The House of Favourite Newspapers

Joan Wicken: Mwingereza Aliyekuwa Msaidizi wa Nyerere

Joan (kulia) akiwa na Nyerere na Malkia Elizabeth na Uingereza.

Na WALUSANGA NDAKI| RISASI JUMAMOSI| NAJUA UNAJUA

ALIKUWA ni mama kutoka Uingereza.  Ni marehemu Joan Wicken aliyekuwa msaidizi binafsi wa Mwalimu Julius Nyerere tangu mwaka 1964 hadi alipoondoka madarakani 1985. Joan aliyekuwa na digrii ya falsafa, siasa na uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Somerville, Oxford, Uingereza, alikutana na Nyerere miaka ya 1950 huko Uingereza na Mwalimu akapendekeza aje Tanzania asaidie kutafuta fedha za kujenga chuo kwa ajili  ya wafanyakazi jijini Dar es Salaam.

Alipokuja nchini, mama huyo aliyekuwa muumini wa Usoshalist (Ujamaa) alikataa kukaa nyumba za vigogo maeneo ya Oysterbay na kadhalika, akaamua kukaa kibanda kidogo huko Mgulani katika Jeshi la Wokovu, kila siku akienda ikulu kwa pikipiki aina ya Vespa,
akisema kuishi maisha ya anasa ni kinyume na Ujamaa.

Pamoja na kuwezesha kujengwa chuo cha wafanyakazi – ambacho leo ni Chuo cha Kivukoni – alikuwa pia mwandishi wa hotuba za Mwalimu Nyerere, akajipikia chakula chake kwenye jiko la mafuta ya taa (jiko la Mchina) na akajishonea nguo zake kwenye cherehani aliyokuwa nayo.

Alikuwa ni mmoja wa wasiri wakuu wachache wa mipango ya serikali ya Nyerere.  Alishirikiana na Mwalimu hadi kifo chake alipoamua kurejea Uingereza baada ya kukataa eneo alilopewa kuishi kijijini Butiama.  Alifariki kwa numonia huko Uingereza akiwa na umri wa miaka 79. Joan alikuwa moja ya nguvu kuu zilizompa Nyerere heshima nchini na duniani japokuwa hakufahamika kwa Watanzania wengi.

 

Save

Comments are closed.