The House of Favourite Newspapers

JINSI YA KUKABILIANA NA MAUMIVU YA KICHWA!

KHALID Chokoraa ameimba; kuachwa kuachwa, kuachwa ni shughuli pevu, wewe unakonda mwenzako ananenepa kwa mawazo…kwa mawazo…kwa mawazo.  Hicho kilikuwa ni kibwagizo tu katika wimbo wake uitwao Kuachwa.

 

Chokoraa katika wimbo huo amejaribu kuonesha maumivu ya kuachwa kiasi cha mtu kufikia hatua ya kukonda.

Ndugu zangu, mapenzi yanauma haswa kama unakutana na kuanzisha uhusiano na mtu ambaye umempenda kutoka moyoni kisha akakuacha. Utatamani dunia ipasuke utumbukie ndani. Hukutarajia kuachwa solemba, unaumia kumuona mtu ambaye unampenda anakuacha.

 

Kwa ambaye hajawahi kukutwa na kitu hicho anaweza asielewe sana lakini ukweli ni kwamba, inapotokea mtu uliyempenda kabisa kutoka moyoni halafu akakuacha, lazima utaumia na wengi tu wamejikuta kwenye lindi la mawazo kwa muda mrefu.

 

Hawajui wafanye nini ili kujinasua. Wapo ambao hufikia hata hatua ya kunywa sumu kwa sababu tu ya kuachwa. Wapo wanaoshindwa kufanya shughuli zao za kila siku kwa sababu tu ya kuachwa. Wengine huenda hata kwa waganga kuwaroga wapenzi wao ili ne.

 

Wapo wengine ambao huthubutu hata kuwaua wapenzi wao na wao kujiua kutokana na jinsi walivyokuwa wanawahusudu wapenzi wao, kuwathamini na kuwapa mioyo yao kisha kuishia kupata maumivu ya kuachwa.

 

Marafiki zangu, leo nataka niseme na nyinyi. Nataka niseme na wewe ambaye kwa namna moja au nyingine upo kwenye maumivu ya kuachwa. Wewe ambaye pengine uliachwa mwezi uliopita, mwaka uliopita na hata ambaye umeachwa juzijuzi tu.

 

Kuachwa kwenye mapenzi kupo tu. Usione kama wewe ndio wa kwanza, usiwe mnyonge sababu maisha bado yapo tu bila huyo mtu uliyekuwa naye. Unachotakiwa ni kukubaliana na hali hiyo. Kweli unampenda, unamhitaji lakini kuna wakati unafika lazima ukubaliane na ukweli kwamba penzi linaweza kuisha. Penzi linaweza kufa kutokana na sababu mbalimbali.

 

Yawezekana mmepitia mambo fulani yaliyomfanya mwenzi wako achukue njia yake, yawezekana hakuwa amekupenda kwa dhati. Yawezekana umekuwa ukimkwaza mara kwa mara, hamuendani.

Yawezekana akawa amempata mtu mwingine ambaye pengine amemuona ni bora kuliko wewe, usiumie. Usijipe nafasi ya kuumia sana na mawazo. Unachotakiwa kufanya ni kuikubali ile hali. Chukua muda kutafakari, chukua muda wako kuumia kwa muda kisha fanya maamuzi haraka ya kutoutesa moyo wako. Sema; ‘acha aende.’

 

Usiruhusu akili yako kutawaliwa na mawazo ya aliyekuacha kwa muda mrefu sana. Fanya maamuzi ya kumtoa haraka moyoni. Sema na moyo wako kwamba kama mtu ameamua kukuacha, amekuona huna umuhimu, hauna sababu wewe kumuona ni wa muhimu.

 

Yawezekana akawa amefanya maamuzi ya kukurupuka na kukuacha, akirudi na wewe ukiwa tayari umeshaanzisha mahusiano mengine basi shauri yake. Mpe ukweli wake kwamba amechelewa, amecheza na dunia na wewe ukamchezea kwelikweli.

 

Kikubwa wewe ni kuuchangamsha moyo wako kwa kufanya mambo yatakayokufanya usiwe unamuwaza mara kwa mara. Kuwa bize na mambo yako mengine, usijifungie peke yako na kumuwaza yeye. Muombe Mungu akupe mtu sahihi, usiteswe na kelele za watu kwamba kwa nini unaishi bila ya kuwa na mtu.

 

Mtu wako yupo. Atakuja kwa wakati wake. Usiharakie kuingia kwenye uhusiano kwa sababu tu mwenzako ameingia. Kila mtu ana muda wake na wewe utafika wakati wako ambao Mungu amekupangia.

 

Bila shaka utakuwa umenielewa. Tukutane wiki ijayo. Unaweza kunifuata kwenye mitandao yangu ya kijamii, Instagram na Facebook natumia Erick Evarist, Twitter natumia ENangale.

Comments are closed.