Joto la Mapenzi – 40

ILIPOISHIA:

“Jinsi ya kuishi si tatizo, la muhimu ni nyinyi kutubariki, ni kweli mmemfanyia kitu kibaya hasa baba kwa kweli kitendo ulichokitenda ni kibaya sana si cha kibinadamu.  Alitaka kulipa kisasi cha kuuawa baba yake.”

“Nani kamwambia nimemuua baba yake? Yule mzee si amekufa kwa ajali.” Mzee Mtoe aling’aka.

“Baba ni wewe ndiye uliyemuahidi atakufa na baada ya muda mfupi ulimtuma mtu akamuua kwa kumgonga na gari.”

“Ndivyo alivyokudanganya mpumbavu mwenzako, basi mwambie haniwezi na yeye nitampoteza kama baba yake,” mzee Mtoe alijisahau na kumwaga siri nje japo alikataa.

“Haya baba unakataa nini unasema nini?”

“Kwani nimesemaje?”

“Baba acha roho mbaya, ni wengi umewapoteza kwa siri, lakini kila chenye mwanzo kina mwisho.”

“Sasa unanitisha, ningejua ningekuacha akafia jalalani kuliko kuleta balaa nyumbani kwangu.”

“Hata mimi usinitishe, sikukutuma unichukue ni kiherehere chako,” Koleta aliropoka.

“Wee, Koleta kuwa na adabu unajua unazungumza na baba yako?” mama Koleta aliingilia kati.

“Najua nazungumza na baba, lakini hawezi kunifanyia aliyonifanyia kwa kunidanganya kuwa mpenzi wangu ameoa kumbe uongo wake ili tu niolewe na mtu mwingine, bado kamuua baba wa mpenzi wangu kwa ajili yangu hiyo haikutosha alimfunga mpenzi wangu kwa kumtengenezea kesi ya uongo.”

“Sawa, lakini unatakiwa kumheshimu baba yako, ni zaidi kuliko huyo Ambe, unaweza kuolewa na mwanaume yeyote lakini baba yako atabakia huyu.”

“Ambe naweza kusema ni zaidi ya baba yangu kwa vile amejitolea kuokoa maisha yangu ambayo baba alikuwa tayari yapotee.”

“Sasa nasema huyo Ambe nikimuona hapa namuua kwa risasi.”

“Baba huwezi, si unakumbuka kilichompata mzee Samjo?”

“Si amekufa kwa presha?”

“Mnajidanganya, basi yule mzee alikuwa na tabia kama zako, rafiki ya baba Junior waliosema amekufa kumbe hakufa naye alifungwa kama alivyofungwa  Ambe. Na ndiye aliyemtorosha mpenzi wangu baada ya kuiba bunduki kumbe baba Junior wala hata hiyo bunduki alikuwa hajaishika.

“Yule rafiki wa baba Junior aliiba ile silaha ili aje alipe kisasi, baada ya kutoka kuna sehemu wameishi zaidi ya mwaka na nusu bila kuonekana ndipo walipokuja kulipa kisasi katika watu hao na wewe ulikuwemo. Walimvamia na kumlazimisha kusema ukweli tena mbele ya watumishi wa Mungu kuwa amemuua baba wa rafiki wa baba Junior na kudhuluma mali zake. Baada ya kusema ukweli ule alipatwa na presha na kufa.Baada ya kutoka huko walikuja hapa ili kukutia adabu lakini kwa vile baba Junior ananipenda nimembembeleza sana asikufanye kitendo kibaya japo ilikuwa kazi kubwa lakini alinielewa na kumuomba niwaombe mkutane naye mumuombe radhi tuanze upya.

“Lakini nafika hapa mnanitoa akili, hivi nikimruhusu afanye anavyotaka baba huchukui hata siku mbili utabakia jina.”

“Sasa wewe utafurahi baba yako akifa?” mama yake aliuliza.

“Kwa mtindo huu nitapiga na vigelegele,” Koleta alijibu kwa kujiamini.

“Mama Koleta si unamsikia mwanao.?” Baba Koleta alisema.

“Koleta ni maneno gani hayo?”

“Baba kanikosea mangapi nimekaa kimya? Sema mama hata wewe ulifika wakati ukamshangaa.”

“Lakini bado ni baba yako.”

“Sasa sijapata jibu, mpaka sasa mmeamua nini juu ya baba Junior?”

