KUKABILIANA NA MAUMIVU KWENYE TENDO LA NDOA KWA MWANAMKE

TATIZO hili kitaalamu linaitwa ‘Dyspareunia ‘. Maumivu hutokana na suala kubwa la matatizo katika tendo la ndoa au’ sexual Dysfunction’ ambalo linahusisha hali ya kutokuwa na hamu ya tendo la ndoa na kupoteza msisimko wa tendo la ndoa na kutofika kileleni wakati wa tendo hilo. Hayo yote mwisho wake ni huu mwanamke anahisi maumivu wakati wa tendo. Katika tatizo hili mwanamke anahisi maumivu ukeni ambayo yanakuwa mwanzo wa tendo la ndoa anapoanza tu, anapoendelea na anapomaliza. Maumivu haya hutokea zaidi kwa wanawake kama tulivyoona.

Hali hii ya maumivu huvuruga mfumo wa maisha ya mwanamke na kumkosesha furaha. Maumivu haya yanapotokea pia uhusiana na magonjwa mbali mbali kama maambukizi katika njia ya mkojo au yutiai, kutokwa na uchafu na muwasho ukeni au maumivu wakati wa hedhi.

CHANZO CHA TATIZO

Chanzo cha tatizo hili kimegawanyika kufuatana na jinsi tatizo linavyotokea, muendelezo wa tatizo na eneo husika yaani viungo vya uzazi vya mwanamke kuanzia ukeni.

JINSI TATIZO LINAVYOTOKEA

Utokeaji wa tatizo hili umegawanyika katika maeneo makuu mawili, kwanza ni utokeaji wa awali au ‘ Primary’ na pili utokeaji wa baadaye ‘Secondary’, utokeaji wa awali au’ Primary onset ‘ unahusiana endapo mwanamke ni mara yake ya kwanza kufanya tendo hilo hivyo anapata maumivu, wakati mwingine utokeaji huu huwa ni tatizo la kisaikolojia kutokana na woga au hofu ya kupata ujauzito au anaibia tu.

Wengine hupata maumivu haya kutokana na historia ya tangu utotoni kama alibakwa au aliingiliwa na kuumizwa ukeni, wengine hupata maumivu kwa kujilazimisha kushiriki tendo hili huku wakihisi aibu au wanajitoa kwa ajili ya jambo fulani mfano ili apate kazi au afaulu masomo, lakini nafsi zao haziko tayari. Mwingine kabla hajaingiliwa tayari ameshajenga hisia kwamba atapata maumivu pindi tu atakapoanza.

Maumivu yanayokuja kutokea baadaye au ‘Secondary onset’ ni kwamba hapa mwanamke hana historia yoyote ya kuwa na maumivu na siku zote anashiriki tendo hili bila tatizo lakini mara anaanza kuhisi maumivu taratibu kadiri siku zinavyosonga mbele, mara nyingi chanzo hapa ni hali ya kimaumbile labda ana ugonjwa na tatizo jingine lolote limejitokeza. Lakini pia hali hii ya tatizo la kimaumbile inaweza kutokea hata kwa mwanamke ambaye hana historia ya kuingiliwa.

JINSI TATIZO LA KIMAUMBILE LINAVYOTOKEA

Tatizo hili la kimaumbile tunaweza kuligawa katika makundi manne, kwanza ni endapo mwanamke anakasoro za kuzaliwa nazo ‘congenital Disorders’ ambazo ni uke kutofunguka au uke kuziba ‘Imperforated hymen’ kwa hiyo uume hauwezi kupenya na hapa hata damu ya hedhi haitoki. Tatizo jingine hapa ni ‘ vaginal septum’ambapo uke unagawanyika sehemu mbili kwa ndani hivyo kuhisi kama kuna kitu kwa ndani kinazuia . Tiba ya matatizo haya ni upasuaji.

Tatizo jingine la kimaumbile ukeni ni maambukizi sugu ukeni’ vaginitis ‘ kutokana na bakteria au fangasi ambapo mwanamke anahisi kutokwa na uchafu unaotoa harufu na muwasho ukeni, kubana kwa misuli ya uke ‘Vaginismus’ kunakosababisha upate maumivu. Mara tu tendo linapoanza, hii inatokana na woga au hofu dhidi ya tendo hili.

Matatizo ya tumbo na sehemu ya chini ya kitovu ‘Abdominal pelvic disorders’ ni mojawapo ya vyanzo hivi na mojawapo ya matatizo yanayochangia ni magonjwa kama ‘Endometriosis’ na uwepo wa uvimbe na maambukizi sugu ya kizazi.

Matatizo ya mfumo wa chakula nayo huchangia mfano kufunga kupata choo kikubwa kwa muda mrefu, na magonjwa ya utumbo mkubwa. Muendelezo wa matatizo haya ya maumivu yanaweza kuwa moja kwa moja yaani kila mara mwanamke anahisi maumivu hakuna siku hajapata maumivu kiasi kwamba hata mumewe nguvu za kiume zinapungua.

Maumivu pia hutokea na kupotea, yaani sio mara kwa mara anapata maumivu hali hii tunaita ‘conditional’ , hali hii ya maumivu inaweza kutokea au kupotea kutegemea na jinsi tendo lilivyoandaliwa, mlalo au ‘position’, kwa hiyo chanzo chake kinaweza kuwa hali ya maumbile au kisaikolojia.

AINA ZA MAUMIVU

Maumivu haya yamegawanyika katika sehemu kuu mbili, kuna maumivu ya juu juu ‘Superficial Dyspareunia’ ambayo ni kama vile ‘ Vulvodynia’, mwanamke uhisi maumivu ya kusuguliwa ndani ya uke na kama amewekewa pilipili, maumivu huendelea hata anapomaliza tendo.

‘Vaginismus’ uke unabana na uume unashindwa kupenya, mwanamke anaumia na mwanaume pia anaumia, nguvu za kiume zinapungua tendo linashindwa kuendelea. Maumivu mengine mwanamke anayapata baada tu ya kuzaa endapo alichanika msamba.

USHAURI

Matatizo haya huchunguzwa na kutibiwa katika kliniki za madaktari wa magonjwa ya kinamama. Matibabu hufanyika baada ya uchunguziwa kina, tiba hutegemea na chanzo, kama ni tatizo la kisaikolojia basi amwone mtaalamu wa kisaikolojia .

Tiba nyingine ni wewe mwenyewe kwa kuhakikisha unasisimka na unatoa majimaji ya kutosha ukeni, tumia milalo itakayokusaidia kufurahia tendo, tumia vilainishi vya ukeni utakavyoshuriwa na daktari wako. Matibabu mengine yatatolewa kadiri daktari atakavyoona inafaa.

Loading...

Stori zinazo husiana na ulizosoma

Toa comment