The House of Favourite Newspapers

Jinsi Ya Kutengeneza Pesa Wakati ‘Vyuma Vimekaza’!- 02

0

WIKI iliyopita nilieleza kwa kina kwenye kipengele cha kubana matumizi kadiri uwezavyo. Kwenye makala haya ya jinsi ya kutengeneza pesa wakati huu ambao vijana wengi wameupa jina la ‘vyuma vimekaza’, leo nahitimisha kwa vipengele vinne vilivyosalia. Narudia kusema tena. Pesa inahitaji nidhamu kubwa. Achana kabisa na matumizi yasiyokuwa na lazima katika maisha.

 

Kama una tabia hiyo, nataka nikuhakikishie kwa wimo wa moyo kwamba hutafanikiwa wala kufika mahali popote kimaisha zaidi ya kuishi kama viumbe wengine wa mwituni, jambo ambalo ni kosa kubwa katika maisha ya binadamu awaye yeyote.

 

7: VIPATO VINGI

Upo msemo mmoja ambao kila nikiukumbuka huwa ninalazimika kuipa kazi ya ziada akili yangu. Waswahili wa huku Pwani wanasema: “Ni panya mjinga tu mwenye shimo moja la kuingia na kutokea nyumbani kwake.” Maana halisi ya msemo huo ni kwamba katika maisha hupaswi kuwa na njia moja tu ya kukuingizia kipato. Ni lazima utengeneze vyanzo vingi vya kukuingizia kipato.

 

Katika hili, hakikisha unaanzisha au kufungua miradi ambayo una uwezo na uzoefu nayo au kwa maneno mengine, anzisha biashara ambayo una uelewa nayo, usikurupuke kuanzisha miradi ambayo huna maarifa juu yake, eti kwa sababu tu kanuni ya maisha inasema ni lazima uwe na vyanzo vingi vya mapato, ukifanya hivyo utaishia kulia. Ukweli ni kwamba, kama kuna kosa kubwa ambalo unalifanya katika maisha yako ni kuwa na njia moja tu ya kuingiza kipato.

 

Hivi unawezaje kuishi maisha ya aina hiyo? Hebu fumba macho hapo ulipo kisha fikiria kwa kina kwamba siku inayofuata njia hiyo moja unayoitegemea kukuingizia kipato haitakuwepo, maisha yako yatakuwaje? Inahitaji akili iliyopanuka sana kupambana na maisha haya. Kama umeajiriwa kwa mfano, hakikisha unabuni biashara ambayo itakupa kipato kingine na ikiwezekana fanya zaidi ya chanzo kimoja.

 

Faida yake ni kwamba hutaishi kwa madeni na mshahara wako unakuwa na ulinzi mkubwa, kwani utakuwa unatumika kwa mambo mengine muhimu, zaidi ya kuishia kwenye kulipa madeni na kubangaizia chakula na mahitaji mengine ya ndugu huko kijijini.

 

Hivi kuna ubaya gani kama umeajiriwa, lakini ukatafuta vijana watatu waaminifu, mmoja ukampa mradi wa kutembeza mayai ya kuku wa kienyeji, mwingine mbogamboga kwenye beseni na wa tatu visheti, vitumbua au bagia na kuvipitisha mashuleni wakati wa mapumziko au majumbani kwa watu wenye uvivu wa kuamka na kutafuta vitafunwa mitaani?

 

Mwanzoni utaona kama umepoteza pesa, lakini faida yake ikianza kuingia inakuwa inakidhi mahitaji muhimu ya kimaisha na wala hutakuwa unaulizia allowance (posho) na tarehe ya mshahara, kwa upande wako maisha yanakuwa yanakwenda huku wengine wakiendelea kulalamikia ugumu wa maisha wewe unapambana na maisha kwa vitendo huku ukimuomba sana Mungu akujalie hekima, busara na kiasi kwa kila ulitendalo. Kwa kufanya hivyo utaiona dunia hii ni pepo ndogo wakati
wengine wanalia.

