The House of Favourite Newspapers

JOKA LA JABU LATIKISA DAR

DAR ES SALAAM: Patashika nguo kuchanika! Ndivyo unavyoweza kusema kufuatia joka linalodaiwa kuwa la ajabu kuonekana mara kwa mara na kuzua taharuki maeneo ya Kinondoni- Shamba, jijini Dar.

 

Kwa mujibu wa shuhuda, joka hilo linalosemekana kuwa ni aina ya chatu, linadaiwa kuonekana kwenye bwawa kubwa linalozunguka eneo hilo la Kinondoni-Shamba.

“Yani hili lijoka ni la ajabu maana linatokea likiona mtu mmoja wakiongezeka tu linatoweka kimaajabu,” alisema mmoja wa mashuhuda.

 

Akizungumza na Risasi Jumamosi hivi karibuni, bibi aliyejitambulisha kwa jina la Prisikila Mmari, ambaye anaishi jirani zaidi na bwawa hilo, alisema amekuwa akiishi maisha ya hofu tangu amshuhudie kwa macho nyoka huyo akijirusha kwenye maji baada ya kuibua kichwa chake nje na kukirudisha bwawani.

 

“Unavyoniona mimi hapa siwezi kukaa nyumbani kwangu hapa peke yangu hata siku moja kama wajukuu zangu hawapo na mimi naondoka sikai kabisa na nimekuwa nikiogopa sana kila ninapokuwa nyumbani kwangu hapa maana sasa nimekuwa kama mkimbizi, naogopa hata kwangu na wala taa usiku hatuzimi kabisa,” alisema bibi huyo.

 

Akiendelea kuzungumza nyoka huyo aliyedai kuwa ni wa ajabu, bibi huyo alisema awali katika bwawa hilo kulikuwa na vyura wengi wanalia kutokana na maji hayo lakini sasa hivi hakuna vyura hivyo wanahisi nyoka huyo atakuwa amewala vyura hao na ndio hawasikii kelele zao.

 

“Zamani kulikuwa vyura  sana, wanalia usiku kucha lakini toka nimuone nyoka huyo hakuna chura hata mmoja, bwawa liko kimya kabisa kitu ambacho kinazidi kuniogopesha maana kama kamaliza vyura atakuja nyumbani kwangu sasa aingine ndani,” alisema bibi huyo.

Bibi huyo alisema aliwahi kutoa taarifa kwa mwenyekiti wa serikali ya mtaa wake ambapo walifika watu wake kuangalia lakini hakuna kichofanyika. “Hakuna kilichofanyika hata kunyonya haya maji yaishe hata kama watamuona wajue jinsi ya kumuua lakini wapi,” alisema.

 

Mmoja wa wajukuu wa bibi huyo anayeishi naye nyumbani hapo aliyejitambulisha kwa jina la Allen, alisema hata yeye alishamuona nyoka huyo akiwa kwenye maji akitikisa magugu ya kwenye bwawa hilo ambapo baada ya kumuona alitoa mbio na kwenda kumuita bibi yake na waliporejea hawakumuona.

 

Risasi Jumamosi lilifika mpaka katika Ofisi za Serikali ya Mtaa wa Kinondoni- Shamba na kuzungumza na mwenyekiti aliyejitambulisha kwa jina la Chau George Timbuka ambaye alikiri kuwa wameshapata taarifa hizo na wakatoa taarifa kwa mamlaka ya wanyama.

Alisema baada ya kutoa taarifa na mamlaka hiyo kuahidi kushughulikia, yeye na maofisa wenzake walienda mpaka eneo kushuhudia.

 

“Ni kweli bibi alikuja na kutupa taarifa hizo na mimi nilizifisha kwa mamlaka husika kisha nikaenda mpaka sehemu yenyewe na kuangalia mazingira ya pale hivyo bado tunalifanyia kazi na tutalipatia uvumbuzi hivi karibuni,” alisema mwenyekiti huyo.

STORI: Imelda Mtema  Risasi Jumamosi

Alichozungumza Balozi wa Switzerland Maadhimisho ya Wiki ya Uchoraji

Comments are closed.