NI Jumatatu nyingine, tumejaliwa na Mwenyezi Mungu, nami nakukaribisha jamvini mdau tupate elimu ya mapenzi na maisha kwa jumla. Kama kichwa cha mada hii kinavyojieleza, kuna njia nyingi za kuweza kumteka mpenzi hasa mwanamke na kumfanya awe wako peke yako katika kipindi hiki chenye changamoto nyingi za usaliti.
Mpenzi msomaji, ili kujihakikishia upo peke yako kwa mpenzi wako wa kike au mkeo, kila siku hakikisha unamsifia kwa kumwambia ni kiasi gani alivyo mzuri. Kumbuka, kila mwanamke anapenda kusifiwa hivyo unapomwambia yeye ni mzuri, anaona unamthamini kuliko wanawake wengine wote. Kama hiyo haitoshi, wakati wowote ukipata nafasi, muandikie SMS kwenye simu, mweleze hisia zako ya kwamba ni kiasi gani unampenda. Kumbuka wanawake hupenda kusikia zaidi kutoka kwa wapenzi wao ni kiasi gani wanapendwa. Haitakiwi iwe tu katika kipindi cha siku ya wapendanao ndiyo umuoneshe kuwa unampenda, la hasha, muoneshe mwanamke wako ni kiasi gani yeye ni muhimu kwako.
Mfanyie mambo ya tofauti kama kumpiga busu la ghafla na kumshika mkono wakati mkitembea pamoja, hii itamfanya yeye kujisikia raha zaidi. Na wakati mwingine mshtukize kwa kumtembelea kazini au sehemu alipo mara kwa mara. Hii itamfanya akuone wewe ni mtu muhimu pale unapokuwa upo mbali na kumfanya kukuhitaji zaidi.
Ni vyema pia ukatambua mahitaji yake muhimu. Unatakiwa uwe msaada kwake, kipindi ambacho mpenzi wako amekasirika kuwa pale kwa ajili yake na ukimpooza kwa sauti ya upole na mahaba. Utashangazwa na kiasi gani msaada huo utakavyoleta mabadiliko kwake. Hakikisha unamsaidia katika shida zake. Hapa ndipo kuna tatizo kwa wanaume wengi. Mapenzi si pesa, lakini kuna kipindi ambacho pesa huhitajika kulinda penzi lako. Si mwanamke anapokuomba pesa ina maana ana nia ya kukuchuna au amekupendea pesa, kuna shida nyingine inabidi akuombe wewe, tena kwa kukupima kama utakuwa tayari kumsaidia.
Jambo lingine la kumteka mwanamke ni pamoja na kumtoa ‘auti’, mara nyingine itamfanya ajisikie furaha sana kwa sababu wasichana hupenda kufurahia maisha wakiwa na wenza wao. Hii haitamfanya mpenzi wako tu kuwa na furaha, bali itawafanya ninyi kwa pamoja kujuana na kufahamiana zaidi.
Katika mapenzi yenu kuwa muwazi kwake, usimfiche jambo linalokuhusu. Mwanamke hupenda kutoa ushauri kwa mtu ampendaye hivyo unapokuwa muwazi atajisikia kuthaminiwa nawe na kukuona umemuamini. Ukijiona upo bize sana, usithubutu kuacha japo kumpigia simu mara mbili kwa siku hata kama ukishindwa kumpigia wakati upo ofisini, darasani au kwingineko, hakikisha unapopata nafasi japo mtumie ujumbe mfupi wa kumwambia unampenda.
Mkumbatie mara kwa mara, kuna jambo kubwa sana hutokea. Si kwake tu, hata kwako. Hali ya joto lenu huwaweka pamoja kifikra hata pale msipokuwa pamoja. Epuka ugomvi na hasira za mara kwa mara ukiwa naye. Mwanamke hupenda ustaarabu kwa mtu ambaye yupo ‘siriaz’ naye hivyo ukionesha hasira unaweza ukamkosa hivihivi kwani wanawake huwaogopa wanaume wenye hasira na wagomvi kwa sababu hupenda kubembelezwa.
Mwisho wa yote ni kumdekeza. Mwanamke anapenda kudeka na kubembelezwa hivyo mwanaume ukidekewa usikasirike eti huyu mwanamke kazidi, wewe ndiyo wakati wako wa kumuonesha mwanamke wako unampenda. Mdekeze hadi aone aibu kudeka siku nyingine. Wasichana wameumbwa kwa ajili ya wanaume ndiyo maana hudeka, hii ndiyo silaha pekee na ya mwisho kwa mwanamke.
Kwa maoni, nicheki kwenye namba hapo juu. Pia usikose kutembelea ukurasa wetu wa Gazeti la Ijumaa Wikienda kwenye Facebook.
Comments are closed.