The House of Favourite Newspapers

Joshua kurudiana na Ruiz Saudi Arabia

 

PAMBANO  la marudiano kati ya Andy Ruiz Jr na Anthony Joshua litafanyika mwezi Desemba mwaka huu nchini Saudi Arabia, promota wa Joshua, Eddie Hearn, amethibitisha.

Kumekuwa na tetesi kuwa Ruiz Jr hayupo tayari kwa pambano hilo, lakini Hearn amesema kuwa mabondia wote wawili wamesaini kucheza mpambano huo Desemba 7 mwaka huu.

Ruiz aliushangaza ulimwengu wa masumbwi kwa kumchakaza Joshua mwezi Juni na kutawazwa kuwa bingwa wa dunia. Bingwa huyo mpaka sasa hajawaarifu chochote mashabiki wake kupitia mitandao ya kijamii kuhusiana na mpambano huo wa marejeano toka ulipotangazwa siku ya Ijumaa. Mkufunzi wake, Manny Robles amesema “kuna sababu inayomfanya” Ruiz kukaa kimya.

“Mabondia wote wawili wameshatia saini. Vyombo vya usimamizi (wa ndondi) vimeshaarifiwa,” amesisitiza Hearn. Katika mkutano na wanahabari, ambao, hata hivyo, si Joshua wala Ruiz ambaye alihudhuria, Hearn alitangaza kuwa mpambano huo utafanyika katika uwanja wa wazi katika kitongozji cha Diriyah, nje kidogo ya jiji la Riyadh.

Omar Khalil, ambaye anafanya kazi na Serikali ya Saudia katika kuandaa pambano hilo pia ametangaza kuwa wote watakaonunua tiketi za mpambano huo moja kwa moja watakuwa wamepewa viza ya kuingia nchini humo. Upande wa Ruiz uliweka wazi kuwa usingekubali kucheza pambano la marejeano nchini Uingereza huku upande wa Joshua ukitaka pambano hilo lichezwe nje ya Marekani.

“Tulipata ofa kutoka Saudi Arabia, Abu Dhabi, Dubai na Qatar,” alisema Hearn na kuongeza: “Tulitaka kwenda sehemu ambayo wana maono ya mbali na mchezo wa masumbwi. Tulijua Saudia inamaanisha na imewkeza kwenye mchezo huu.  Inabidi tutambue kuna ulimwengu mwingine nje ya Uwanja wa Cardiff na Madison Square Garden. Tunalazimika kukuza mchezo huu katika maeneo mengine duniani.”

Ruiz, alimpoka Joshua mikanda ya IBF, WBA na WBO Juni mosi baada ya kumuangusha mara nne kabla ya mpambano huo kukatishwa na mwamuzi. Mkataba unamlazimisha kucheza pambano la marudiano, na awali ilidhaniwa kwa ukimya wake labda hajasaini pambano hilo. Kuna wanaodhani kuwa ukimya wa Ruiz unatokana na kudai kitita kikubwa zaidi ya alichopewa awali.

Pambano hilo linatarajiwa kuingiza pesa nyingi, mpaka sasa inaarifiwa kuwa waandaaji nchini Saudia wametoa dola milioni 40, na bado hapo kuna kitita cha watakaolipia watazamaji kwenye runinga hakijajumuishwa. Waandaaji nchini Saudia wanasema nchini mwao kuna hamu kubwa ya matukio kama hayo kutokana na uhalisia kuwa 70% ya wananchi milioni 40 ni vijana chini ya miaka 24.

Hata hivyo, makundi ya kutetea haki za binaadamu yanapinga vikali kuandaliwa kwa mpambano huo humo wakidai kuwa matamasha ya michezo na burudani yanatumiwa na serikali ya kifalme kuonyesha kuwa nchi hiyo imebadilika na kuwa ya kisasa ilhali haki za binadamu zinaendelea kuvunjwa kila uchao.

Comments are closed.