 

8: NUNUA ZAIDI KULIKO KUUZA!

Hapa nitashangaza wengi. Kwa wafanyabiashara na matajiri wengi duniani, kanuni hii haitawashangaza, ni ya zamani na haijawahi kumuaibisha mfanyabiashara yeyote mwenye kuwaza mbali na boksi. Katika kipindi hiki watu wengi hufikiria kuuza vitu ili kukabiliana na maisha. Nataka nikueleze kwamba, katika kipindi ambacho unapaswa kununua vitu vingi ni kipindi cha ‘vyuma kukaza’. Maana yangu hapa ni nini? Faida ya kununua vitu vingi kwenye wakati mgumu ni moja, kwamba, ni akiba ya baadaye pale ‘vyuma vitakapolegeza’. Unajua, kuna jambo moja muhimu kuhusu pesa. Inapenda sana kuwekezwa kwenye vitu ambavyo matokeo yake vitazaliana maradufu. Yaani raha ya pesa ni kutafuta wenzake wengi.

 

Pesa huwa inaona fahari sana kuongeza wenzake na humpenda sana mtu anayeiwekeza ili iwaite wenzake wajazane mifukoni na kwenye akaunti, hiyo ndiyo kanuni ya pesa, ukiiheshimu na kuitunza, hakika utaikimbia kwa wingi wake, mapenzi yake kwa waijuao thamani yake huwa ni makubwa mno na ndiyo maana huwezi kusikia watu kama Dk Reginald Mengi, Bakhresa, Mfuruki, Kishimba na wengine wengi wamefilisika, japokuwa inaweza kutokea mara chache. Sababu ya wao kuendelea kuwa matajiri ni nini? Wanaiheshimu pesa na wanaitafutia njia nyingi zaidi za kuzaliana. Wananunua vitu vingi vya muhimu wakati mgumu ili baadaye waviuze kwa faida kubwa zaidi, hiyo ndiyo akili ya biashara na pesa.

 

9: BIDII KATIKA KAZI

Hapa ndipo kwenye mzizi wa mafanikio. Huwezi kufanikiwa kama hufanyi kazi kwa bidii. Tena ngoja niweke MKAZO: “Fanya kazi kwa bidii zaidi kuliko
kawaida.” Kama ni mwajiriwa, hakikisha unafanya kazi kwa kiwango, hata kama kuna ugumu kiasi gani kiuchumi, kampuni au serikali haitakubali ikuache uondoke, itakukumbatia kwa kukuongezea maslahi kwa sababu bidii yako ni muhimu kwa ustawi na ufanisi. Kama ni mfanyabiashara, achana kabisa na ubosi! Hiki ni kipindi ambacho mambo yanatakiwa yaende kinyumenyume! Kama ulizoea kuamka saa tatu, sasa ni wakati wa kuamka saa kumi na moja! Fanya kazi zaidi ya mazoea. Haijalishi wewe ni tajiri kwa kiwango gani. Katika kutafuta kwangu habari za watu waliofanikiwa ili iwe chachu kwangu na kwako, nimegundua kuwa hata Bill Gates wakati mwingine kabla hata ya wafanyakazi anaowalipa mishahara minono.

 

Donald Trump, kupitia kitabu chake cha Make it Happen in Business and Life; anasema kwamba bidii inalipa. Trump hulala saa tatu tu kila siku, muda mwingi huutumia kufanya kazi na hii ndiyo sababu kubwa iliyomfanya ajitengenezee ofisi kila mahali alipo. Ana ofisi nyumbani, kwenye magari, ndege, helikopta na maeneo mengine kila anapokuwepo kwa muda mrefu, anapenda kufanya kazi na ndiyo maana huwa haoni nongwa kujisifia mbele za watu akisema: “I’m very rich and I’m rich because I work very hard.” (Mimi ni tajiri sana na niko hivyo kwa sababu ninafanya kazi kwa nguvu sana). Willie Jolley, katika kitabu chake cha It Only Takes A Minute To Change Your Life, aliandika: “Work hard as much as you can, but remind you, someone is there watching you.”

