JINSI YA KUMTAMBUA MWANAUME AMBAYE SI MUOAJI

ULIMWENGU wa sasa umejaa sanaa. Watu wameingiza sanaa kwenye kila eneo. Sanaa ipo hadi kwenye masuala ya uhusiano. Mtu anamfuata binti, anaingia na gia kabisa za kuoa kumbe siyo muoaji. Anakuwa na kitu anachokitaka, akikipata basi biashara imekwisha.  Matokeo yake wanawake wamekuwa waoga. Wapo ambao wamekata tamaa kabisa, hawataki kusikia kitu kinachoitwa ndoa maana kila walipojaribu kutupa karata wamejikuta wakiambulia maumivu. Hivyo wanaona bora kuishi kivyaovyao tu.

Mapenzi ni hisia, mtu anapowekeza hisia zake halafu akiambulia maumivu huwa inamkatisha sana tamaa. Anakuwa ameamini kwamba huyu ni mpenzi wangu, amemuweka moyoni halafu anakuja kuambulia maumivu, inauma. Wanawake wamekuwa wakiwaona wanaume wengi wa siku hizi ni waongo, wahuni na watu ambao mwalimu wao ni mmoja. Wanajua hata mtu aje vipi, bado atakuwa ni walewale ambao wanaleta sanaa zao awali halafu mwishoni wanapotea.

Kwa kuzingatia hilo, nimeona ni vyema leo tukaangalia baadhi ya ishara ambazo ukiziona kwa mwanaume wako ujue kabisa huyo si muoaji bali ni mzugaji au tapeli tu wa mapenzi. Yupo kwako kwa ajili ya maslahi fulani na baada ya muda atakuacha.

Ukiona mtu ambaye yupo kwako halafu hana muda na wewe zaidi ya kukuhitaji tu kwa ajili ya kujiburudisha, huyo anza kumtilia shaka. Tena kama mtu huyo anafanya hivyo kwa muda mrefu, jua kabisa ana kusudi lake binafsi na si pendo kwako.

Anakuwa hana habari na wewe zaidi ya kukuulizia pale anapohitaji jambo fulani, hana muda wa kujua umeshindaje, sijui unaishi vipi au pengine una tatizo gani mtu wa aina hiyo jua ni mzugaji. Ishi naye kwa tahadhari na ukiona anaendelea na maisha hayo, muepuke haraka.

Ukimuona mwanaume anakuwa muongomuongo, hana kauli moja katika maisha yenu hiyo pia ni dalili mbaya. Mwanaume ambaye ana nia thabiti ya kuwa na wewe, hawezi kuwa mjanjamjanja. Kama ni sanaa hizo atazifanya kwa watu wengine lakini si kwako.

Mwanaume ambaye anakufunga ‘kamba’ za waziwazi hata wewe mpenzi wake, unapaswa kuwa naye makini. Aina hiyo ya wanaume ni wale ambao wanakuwa na wewe kwa maslahi fulani. Yawezekana akawa anakuganda sababu ya pesa au maslahi mengine binafsi. Mwanaume ambaye sio muoaji atajifanya ni mpenzi wako lakini pia hapendi umjue sana. Hahitaji uingie kwenye maisha yake kiundani, mnakutana tu barabarani au hotelini biashara imeishia hapo. Hataki kukutambulisha kwa ndugu au hata marafiki. Ukimuona yupo hivyo, anza kuwa naye makini.

Wanaume matapeli mara nyingi huwa wanakuwa hawapendi sana kuzungumza mipango endelevu na watu wao. Mwanamke anapoanzisha tu habari hizo, anaruka fasta na kuchomekea mada nyingine. Hayupo tayari, hawezi kukuvumilia uanze kuzungumza habari za sijui kuwa na familia, kuwa na watoto na mambo mengine kama hayo.

Anataka mzungumzie zaidi viwanja vya starehe, kula raha na kumaliza mahitaji yake ya kimwili. Baada ya hapo, hana mpango tena na wewe. Atakutafuta pale atakapokuhitaji. Unapaswa kuwa makini na watu wa aina hii. Mwanaume anapokufuata, mchunguze taratibu kabla ya kuruhusu moyo wako uzame katika himaya ya penzi lake.

Ukiona haelekei na pengine ana tabia kama nilizoziainisha hapo juu basi chukua hatua haraka za kumuepuka. Tukutane wiki ijayo. Unaweza kunifauta kwenye mitandao ya kijamii, Instagram na Facebook natumia Erick Evarist, Twitter natumia ENangale.

Loading...

Toa comment