The House of Favourite Newspapers

JINSI YA KUZUIA U.T.I KWA WATOTO

UGONJWA wa mfumo wa mkojo kitaalamu Urinary Tract Infection (U.T.I) umekuwa ukisumbua watu wengi. Leo tutazungumzia ugonjwa huu kwa watoto wadogo.  Vimelea vinavyosababisha ugonjwa katika mfumo wa mkojo hukua na kusambaa endapo kinga ya mwili inakuwa ndogo hivyo makundi yaliyo katika hatari ya magonjwa haya ni pamoja na watoto chini ya miaka mitano. U.T.I ni ugonjwa unaoathiri njia ya mkojo na husababisha maumivu makali mwilini. Ugonjwa huu hutokea pale mlango wa njia ya haja ndogo inaposhambuliwa na bakteria. Bakteria hawa wasipotibiwa mapema huenea hadi kwenye figo na athari zake zinaweza kuwa mbaya zaidi.

Ugonjwa huu hutibika kwa dawa nyingi jamii ya vijiuasumu (antibiotic). Baadhi ya dawa hizo ni tetracycline, ampicillin, Ciprofloxacin, Cefalexin, Cefadroxil, clavam, Fosfomycin, Monurol, Furadantin, Sulfam ethoxazole, co-trimax, ampicillin, gentamicinn na nyinginezo. Mzazi/mlezi kumbuka kutokutumia dawa hizo pasipo maelekezo ya daktari. Mlezi au mzazi anaweza kuzuia maambukizi ya ugonjwa huu kwa watoto wadogo kwa kufanya yafuatayo: Hakikisha unakuwa na matumizi sahihi ya dawa za kuzuia bakteria (antibiotics) kwa watoto pale unapoandikiwa na mtaalamu wa afya.

Matumizi yasiyo sahihi ya dawa hizi yanaweza kumuweka mtoto katika hatari zaidi ya kupata maambukizi. Pale unapoandikiwa dawa hizi hakikisha unampa mtoto kwa wakati husika na dozi sahihi na usizidishe muda wa matumizi bila ushauri wa daktari. Pia hakikisha mtoto anakunywa maji mengi kwa siku kulingana na umri wake. Mtoto wa miaka mitatu na kuendelea anashauriwa kunywa maji glasi sita mpaka nane kwa siku ili kuepuka upungufu wa maji mwilini (dehydration).

Njia sahihi ya kumsafisha mtoto wa kike sehemu za siri ni kutoka mbele kwenda nyuma ili kuepuka kusambaza bakteria wa njia ya haja kubwa maarufu kama normal flora ambao kwa kawaida wakitoka katika njia ya haja kubwa kwenda katika njia ya mkojo wanasababisha ugonjwa katika mfumo wa mkojo (U.T.I).

Kwa mtoto ambaye ameanza kunawa mwenyewe hakikisha unamfundisha njia sahihi ya kunawa ili kuepuka maambukizi. Kwa mtoto wa kiume hakikisha anatahiriwa mapema ili kuepusha hatari ya maambukizi ya ugonjwa huu na kwa yule ambaye hajatahiriwa bado hakikisha unamsafisha ndani ya ngozi ya uume wa mtoto mara kwa mara kuepuka kukua kwa bakteria katika mfumo wa mkojo.

Ikiwa mtoto ameanza kunawa mwenyewe hakikisha unamfundisha njia sahihi ya  unawaji. Pia epuka matumizi ya sabuni kali zenye kemikali kwa mtoto ambazo zinaweza kusababisha muwasho unaoweza kusababisha michubuko katika sehemu za siri hali inayorahisisha maambukizi ya vimelea vya magonjwa ya mfumo wa mkojo (U.T.I).

Hakikisha mtoto havai nguo zinazombana sana katika maeneo ya siri kwa kumvalisha nguo zinazoruhusu hewa kupita ili kuzuia joto na unyevunyevu unaoeneza mazingira mazuri kwa ukuaji wa vimelea vya magonjwa katika mfumo wa mkojo. Vilevile hakikisha mtoto anakojoa mara kwa mara na hakai na mkojo kwa muda mrefu.

USHAURI

Kama mtoto atakuwa na dalili ya ugonjwa wa mfumo wa mkojo kama vile homa, maumivu wakati wa kukojoa, mkojo wenye mawingu na unaotoa harufu kali, mpeleke mapema katika kituo cha afya na hakikisha unatumia kwa usahihi dawa alizoandikiwa.Usitumie dawa zozote bila ushauri wa daktari.

Comments are closed.