visa

Joto la Mapenzi – 41

ILIPOISHIA

Siku ya pili Koleta alirudisha majibu kwa mpenzi wake kuwa amekubaliwa akutane na wazazi wake na wako tayari kumuomba msamaha.“Mbona kama imekuwa rahisi sana kuna ukweli juu ya uliyosema?” Ambe alikuwa na wasiwasi na majibu ya mpenzi wake.“Ni kweli baba alikuwa hataki lakini nimelazimisha ndiyo amekubali.” “Amekukubali kukuridhisha au kweli?”

Endelea Nayo…

“Nina imani kwa yote niliyomwelezea kama atakwenda kinyume atakuwa hana moyo ya kibinadamu.”

“Sikiliza Koleta, kama baba yako atakwenda kinyume hata wewe sitasita kuwaueni kwa mkono wangu.”

“Hawezi.”

“Kwa kauli yako kuna walakini, kwa vile nakupenda nitakuja lakini bado simuamini baba yako. Anaweza kunizidi akili lakini atakufa kabla sijafa,” Ambe alimtahadharisha mpenzi wake.

“Mpenzi niamini sitakupoteza nipo radhi kupoteza chochote duniani lakini si wewe.”

“Hata mwanao?”

“Mtoto anapatikana lakini mume ni bahati hasa kumpata mwenye mapenzi ya kweli kama wewe.”

“Basi waambie wazazi wako wiki ijayo tutakuwa wageni wao ila kosa lao moja nyumba yenu itakuwa uwanja wa damu.”

“Haitatokea hata siku moja na hapa nikitoka nitaenda kuwasisitizia wasiende kinyume na makubaliano yetu.”

Baada ya makubaliano Ambe alikutana na Mabina kuzungumzia aliyoambiwa na mpenzi wake.

“Ambe tuwe makini maneno ya mpenzi wako yana walakini.”

“Hata mimi nimeyaona.”

“Basi tuwe makini.”

“Kwa hiyo unanishauri tusiende?”

“Twende lakini tuwe makini sana, wasiwasi wangu huenda mzee akatuendea kinyume.”

“Huo wasiwasi ninao huoni kama tutakuwa tumejiingiza wenyewe mikononi mwa serikali?”

“Tusiwe waoga, twende litakalotokea tutajua hukohuko.”

“Lakini tusiende kikondoo.”

“Hilo linajulikana, hakikisha bastola ile tunaipata,” Mabina alimkumbusha rafiki yake.

“Tena umenikumbusha nitampigia simu.”

“Ipo hiyohiyo moja au zipo nyingine?”

“Nitamuuliza.”

“Kama zipo zaidi ya moja itakuwa vizuri siku ya kwenda pale kila mmoja awe na yake kiunoni ili likitokea tuweze kujiokoa kwa pamoja kuliko kutegemeana.”

“Hakuna tatizo.”

Baada ya makubaliano Ambe alimpigia simu mpenzi wake Koleta.

“Haloo,” upande wa pili ulipokea.

“Haloo.”

“Nani?”

“Mpenzio.”

“Baba Junior?”

“Ndiyo.”

“Hii simu yako?”

“Hapana nimeazima ili niwasiliane na wewe.”

Siku zote Ambe alimkatalia mpenzi wake kuwa hana simu, pamoja na kuwa naye bado hakumuamini kwa asilimia mia kwa kuhofia huenda akabanwa na kuwapa namba yake ya simu ambayo ingemkamatisha.

“Ulikuwa unasemaje honey?”

“Nilikuwa na shida na ile bastola.”

“Ya nini tena baby?”

“Nina shida nayo muhimu sana kabla ya kuja kuonana na wazazi wako.”

“Baby si ungesubiri mpaka tumalize shughuli yetu?”

“Nitaifanya baada ya shughuli yetu.”

“Basi nitakupa tukimaliza shughuli yetu.”