 

(Fanya kazi kwa nguvu kadiri ya uwezo wako wote, lakini kaa ukijua kwamba kuna mtu mahali anakutazama). Amka alfajiri, kama ni muumini wa dini f’lani, ukishasali, pata muda kidogo wa kusoma kitabu kuhusu maisha, fanya mazoezi ya viungo na baada ya kuoga, nenda kazini. Haijalishi umeajiriwa au ni mfanyabiashara, kafanye kazi zaidi ya ilivyokuwa jana, fanya kazi kwa bidii kama siku hiyo ndiyo ya mwisho wa wewe kuishi. Nakuhakikishia kwa kufanya hivyo, Gladness, Joshua, wewe Japhet unayesoma hapa, nazungumza na wewe Revocatus, sijakuacha Joyce na wala sijakusahau Agness, ni lazima utafanikiwa na maisha yako yatakuwa mengine kabisa na usishangae ukianza kusikia maneno mitaani wakikuita ‘Freemason’ kwa kufanikiwa wakati huu wa ‘vyuma kukaza’. Maisha ni kanuni, ukizipatia tu umeula. Endelea na mapambano. Songa mbele. Lenga parefu zaidi. Jipange kwa mapinduzi makubwa. Kamwe usipaki gari na kumngoja mtu atakuja kukusukuma, haitatokea. Badili mtazamo kuhusu maisha na utafurahia na kuvuna matunda, wakati ukifika na kusahau kabisa mtiririko wa jasho na wingi wa tabu na magumu yachoshayo moyo, hayo ndiyo maisha.

 

10: SAIDIA SANA

Hii inawawia vigumu wengi kwa kipindi hiki. Kwamba mtu atoe shilingi mia tano au elfu mbili kumpa mtu! Utasikia “kwa usawa huu?” Ndugu zangu, jambo la kusaidia halina usawa mgumu na laini. Saidia kwa kiwango ambacho unacho, lakini usiishiwe kabisa. Akina Cristiano Ronaldo, Mengi, Bakhresa, Sabodo na wengine wengi wanaosaidia wanazidi kutajirika kwa sababu kusaidia ni moja ya kanuni ya kufanikiwa. Toa bila kukumbuka na pokea bila kuacha kushukuru, maisha yanahitaji nidhamu mno. Saidia kwa kipindi hiki. Saidia wazazi, ndugu na jamii inayokuzunguka, pale jambo hilo linapokuwa ndani ya uwezo wako na kwa kufanya hivyo maisha lazima yanyooke.

 

JALI AFYA YAKO!

Ingawa wanasema ugonjwa haukimbiwi, lakini hakikisha unaepuka mazingira ambayo yanahatarisha afya yako. Nenda hospitali ukapime afya mara kwa mara na kudhibiti magonjwa ambayo yakiachwa yanaweza kuwa sugu hivyo kuondoa kabisa furaha yako ya kimaisha hata kama una bidii kiasi gani katika kufukuzia mafanikio. IMARISHA

 

UHUSIANO WAKO NA MUNGU

Hapa ndipo penyewe. Hapa, ohooo ndipo penyewe ndugu yangu. Nina swali dogo sana. Unapumua kwa uamuzi wako mwenyewe au hujikuta tu ukipumua? Sasa kama umebabaika na swali dogo kama hilo, unapata wapi jeuri ya kujitenga mbali na Mungu? Acha mambo yako, jikite sana katika kuimarisha uhusiano wako na Mungu. Namalizia kwa kukusisitiza tena, kama kuna mahali ulihitilafiana na Mungu, tafadhali sana mrudie na ukapige magoti na unyenyekee kwa wimo wa moyo. Asubuhi omba, mchana fanya maombi na usiku liite jina lake kwa sauti kuu ipitayo matamshi yote, vinginevyo yatakupata makubwa, mimi naishia hapa.

 

Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine ya kutengeneza pesa. Kwa maoni na ushauri, nicheki kwa namba hizi; 0673 42 38 45

Leave A Reply