The House of Favourite Newspapers

Jokate Awataka Yanga Kujaza Taifa Waiue Simba

0
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, Jokate Mwegello.

MMOJA wa wapenzi maarufu wa Yanga ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, Jokate Mwegello, amewataka wapenzi wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati watakapopambana na watani wao wa jadi, Simba.

 

Mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambao Yanga ndio watakaokuwa wenyeji, unatarajiwa kupigwa kesho saa 11:00 Jioni kwenye Uwanja wa Taifa. Ikumbukwe katika mchezo wa mzunguko wa kwanza baina ya timu hizo uliisha kwa sare ya mabao 2-2.

 

Simba waliongoza kwa mabao 2-0 kabla ya Yanga kupambana na kuchomoa yote ndani ya dakika saba. Akizungumza na Championi Jumamosi, Jokate alisema Yanga watashinda mchezo huo wa Jumapili kutokana na ubora wa kikosi chao.

“Sina wasiwasi na timu yangu ya Yanga, naamini itashinda tu mbele ya Simba, niwaombe mashabiki wa Yanga wajitokeze kwa wingi uwanjani wakiwa wamevaa jezi za timu yetu ili wawape morali wachezaji wetu waweze kupambana na kupata ushindi,” alisema Jokate aliyeitikisa fani ya urembo mwaka 2006, ikidaiwa ndiye aliyestahili kutwaa taji la Miss Tanzania badala ya aliyepewa ushindi.

 

Aliongeza kuwa, kwa kauli mbiu ya Yanga kuelekea mchezo huo ni vaa kibingwa, basi kila shabiki avae jezi ya mchezaji wa timu hiyo anayempenda ili kunogesha siku hiyo wakiwa kama wenyeji wa mchezo.

 

“Kwa sasa nipo kwenye ziara huku vijijini, ila natamani niwepo uwanjani siku hiyo, lakini hata kama nikishindwa kwenda, najua vijana wetu hawataniangusha, tutashinda tu,” alisisitiza.

 

Kwa upande wake, Meneja Masoko na Mawasiliano wa GSM Group, Matina Nkurlu, alisema wametengeneza jezi za kutosha ili kila shabiki wa Yanga aweze kupata na kwenda nayo uwanjani Jumapili kushuhudia pambano hilo.

 

“GSM tunafahamu mvuto wa mchezo huo, na tukiwa kama wadhamini wa Yanga na watengenezaji rasmi wa jezi za klabu hiyo, tumehakikisha tunatengeneza jezi za kutosha zenye ubora wa hali ya juu ili kukidhi mahitaji ya Wanayanga.

 

“Jezi zimeshaanza kuuzwa katika maeneo mbalimbali na zaidi maduka ya GSM yaliyopo Mlimani City, Pugu Mall, Lumumba na kwingineko hivyo kila shabiki wa Yanga ahakikishe ananunua jezi halisi (original) ya Yanga na kuepuka kununua zile za mitaani ambazo hazina maslahi yoyote na klabu yao,” alisema.

 

“Jezi zetu zipo katika ubora wa hali ya juu unaolingana na hadhi klabu ya Yanga. Niwaombe Wanayanga wasikubali kununua jezi za mitaani ambazo ni za wajanja wachache ambao wamekuwa wakipiga fedha kwa kupitia nembo ya Wanajangwani hao.”

Leave A Reply