JOKATE YAMKUTA YA AMINA CHIFUPA
SIKU tatu baada ya Mwanamitindo Jokate Mwegelo kuteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, gumzo la aina yake limeibuka kumhusu mrembo huyo kitendo ambacho kimeshabihiana na mambo yaliyomtokea marehemu Amina Chifupa aliyekuwa mbunge wa kuteuliwa. Jokate aliteuliwa Julai 28, mwaka huu baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli kufanya mabadiliko ya wizara, mikoa na wilaya.
MITANDAO YAANZA KUMUANDAMA
Mara baada kuteuliwa, mijadala mbalimbali iliibuka mitandaoni kwa watu kuonesha kumkubali lakini wengine wakionesha kutomkubali kutokana na nafasi yake aliyokuwa nayo awali ya uanamitindo. Waliokuwa wanamkubali, walijenga hoja kuwa mrembo huyo ana ujasiri, ana hekima na anaweza kumsaidia rais katika nafasi hiyo ya ukuu wa wilaya kwani kupitia taasisi yake ya Kidoti, ameshafanya mambo makubwa kwenye jamii.
“Huyu Jokate mnamuona hivi tu lakini mimi nawaambia ni mtu ambaye anajua kusimamia vitu, ana hekima na busara hivyo jukumu la ukuu wa wilaya naamini kabisa anakwenda kulitendea haki. “Unajua hata mheshimiwa mwenyewe hadi kufikia hatua ya kumteua, ameona mbali kwa mrembo huyu hivyo kamwe hawezi kumuangusha,” alichangia mdau aliyejitambulisha kwa jina la Ibra katika mtandao wa Instagram.
HOJA YA WALIOMKOSOA
Waliokosoa wengi wao walisimamia hoja ya upole wa Jokate na kudai kwamba pengine anaweza kushindwa kuwakemea watumishi ambao watakuwa chini yake. “Unajua kasi ya JPM bwana sasa hivi ni mwendo wa maagizo na kusimamia mambo yaende kwa haraka sasa nikimtazama Jokate namuona kama mpole hivi,” alichangia mdau mmoja mtandaoni aliyejiita Kije.
MJADALA WAZIDI KUTAWALA
Mwanamitindo huyo alizidi kujadiliwa na kutazamwa zaidi katika mtandao wa YouTube ambapo kwenye kila video ya uteuzi wake iliyowekwa na akaunti mbalimbali za mtandao huo, ilionekana kutazamwa na watu wengi zaidi kuliko wateule wengine walioteuliwa na rais siku hiyo.
Mbali na kutazamwa, watu ‘walikomenti’ maoni mbalimbali kwa kila mmoja kuweka maoni na mtazamo wake juu ya Jokate huku wengine wakikumbushia safari yake ya kisanii na hata kisisiasa akiwa Umoja wa Vijana Kitengo cha Chipukizi katika Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kuhusu wale waliompinga, mchambuzi mmoja wa masuala ya masuala ya kisiasa aliyeongea na Uwazi, alisema kinachomtokea Jokate ni sawa na kilichomtokea marehemu Amina Chifupa lakini anaamini atakuja kufanya vizuri na kuwashangaza Watanzania.
“Unajua Amina alipoteuliwa mwaka 2005 kuwa Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Dar es Salaam akitokea kwenye utangazaji akiwa mrembo watu waliona labda pengine Umoja wa Vijana (CCM) walikosea kufanya uteuzi huo bila kujua kwamba waliona kitu kwake na baadaye akaja kuwashangaza.
“Walianza kumsema sana, wakamponda wee, wakamzushia mambo kibao lakini mwisho wa siku mambo yakaja kuwa tofauti. Amina alikuja kuonesha makucha yake baadaye kwamba ni jasiri, mchapakazi na mtu ambaye aliibua na kukemea suala zima la madawa ya kulevya ambalo lilikuwa ni tatizo kubwa nchini ambalo lilihusisha baadhi ya vigogo serikalini,” alisema mchambuzi huyo na kuongeza:
“Mimi nafikiri tumpe muda tu Jokate, mimi naamini kabisa huyu binti atafanya mambo makubwa sana katika nafasi yake na ninamtabiria anaweza kufika mbali sana kisiasa endapo atazidi kujipambanua katika siasa kwani nguvu ya ushawishi anayo.”
NGAWAIYA AMPA TANO
Naye mbunge wa zamani wa Moshi Vijijini, Thomas Ngawaiya akizungumzia uteuzi huo, alisema rais anachagua vijana zaidi katika nafasi mbalimbali kutokana na kuwa na nguvu ya kufanya kazi kwa masaa mengi bila kuchoka na wengi wao wana elimu ya juu hivyo kutomuangusha. “Rais ana imani kubwa na vijana sababu anaamini wanaweza kufanya kazi kwa saa nyingi na pia wengi hawajamuangusha hivyo amezidi kuwapa nafasi na mimi naona ni jambo jema,” alisema Ngawaiya.
UTEUZI WA JERRY MURO NAO WAIBUA MANENO
Mbali na Jokate, uteuzi wa aliyewahi kuwa msemaji wa Timu ya Yanga, Jerry Muro ambaye amekuwa Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, nao uliibua maneno huku wengi wakidai kuwa huenda mwanahabari huyo akawa na yale maneno ya ‘shombo’ ya kimpira katika nafasi hiyo.
Lakini hata hivyo, wengine waliochangia kwenye mitandao ya kijamii walisema Jerry anaweza kufanya vizuri katika nafasi hiyo kwani safari yake ya uanahabari na kisiasa, imeonesha ni mzalendo wa kweli na mtu mwenye kupenda haki itendeke.
Wengi waliochangia hoja hiyo walishibisha zaidi kwa kukumbushia sakata la rushwa kwa madereva na askari wa usalama barabarani alilofichua mwaka 2010 akiwa mwanahabari. Walisema ni mtu ambaye aliichukia rushwa, jasiri, alijitoa muhanga kuhakikisha anakomesha tatizo hilo na kweli matunda yalionekana kwa kurusha picha za madereva wakitoa rushwa na kupokelewa na askari wa usalama barabarani.
Akizungumza na mwanahabari wetu siku moja kabla ya kuteuliwa kushika wadhifa huo, Jerry alisema amekuwa akiwasaidia sana wananchi wa kijijini kwake Machame, Moshi. “Kwa kweli nimekuwa pamoja na wananchi wa kijijini kwangu, nafarijika kuona nawasaidia kwa hali na mali, na ndio maana ng’ombe wangu wakizaa huwa natoa ndama kwenye vikundi vya akina mama,” alisema Jerry.
Stori: MWANDISHI WETU, Dar
Comments are closed.