“Hapana naitaka kabla.”

“Mmh! Sawa sasa unaitaka lini?”

“Hata kesho.”

“Hakuna tatizo ukija utaikuta, ila naomba kesho tuwe pamoja mpaka siku itakayofuata.”

“Hakuna tatizo, chochote ukitakacho kwangu nipo radhi.”

“Nashukuru mpenzi wangu ndiyo maana nakupenda sana.”

“Eti mpenzi mzee ana silaha moja tu?”

“Mmh! Nina imani anazo kama tatu.”

“Naweza kupata mbili?”

“Mpenzi mbili za nini?”

“Zina umuhimu wake nikimaliza kazi yake utanisifu.”

“Lakini kweli ile mliichukua na kuirudisha bila kutumika risasi hata moja.”

“Hatuchukui kwa ajili ya kuua bali kuwatisha watu.”

“Mmh! Sawa, kesho nitakuletea zote, fedha je?”

“Niletee.”

“Shilingi ngapi?”

“Milioni moja.”

“Nitakuletea tano.”

Baada ya makubaliano ambayo Mabina naye aliyasikia, Ambe alimuuliza mwenzake.

“Nina imani mambo yatakwenda bambam.”

“Tena sana, kuna kitu kinanichanganya sana.”

“Kitu gani rafiki yangu?”

“Mapenzi ya demu wako ni makubwa sana, kama angekuwa magumashi yule mzee wake ilitakiwa tumzime mara moja tufanye kazi zingine.”

“Ni kweli hata mimi ananichanganya sana.”

“Lakini akitugeuka utanilaumu.”

“Kwa nini?”

“Mkono wangu nikiunyoosha hautarudi mtupu.”

“Kwa hilo wala usiwe na wasi hata mimi bado nina hasira na yule mzee. Nakuapia hata asipofanya chochote lakini lazima nimuue kwa mkono wangu.”

“Na mpenzi wako itakuwaje?”

“Hawezi kujua.”

“Basi tujipange kuhakikisha hatufanyi makosa.”

Baada ya makubaliano ya marafiki wawili, Koleta naye alikuwa akizungumza na mama yake.

“Mama mbona simuamini baba.”

“Kwa nini?”

“Kauli yake ina walakini, huoni anaweza kunigeuka?”

“Hawezi mwanangu.”

“Mamaa, asifike siku hiyo ikawa historia mbaya kwetu?”

“Wala mwanangu kila kitu kitakwenda kama kilivyopangwa.”

“Kwa hiyo akija baba mwambie watakuja wiki kesho ila narudia chondechonde mama baba asinigeuke. Ya awali niliyavumilia lakini haya sitakubali nitakuwa tayari hata kunyongwa.”

“Kwa hiyo unataka kumuua baba yako?”

“Kama atamuua baba Junior sitamuacha nami nitamuua.”

“Mwanangu kupenda gani huko kiasi cha kumchukia baba yako hivyo?”

“Mama mliyomfanyia baba Ambe na leo yupo tayari kuwasikiliza lazima muone aibu, halafu aje hapa mumgeuke sitakubali hata kidogo nitakufa na mtu.”

“Hatutamgeuka mwanangu.”

“Kama itakuwa hivyo nitashukuru, lakini..Mmh! Sisemi kitu ilaaa, siongezi kitu lakini wazazi wangu siku hiyo mtanisamehe.”

Baada ya mazungumzo Koleta alirudi chumbani kwake kulala na kumuacha mama yake akiwa katika wakati mgumu sana hasa kutokana na tabia za mumewe za ubishi. Kama mumewe angemsikiliza tangu mapema wala yote hayo yasingetokea. Alipokuwa akitaka kumgeuka Ambe alimweleza mumewe lakini alimkatalia.

Je, nini kitatokea? tukutane wiki ijayo.

JIUNGE NA GLOBAL BREAKING NEWS!
Toa comment