Johan Borgstam, Mjumbe Maalum wa Umoja wa Ulaya (EUSR) kwa Mkoa wa Maziwa Makuu, ametembelea Tanzania kuanzia tarehe 10 hadi 13 Machi 2025, ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika nchi za Afrika Mashariki.
Borgstam amekutana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Veronica Nduva, pamoja na wawakilishi wa kidiplomasia na mashirika ya kijamii.
Majadiliano yao yamejikita katika hali ya kiusalama Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ambapo mgogoro unaendelea kutokana na shambulizi la M23, ambalo linadaiwa kuungwa mkono na Rwanda. Borgstam ametaka kusitishwa kwa mapigano na kuchukuliwa hatua za haraka kimataifa ili kutatua mgogoro huo wa kibinadamu.
Borgstam amepongeza juhudi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na SADC katika kutafuta suluhu za kikanda. “Umoja wa Ulaya unahofia sana kuongezeka kwa migogoro katika Mashariki ya DRC. Tunalaani vikali ukiukwaji wa haki za binadamu na tunasisitiza haja ya kupatikana kwa suluhu ya kudumu,” alisema.
Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Christine Grau, alisema ziara ya Borgstam inathibitisha umuhimu wa Tanzania katika juhudi za kumaliza mgogoro huo na kuimarisha usalama katika eneo la Maziwa Makuu.