Jinsi ya kulikabili tatizo la kuvimba miguu!

WATU wengi hasa watu wazima wamekuwa wakipata matatizo ya kuvimba miguu na kupata maumivu makali.  Tatizo la kuvimba miguu husababishwa na kujikusanya kwa majimaji ambayo huvuja kutoka katika mishipa ya damu kutokana na sababu mbalimbali zinazosababisha damu ishindwe kurudi kwenye moyo kutoka katika miguu.

Kuvimba kwa miguu si ugonjwa bali ni dalili za ugonjwa fulani, unaweza kusababishwa na sababu zifuatazo; moja, kusimama au kukaa kwa muda murefu, pili; mri mkubwa, tatu; kwa wanawake wenye ujauzito, nne; ukosefu wa lishe bora, tano; kutokufanya mazoezi na sita mzunguko hafifu wa damu. Lakini pia kuumia au upasuaji wa mguu au enka husababisha pia kuvimba kwa miguu.

Kuvimba kwa miguu ni tatizo ambalo kila mmoja wetu anaweza kulipata, wakati mwingine hutokana na ugonjwa uitwao kitaalamu Edema. Uvimbe unapoongezeka humfanya mtu kuwa katika hali isiyo sawa na anaweza kushindwa kutembea na dalili nyingine husababisha maumivu na miguu kuwa myekundu.

Hali hii huweza kutokea pia kwenye mapafu, ubongo, tumboni na kwenye mapaja lakini kutokana na mvuto wa ardhi huweza kuonekana zaidi kwenye upande wa miguu wakati mwingine bila hata maumivu yeyote. Mambo yanayochangia na kusababisha tatizo ili mara nyingi huwa ni ujauzito, wajawazito wengi miguu yao huvimba lakini hawa huwa hawapati maumivu yoyote. Iwapo unaugua ugonjwa sugu wa ini, miguu huweza kuvimba na hakika ni dalili mojawapo ya kuumwa ini.

Figo vilevile zinapopata maradhi husababisha miguu kuvimba lakini pia magonjwa ya moyo ambayo husababisha kushindwa kufanya kazi yake sawasawa husababisha miguu kuvimba. Wengine ambao huvimba miguu ni wale wanaotumia dawa za kudhibiti shinikizo la damu. Dawa hizi husababisha miguu kuvimba sana, hali ambayo si nzuri kwa binadamu. Lakini pia kuna baadhi ya watu wanaposafiri kwa muda mrefu wakiwa kwenye mabasi, magari ya kawaida au hata ndani ya ndege, miguu yao huvimba.

TIBA NA USHAURI

Kuna njia mbalimbali ambazo unaweza kufanya ili kuisaidia miguu yako isivimbe na iwe na hali ya kawaida lakini kwanza muone daktari endapo kuvimba kwa miguu kunaambatana na kubanwa na kifua, kushindwa kupumua, maumivu makali ya kifua, kuna maumivu au joto kali miguuni mwako na kama una matatizo ya magonjwa yoyote ya moyo, ugonjwa wa ini na maradhi ya figo.

Kuna njia nyingi za kukabiliana na tatizo hili, moja wapo ni CONTRAST HYDROTHERAPY! Hii ni njia rahisi inayoweza tumika nyumbani. Tiba hii huhusisha maji baridi na maji ya vuguvugu, weka migiuu yako kwenye beseni lililojaa maji ya vuguvugu kwa dakika 3 hadi nne kwa haraka hamishia kwenye beseni lenye maji ya baridi kwa muda wa dakika1, rudia vitendo hivyo mara 15 kila siku mpaka utapona.

Kama ni ugonjwa wa ini, figo nk. daktari atatoa tiba husika. Lakini kama huna dalili hizo za maradhi tuliyotaja hapo juu, unaweza kufanya yafuatayo kujitibu mwenyewe nyumbani Kwanza fanya mazoezi kwa kuinua miguu yako juu kuelekea upande wa kichwa na wakati umelala angalau kwa muda wa dakika 30 ili kuwezesha damu ya kutosha kurudi kwenye moyo.

Pili, fanya hivi angalau mara 3 kwa siku kupata matokeo bora zaidi lakini njia ya tatu ni kufanya mazoezi laini pia itakusaidia kupeleka damu kwenye moyo na hivyo kurekebisha mzunguko wa damu. Jambo la nne ni kwa wasafiri, wakati unasafiri safari ndefu hakikisha unasimama mara kwa mara ili kuifanya damu kuweza kupanda na kushuka miguuni.

Wakati huo wa safari epuka kuvaa kwa muda mrefu nguo zinazobana sehemu za mapaja na kama umnene kupita kiasi fanya mazoezi mara kwa mara ili kupunguza uzito. Lakini yote hayo ukiyafanya na miguu kuendelea kuvimba ni vema ukamuona daktari ili akupime na kisha kukupa dawa stahiki ili upone kabisa.


Loading...

Toa comment