa mlango wake wa kizazi.

HISIA ZA TENDO LA NDOA

Hisia hizi ni dalili nyingine na mwanamke wakati mwingine huwa muongeaji zaidi au kutamani kuongea na wanaume. Mwanamke pia akijiona ngozi inakuwa laini kuliko kawaida na kujihisi kuwa na mvuto zaidi kimwonekano ni dalili pia. Sambamba na hilo, hata harufu ya mwili ya mwanamke huwa nzuri pia inayovutia wanaume katika kipindi hiki.

KUONGEZA UWEZO WA KUPATA MIMBA

Kama unatafuta mtoto, jaribu kukutana na mumeo kila baada ya siku mbili au tatu. Mbegu zenye uogeleaji mzuri zitakuwa sehemu husika siku yoyote ukiwa kwenye upevushaji. Tendo la ndoa la mara kwa mara kwenye mzunguko wako wote ni hatua inayokupa uwezo mkubwa wa kushika ujauzito. Kufanya tendo la ndoa wakati mlango wa kizazi chako una uteute ni wakati unaoongeza uwezo wako wa kupata ujauzito.

Cha kuzingatia ni kwamba, utumiaji wa mzunguko wa hedhi ni njia moja wapo ya asili ya kujikinga na mimba zisizotarajiwa au njia ya kupanga kuzaa.


Loading...

Toa comment