JINSI YA KUMJUA MTOTO MWENYE TUNDU KWENYE MOYO

Kama kawaida safu hii huwa tunajadili masuala mbalimbali yanayohusu afya na tiba ili kupata ufahamu zaidi juu ya kuimarisha afya zetu na ya jamii nzima kwa ujumla. Leo tutazungumzia ugonjwa unaojulikana kama tundu katika kuta za ventrikali za moyo au kwa kitaalamu Ventricular Septal Defect (VSD). Tatizo ambalo hutokea mara nyingi ambapo watoto wawili hadi 6 kati ya 1,000 huzaliwa na tatizo hilo. Tundu katika kuta za chini za moyo au VSD ni pale panapokuwepo na uwazi katika sehemu ya kuta ya septum inayotenganisha chemba za ventrikali ambazo ni chemba za chini za moyo.

Pale moyo unapoanza kuumbika huanza kama bomba lililo wazi na kuendelea kujigawa katika sehemu mbalimbali na kuunda kuta. Iwapo kitendo hicho hakitatekelezeka ipasavyo, hutokea uwazi katika kuta ya septum kwenye chemba za chini. Kuwepo tundu hilo huruhusu damu yenye oksijeni kupita kutoka chemba ya kushoto ya chini ya moyo na kuingia katika chemba ya kulia ya chini ya moyo, badala ya kuingia kwenye mshipa wa aorta

na kuelekea nje ya moyo kama inavyotakiwa. Tundu la VSD linaweza kuwa dogo, la kati au kubwa. Tundu dogo katika kuta za chini za moyo huruhusu damu ndogo tu kutoka upande mmoja wa moyo kwenda wa pili hivyo haliathiri utendaji wa kawaida wa moyo na kwa kawaida huwa halihitaji matibabu maalumu.

Matundu ya aina hiyo huziba yenyewe wakati moyo unapoendelea kukua kipindi cha utotoni. Matundu yenye ukubwa wa kati na kubwa katika kuta za chini za moyo huruhusu kiwango kikubwa zaidi cha damu kupenya toka upande mmoja wa moyo kwenda mwingine, na mara nyingi huhitaji matibabu maalumu. Watoto wenye tundu dogo katika moyo, huweza kukua bila matatizo yoyote, wakati wale wenye tundu kubwa huanza kuonesha dalili mapema.

Vifuatavyo ni vihatarishi ambavyo vinaweza kusababisha mtoto kuzaliwa na tundu katika kuta za chini za moyo ni mama kuwa na maambukizi ya Rubella katika kipindi cha ujauzito au kuwa na ugonjwa wa kisukari cha wakati wa ujauzito ambao haujadhibitiwa na kuwa mnywaji wa pombe au mtumiaji wa madawa ya kulevya. Mjamzito akitumia bila ushauri wa daktari baadhi ya dawa za hospitali katika

kipindi cha ujauzito pia huweza kusababisha mtoto azaliwe na tundu katika kuta za chini za moyo.

DALILI

Iwapo tundu ni dogo huwa halina dalili yoyote na pale mtoto anapoendelea kukua tundu hilo hujifunga lenyewe. Lakini tundu likiwa kubwa, japokuwa mtoto anayezaliwa huwa haonyeshi dalili yoyote katika kipindiĀ  hicho lakini baadaye huwa na dalili zifuatazo. Rangi ya ngozi yake, midomo na kucha hubadilika na kuwa ya bluu, kunyonya au kula huwa kwa shida sana, pia ukuaji wa shida, kupumua kwa shida, kuchoka haraka, kujaa miguu na kuvimba tumbo, kuwa na mapigo ya moyo ya haraka. Mtoto mwenye tatizo hili anapopimwa na daktari kwa kifaa, huweza kusikia ishara ya ongezeko la sauti ya ziada ya mapigo ya moyo wa mtoto hali ambayo kitaalamu huitwa holosystolic murmur.

MADHARA YA TUNDU KATIKA MOYO

Madhara ambayo yanaweza kusababishwa na tundu katika kuta za chini za moyo ni Eisenmenger syndrome, hali ambayo hutokea pia pale mtu anapokuwa na tundu katika kuta za juu za moyo.

Tatizo hili hutokea wakati mtiririko wa damu unapoongezeka kutoka kushoto kwenda kulia kupitia tundu katika kuta za moyo, suala ambalo huongeza mtiririko wa damu katika mishipa ya mapafu na kusababisha shinikizo la damu katika mapafu. Hali hii husababisha ongezeko la shinikizo la damu katika upande wa kulia wa moyo na kubadilika kutoka kulia kwenda kushoto.

Matokeo yake ni kuwa damu isiyo na oksijeni iliyotakiwa kwenda kwenye mapafu kwa ajili ya kusafishwa huchanganyika na damu yenye oksijeni iliyoko upande wa kushoto na kusambaa mwilini. Madhara mengine ya tundu la VSD ni kupata ugonjwa wa kiharusi, moyo kushindwa kufanya kazi vizuri na pia maambukizi katika kuta za ndani za moyo (endocarditis) ugonjwa ambao Mungu akijaalia tutauelezea katika kipindi kijacho. Akina mama ambao wamezaliwa na tatizo hili, ambao wametibiwa na hawakupata madhara wanaweza kushika mimba na kupitisha kipindi cha ujauzito bila matatizo yoyote.

Isipokuwa wale ambao hawakutibiwa au ambao tayari wameshapata madhara, hushauriwa kutoshika ujauzito kwa sababu ya hatari zinazowezakutokea katika kipindi cha ujauzito. Vilevile kwa akina mama waliozaliwa na tatizo hili, uwezekano wa watoto wao kuzaliwa na tatizo hili huwa mkubwa.

TIBA

Inafaa kujua kuwa, karibu nusu ya wagonjwa wenye tatizo hili huwa hawahitaji matibabu ya aina yoyote ile kwa kuwa tatizo hili hujirekebisha katika miaka ya mwanzo ya maisha yao. Hata hivyo, kwa wale ambao watahitaji matibabu, hutibiwa kwa dawa au upasuaji kwa kutegemea ukubwa wa tatizo lenyewe.

Dawa zinazotumika kutibu ugonjwa huu ni zile ambazo hupunguza kasi ya moyo, huongeza nguvu ya mapigo ya moyo na zile ambazo hupunguza maji mwilini au diuretics. Utaratibu wa kuziba tundu umegawanyika katika sehemu mbili na hufanyika iwapo tundu ni kubwa sana, au halikujirekebisha lenyewe wakati mtoto alipokuwa anakua na pale ikiwa dawa alizopewa mgonjwa hazikusaidia.

Pale inapohitaji upasuaji, mgonjwa hufanyiwa operesheni ambapo kifua hufunguliwa ili kuziba tundu la VSD. Matibabu mengine ni kupitisha mrija katika mshipa wa damu hadi katika sehemu ya tatizo kwenye moyo na kuliziba kwa kutumia kifaa maalumu. Kwa njia hii, huwa hakuna haja ya kufanya upasuaji wa kufungua kifua cha mgonjwa.


Loading...

Toa comment