“Mwambie sina jibu,” mzee Mtoe alijibu kwa mkato.

“Kwa hiyo nimjibu hivyo baba Junior?”

“Baba Koleta punguza hasira jambo hili ni zito tunatakiwa kuwa wavumilivu hasa tukizingatia sisi ni wazazi. Kwa nini turudishe mambo ya nyuma, kumbuka tuliteseka sana baada ya Koleta kutoroka. Tulitulia baada ya kumpata na kumpa kila kitu kizuri ikiwa ni pamoja na kumsomesha mjukuu wetu shule nzuri.

“Ni ukweli ulio wazi Koleta na Ambe wanapendana sana, kumbuka Ambe hakuogopa chochote alipokuwa akimtaka mwenzake. Pia Koleta bado anampenda mzazi mwenzake, kama wapenzi waliopoteana miaka zaidi ya nane leo hii penzi bado motomoto ni wakati mwingine wa kujirudisha chini ili tuweze kufanikisha kiu ya mtoto wetu. Wakati mwingine wazazi huwasikiliza watoto wao japo wamewazaa,” mama Koleta alimweleza mumewe aliyekuwa amefura kwa hasira.

“Nimekusikia mke wangu lakini mwanao kanivunjia heshima sana leo, nimempa vitu vingapi? Hata kama baba yake nikifa leo nakufa maskini kwa kumpa kila kitu mwanangu na mjukuu wangu. Bado haoni umuhimu wangu kwake.”

“Umuhimu wako kwangu ni kuniunganisha na mzazi mwenzangu, zaidi ya hapo vyote ulivyofanya ni bure.”

“Sawa nimekuelewa,” mzee Mtoe alijibu kwa sauti ya chini.

“Kwa hiyo?” Koleta aliuliza.

“Mwambie aje siku mtakayotutaarifu tupo tayari kumpokea kama mkwe wetu,” mama Koleta alisema.

“Lakini jamani chondechonde siyo aje hapa mumuitie polisi, jamani patakuwa hapatoshi.” Koleta aliwatahadharisha wazazi wake.

“Basi inatosha tumekuelewa,” mama Koleta alisema.

“Nashukuru wazazi wangu kwa kunikubalia kumleta mzazi mwenzangu, pia napenda kuomba radhi kwa kuwakoseeni heshima.”

“Tumekusamehe mtoto akinyea mkono huukati bali utausafisha.”

“Nashukuru kwa hilo.”

“Na huyo mwenzako bado mkristo?” mama yake aliuliza.

“Alirudi kwenye dini yake.”

“Sasa itakuwaje?”

“Atakavyoamua mwenyewe.”

“Hata kukubadili dini?”

“Sitakuwa na kipingamizi.”

“Huoni hilo ni tatizo.”

“Si tatizo, alikuja kwenye dini yetu tukashindwa kumpokea, nitambembeleza arudi dini yangu ili tufunge ndoa lakini akikataa sitakuwa na budi kumfuata kwa vile huu ni muda wangu wa kumuonesha namjali kama alivyonijali yeye nina wasiwasi safari hii nitaingia mimi gerezani au kunyongwa.”

“Kwa nini unasema hivyo?”

“Bado siamini kama roho za wote zimekunjuka, baba anaonekana hajakubaliana nami.”

“Amekubaliana nawe si lazima aseme.”

“Asiposema nitajuaje, mbona kwenye kukataa alisema?”

“Nimekubali,” alisema mzee Mtoe.

“Itoke moyoni si mdomoni, itajulikana kwa vile shuka haifuniki moto.”

“Nimekubali mwanangu toka moyoni yote yaliyopita si ndwele tugange yajayo.”

“Asante wazazi wangu,” Koleta aliwakumbatia wazazi wake kwa kukubali kuonana na mzazi  mwenzie.

 

***

Siku ya pili Koleta alirudisha majibu kwa mpenzi wake kuwa amekubaliwa akutane na wazazi wake na wako tayari kumuomba msamaha.

“Mbona kama umekuwa rahisi sana kuna ukweli juu ya uliyosema?” Ambe alikuwa na wasiwasi na majibu ya mpenzi wake.

“Ni kweli baba alikuwa hataki lakini nimelazimisha ndiyo amekubali.”

“Amekukubali kukuridhisha au kweli?”

Je, nini kitafuatia? Usikose wiki ijayo kwenye gazeti

Toa comment