The House of Favourite Newspapers

Jinsi ya kutibu tatizo la kutopata ujauzito

0

pregnancy-test-120305Tatizo la kutopata ujauzito, ugumba kitaalamu linaitwa ‘Infertility’. Hili lipo kwa mwanaume na mwanamke. Uchunguzi wa ugumba hufanyika katika hospitali ya mkoa kwa daktari wa akina mama. Vipimo vipo kwa mwanaume na mwanamke na vinakuwa tofauti.

Tunaposema ugumba ni kwamba watu wawili mke na mume wanatafuta mtoto kwa mwaka mzima bila mafanikio.

MATATIZO KWA MWANAMKE
Mwanamke mwenye tatizo la kutoshika mimba anaweza kuwa na matatizo kwenye mfumo wa homoni kiasi kwamba mayai hayazalishwi au hayapevuki, mzunguko wa hedhi kuvurugika na matiti kutoa maziwa wakati hana mimba wala hanyonyeshi.

Tatizo la kutopata ujauzito pia linaweza kusababishwa na maambukizi sugu katika viungo vya uzazi kunakosababishwa na magonjwa ya zinaa, kuharibika mimba mara kwa mara.

Kuharibika kwa mimba kunaweza kusababishwa na aidha mimba kuharibika kwa bahati mbaya au kwa makusudi na mwanamke anakuwa na dalili mbalimbali kama kuumwa na tumbo chini ya kitovu kwa muda mrefu au mara kwa mara.

Maumivu haya ya chini ya tumbo yanaweza kuwa katikati au kuelekea kushoto au kulia chini ya tumbo. Wakati mwingine mwanamke hulalamika maumivu makali wakati wa hedhi, maumivu wakati wa tendo la ndoa au kutokwa na uchafu ukeni unaoambatana na muwasho.

Mwanamke mwenye matatizo haya hulalamika kutokupata ute wa uzazi unaoashiria upevukaji wa mayai, hajielewi jinsi mzunguko wake unavyokwenda, hupoteza hamu na raha wakati wa tendo la ndoa.

Uchunguzi wa tatizo hili ni vipimo mbalimbali kama vipimo vya Ultrasound, vipimo vya damu kuangalia maambukizi na mfumo wa homoni au vichocheo vya uzazi, vipimo vya ukeni kuangalia kama kuna tatizo gani linaloathiri uzazi au maambukizi.
Mwanamke pia atafanyiwa vipimo vya mirija kuangalia endapo kama mirija ya uzazi imeziba au ina tatizo lolote.

Matatizo ya mirija ya uzazi ni kama vile kuziba mirija kutokana na athari za maambukizi au makovu ya ndani kutokana na upasuaji wa mirija au kizazi katika kuondoa uvimbe.
Maambukizi kama ‘PID’ na makovu husababisha viungo vya uzazi na vingine katika sehemu ya nyonga kushikamana. Maambukizi ya mirija husababisha mirija kujaa maji au mirija kujaa usaha.

Dalili kuu ya matatizo haya ni maambukizi sugu chini ya tumbo. Vipimo vya mirija vitafanyika, kipimo hicho ni ‘HSG’ ambacho kitaonesha jinsi mirija kama ni mizima au imeziba na imeziba vipi.

Matibabu ya matatizo ya uzazi kwa mwanamke hutegemea na uchunguzi, mfano kama ni maambukizi, basi dawa za antibayotiki zitatolewa kadiri daktari atakavyoona inafaa. Matatizo katika mfumo wa homoni pia yana tiba yake kulingana na kiwango cha upungufu huo.

Uzibaji wa mirija pia una njia zake za kuzibua kutegemea na uzibaji. Uwepo wa uvimbe ndani ya kizazi na kwenye vifuko vya mayai pia ni tatizo kubwa ambalo matibabu hutolewa kutegemea na jinsi ulipo na ulivyo na dalili zinazoambatana na uvimbe huo.

USHAURI
Matatizo ya uzazi kwa mwanamke ni tatizo kubwa linaloathiri mfumo mzima wa maisha ya mwanamke kimwili na kisaikolojia. Unashauriwa katika hali hii umuone daktari anayehusika na matatizo ya uzazi katika hospitali ya mkoa kwa uchunguzi na tiba.

Leave A Reply