The House of Favourite Newspapers

Jinsi ya kujifunza kupitia matokeo ya mtihani wako

0

wanafunzi1Nina imani wote ni wazima wa afya na mnaendelea vyema na masomo yenu japo kuwa wengine mpo katika kipindi kigumu cha maandalizi ya mitihani, leo nitazungumzia jinsi ya kujifunza kupitia matokeo ya mitihani yako ili kuboresha kiwango chako cha ufaulu.

Wanafunzi wengi husoma kwa bidii iliyochanganyika na presha kubwa wakati wakijiandaa na mitihani yao, lakini mara baada ya kufanya mitihani hiyo husahau kwamba hatua nyingine ya msingi katika maisha yao ya kujifunza, ni kupitia tena matokeo ya mitihani yao mara baada ya kuipata.

Katika hatua hii mwanafunzi hupaswa kutazama matokeo yake kwa kila mtihani alioufanya kwa umakini mkubwa na kutathmini makosa yake na kufanya juu chini kuyapatia ufumbuzi wa majibu sahihi mara baada ya kujua makosa aliyoyafanya.

Hapa ndiyo mwanafunzi atagundua kama kosa lake kubwa ni kutoelewa vizuri mada fulani au ni makosa ya jinsi ya kujibu maswali ya aina fulani. Wengine huwa na makosa madogomadogo kama vile kusahau kuandika majina yake katika karatasi yake ya kujibia hivyo kupitia matokeo ya mitihani yake anaweza kujisahihisha.

Lengo kubwa la hatua hii ni kumfanya mwanafunzi asiweze kurudia kosa lilelile katika mitihani yake ijayo na kumuongeza ufahamu wa kile kidogo alichokuwa akikifahamu kabla ya kurudia mitihani yake.

Kwa bahati mbaya mitihani mingi mikubwa huishia kwa likizo ambapo wanafunzi hukosa nafasi ya kufanya marudio ya mitihani yao, lakini kwa baadhi ya walimu wachache wanaoelewa maana ya hatua hiyo muhimu, huwakusanya wanafunzi na kufanya marudio ya mitihani kwa pamoja kabla ya kufunga shule.

Walimu pia hushauriwa kuwasahihishia wanafunzi kwa kuwarekebisha baadhi ya makosa madogomadogo waliyoyafanya kwenye mitihani yao kwa wino mwekundu japokuwa wanafunzi wengi hawayatumii vyema masahihisho hayo kujifunza.

Sikatai kwamba kuna baadhi ya walimu na shule ambazo hazifanyi chochote katika kuhakikisha wanafunzi wanarudia mitihani yao lakini hiyo pia inaweza isiwe sababu kubwa sana kwa kuwa mwanafunzi mwenyewe anaweza akafanya juhudi kwa kupitia mitihani ya mwanafunzi mwenzake aliyefaulu vizuri na kuangalia jinsi alivyojibu na kuutumia mtihani wake kama njia ya kujitathmini.

Kama hiyo haitoshi mwanafunzi pia huweza kumtafuta mwalimu wake ili kupata maelekezo binafsi kwa uhakika zaidi wa jinsi ya kujibu kwa usahihi masomo yake.

Tukutane wiki ijayo.

Leave A Reply