Jitihada za Serikali Ujenzi wa SGR Zaungwa Mkono na Benki ya DCB, Chalamila Apongeza
Katika kuunga mkono juhudi zilizofanywa na serikali inayoongozwa na Samia Suluhu Hassan za ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR pamoja na kukuza utalii kupitia Royal Tour, Benki ya Biashara ya DCB imedhamini safari ya walimu zaidi ya 1000 kutumia treni ya SGR kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro na kisha Mikumi ili kukuza utalii wa ndani na kujifunza mambo yatakayowasaidia wanafunzi wao wawapo madarasani.
Akizungumza katika hafla ya kuwaaga walimu hao kutoka Jiji la Dar es Salaam, katika Stesheni ya SGR, jijini humo jana, Mkurugenzi Mtendaji wa DCB, Bw. Sabasaba Moshingi alisema taasisi yao imeshirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo kuwapa nafasi walimu hao kutembelea mbuga za wanyama ya Mikumi ili kujionea vivutio vya utalii vitakavyowasaidia kuwafundisha wanafunzi wa mashuleni.
Alisema DCB inamilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ambalo ndiko wanakotoka walimu hao hivyo akawashauri kutumia huduma zilizoboreshwa za benki hiyo kama vile kuweka amana, bima mbalimbali na mikopo yenye masharti nafuu ili kuboresha maisha yao na kuacha kuangukia katika taasisi zinazotoa mikopo inayowaumiza na yenye masharti magumu.
Naye Mkurugenzi wa Biashara wa benki hiyo, Bw. Ramadhan Mganga alisema DCB ndio mkombozi halisi wa watanzania kwani wanazo huduma na bidhaa tofauti zinazokidhi mahitaji ya kibenki ya watanzania hivyo kutoa hamasa kwa walimu hao na kwa watanzania kwa ujumla kuchangamkia huduma hizo.
Aidha alisema ili kufanikisha safari hiyo wamedhamini mabasi 30 yatakayowasafirisha walimu hao kutoka Morogoro kwenda Mikumi ikiwa pia ni kutambua mchango wa walimu hao katika maendeleo ya benki yao.
Awali akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Albert Chalamila aliipongeza DCB Kwa kufanikisha safari hiyo ya walimu akisema ofisi yake itaendelea kuandaa safari kwa makundi mengine ikiwa ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa kuitangaza treni ya SGR.
“Ziara hii sio tu itaongeza maarifa kwa walimu kupitia ziara ya Mikumi, bali pia itaongeza chachu ya kampeni inayoendelea ya Royal Tour,” alisema.
Benki ya Biashara ya DCB ilianzishwa mwaka 2002 ikitokana na wito wa Rais wa awamu ya tatu, Hayati, William Benjamin Mkapa, kufuatia kilio cha mitaji cha wananchi wenye kipato cha chini na cha kati wa Jiji la Dar es Salaam kukosa mikopo katika benki nyingi za kibiashara kwa kutokidhi vigezo vilivyokuwa vikiweka na benki hizo.