The House of Favourite Newspapers

John woka amekufa na mashairi yake kichwani

0

Makala: OJUKU ABRAHAM

MICHAEL Dennis Muhina maarufu zaidi kama John Woka amefariki dunia alfajiri ya Jumanne wiki hii na kwa mara nyingine, kuipa pigo kubwa sanaa ya muziki wa Kizazi Kipya nchini.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana, marehemu alifariki dunia baada ya kupata ajali ya kulipukiwa na mtungi wa gesi wa gari alipokuwa katika matengenezo na baadhi ya vyuma kumchoma kichwani. Inadhaniwa kuwa damu ilimwagikia katika ubongo.

Nilizungumza na kaka mkubwa wa marehemu, anayezaliwa kwa mama mkubwa, Omary Saidi ambaye alisema msiba uliwekwa Ilala Bungoni, nyumbani kwa baba yao mdogo na mazishi yangefanyika Sahare, Tanga, katika siku ambayo hadi makala haya yanaandikwa, haikufahamika.

Lakini John Woka hasa ni nani? Kwa mashabiki wa Bongo Fleva wa miaka ile ya katikati ya 2000, watakuwa wakimtambua kama mmoja kati ya wasanii waliokuwa na uwezo mkubwa wa kutuma ujumbe kwa jamii kupitia muziki, hasa staili yake iliyompatia mashabiki kibao.

Kilichompatia umaarufu ni staili yake ya kuimba huku akiigiza sauti ya kilevi, lakini iliyokuwa ikitoa maneno yenye mantiki, kiasi cha kujikusanyia mamia ya mashabiki kila alipokwenda katika shoo mbalimbali ndani na nje ya nchi.

John Woka alifanya kazi na wasanii wengi wakiwemo Wagosi wa Kaya, lakini zaidi alikuwa ni mshirika mkubwa wa msanii wa Reggae, Gerald Simba aliyefahamika zaidi kama Ras Lion.

Moja kati ya kazi maarufu zaidi alizofanya na Ras Lion ni vibao vilivyotingisha sana, Hii Kitu na Hodi Mganga ambazo zilipokelewa vizuri na kupata ‘airtime’ ya kutosha katika vituo vingi vya redio enzi hizo.

Aliwahi pia kufanya kazi na Keisha iitwayo Nikikupata na pia akiwa na Ras Lion walimshirikisha mkongwe Mike Tee katika ngoma iliyoitwa Bitozi. Kazi nyingine aliyofanya na swahiba wake huyo mkubwa kimuziki iliitwa Yalaa na ile ambayo nayo ilisumbua sana, iliyojulikana kama Umasikini Huu.

Kwa jinsi John Woka alivyokuwa ‘aki-flow’ katika muziki wake na hata katika baadhi ya video za nyimbo hizo, msanii huyo aliipatia vizuri nafasi yake ya

uigizaji wa kilevi, kama ambavyo mwigizaji maarufu wa vichekesho, Masele anavyofanya.

John Woka anaondoka akiwa bado mdogo mno, lakini mashairi yaliyo kichwani mwake yakiwa yanahitajika sana, hasa katika kipindi ambacho vijana wengi wanaotamba katika Muziki wa Kizazi Kipya wanaimba zaidi mapenzi, badala ya nyimbo zinazozungumzia mafunzo, hadhari na hata tamaduni za Kiafrika.

Woka alikuwa msanii kupitia nyimbo zake, aliweza kuwapa mashabiki vitu zaidi ya kimoja, kwanza angewavunja mbavu mashabiki kwa vituko vyake vya ‘kilevi’ kabla ya kuwapa somo kwa mashairi yake!

Leave A Reply