The House of Favourite Newspapers

Joto la Mapenzi – 44

0

ILIPOISHIA…

“Mama unasema kweli?”

“Nimemsikia kwa masikio yangu akiwaeleza waje, kumbe aliwaeleza watakuwa wapo wawili na wakimshika mpenzi wako watamtesa ili amtaje mwenzake.”

“Mama sikubali, namfuata.”

ENDELEA NAYO…

 

“Mpango wa kumtorosha mpenzi wako.”

“Sasa mama tutafanyaje?”

“Tufanye ufumbuzi wa haraka kabla polisi hawajaingia.”

“Tutaweza?”

“Hata sijui.”Walishtushwa na sauti ya mzee Mtoe, walikatisha mazungumzo na kutoka chumbani alipowaona alijifanya kuchangamka:

“Jamani, naona mtu na mwanaye mnateta.”

“Kawaida tu baba,” Koleta alijibu.

“Mbona umemuacha mkwe  peke yake?”

“Si yupo anazungumza na mwanaye.”

“Sasa jamani tufanye tulichokipanga ili tufanye kazi zingine.”

“Lakini baba ukinigeuka patakuwa hapatoshi humu ndani,” Koleta uvumilivu ilimshinda.

“Kukugeuka vipi mwanangu?”

“Nasikia umewaita polisi wamkamate mpenzi wangu?”

“Mimi?”

“Eeh! Wewe.”

“Mke wangu wewe ndiye uliyemwambia uongo huo?”

“Wala si uongo ni kweli.”Wakiwa katikati ya mabishano mlango ulifunguliwa na kuingiza askari sita wenye nguo za kawaida kila mtu mkononi alikuwa na bunduki nzito.

“Wote chini ya ulinzi,” ilikuwa sauti ya juu iliyoongozwa na askari mmoja aliyekuwa na bastola mkononi. Wote waliwekwa chini ya ulinzi pamoja na Ambe ambaye alijilaumu kwa kukamatwa kizembe namna ile.

“Baba umetimiza ulichotaka kukifanya,”

Koleta alilalamika huku akimwaga machozi.

“Mwanangu si mimi utanionea bure,” Mzee Mtoe alijitetea huku akimwaga chozi la kinafiki.Askari kwa haraka sana walimvamia  Ambe na kufunga pingu na kumlaza chini na kuanza kumpekua na kumkuta na bastola kiunoni.

“Umeona jambazi hili kumbe limekuja na silaha.”

“Si nilimwambia mwanangu akabisha kuwa mchumba wake ni jasusi”

“Mzee baadaye nakutaka kituoni kwa maelezo ya jambazi hili.”

“Baba mpenzi wangu si jambazi kamuua nani? Mabaya yote uliyomtendea leo unamlipa haya,” Koleta alilia sana.Koleta alisema huku akimshika shati baba yake na kumtikisa bila kudhani yule ni baba yake mzazi.

“Koleta mwanangu utanionea bure muulize hata mkuu wa polisi kama mimi ndiye niliyetoa taarifa za kukamatwa kwake.”

“Muongo mkubwa mnafiki mbona yako huyapeleki polisi, kwa nini umekuwa na roho kama shetani, mume wangu wewe ni kiumbe gani usiyetaka kushaurika,” mama Koleta naye uzalendo ulimshinda.

“Mke wangu nimefanya nini?”

“Umewaita polisi tena nimekusikia kwa sikio langu, sasa mtoto wa watu kashikwa utapata faida gani?”

“Jamani makosa yake ya mauaji na kutoroka gerezani nimemtuma mimi na kudhihirisha hilo amekutwa na bastola kama siyo muuaji ni nani?”

“Baba kumbuka nilikuahidi nitalipa kwa yote uliyoyafanya.”

“Utaniua bure mwanangu, nilikueleza toka mwanzo huyu si mwanaume ona leo yupo katika mikono ya sheria siamini kama atapona lazima atanyongwa tu.”

“Wewe endelea kumchafua mpenzi wangu lakini kabla hajafa utakufa wewe,” Koleta alimtolea uvivu baba yake.

“Nani ataniua?” Mzee Mtoe aliuliza.

“Utaona mwenyewe, huwezi kuniumiza mara mbili leo ilikuwa siku kubwa maishani mwangu kumbe ndiyo siku ya kuupasua moyo wangu kwa kisu butu bila ganzi.

“Mama nioneshe baba yangu huyu si baba yangu na kuanzia leo sitakaa katika nyumba hii.”

“Utanilaumu bure huyu si bwana sahihi mwanangu.”

“Sasa mzee sisi tutaondoka na huyu maelezo mengine, kwa vile tuna kazi naye mpaka asubuhi tutakuwa tumempata na mwenzake.”

“Hakuna tatizo.”Baada ya kusema vile Ambe alinyanyuliwa alipokuwa amelazwa chini akiwa amefungwa pingu mikono kwa nyuma. Walipoanza kumtoa nje Koleta alijizoa alipokuwa amekaa akilia na kwenda kumvamia mtu aliyemshika Ambe na kuanguka chini wote watatu. Mmoja wa askari alimshika Koleta kwa nguvu ili awaache wampeleke mtuhumiwa nje kwenye gari.

“Baba yaani umeridhika Ambe apelekwe polisi? Mama mwambie baba nitakachokifanya hatasahau mpaka tunakutana kwa Mungu.”

“Jamani mbona umesimama mpelekeni kwenye gari muda umekwenda si mnajua tuna kazi nyingine nzito ya kumsaka muuaji mwenzake,” alisema jamaa aliyekuwa na bastola mkononi.Jamaa mmoja alimshika Ambe kwa nyuma na kumnyanyua ili amtoe nje, ghafla umeme wa nyumba nzima ulizimika, haikupita muda sauti za maumivu zilisikika ikiwemo ya mzee Mtoe na mkuu wa polisi aliyetoa amri vijana wake wote walale chini kwa sauti ya maumivu makali.

“Jamani laleni chini tunakufa.” Ilikuwa kitendo cha dakika tano, baada ya hapo palitanda ukimya mzito, mkuu wa polisi akiwa mwenye maumivu makali ya bega lililopigwa risasi alijivuta hadi kwenye mlango na kufanikiwa kutoka nje bila kizuizi na kupiga simu kituo cha polisi ambao walifika eneo la tukio na gari zaidi ya kumi na askari zaidi ya hamsini na silaha nzito na kuizunguka nyumba ya mzee Mtoe na kuzuia magari yasipite eneo lile ili kudhibiti usalama na kuweza kumkamata mtuhumiwa. Walivamia nyumba ya mzee  Mtoe na kuizingira,  walitafuta swichi kubwa na kuwasha taa.Sebuleni walikuta askari wawili walikuwa wamekufa  kwa kupigwa risasi za kichwa, Mzee Mtoe alikuwa akiugulia maumivu ya risasi ya kifua. Koleta na mama yake walikuwa wamelala chini kwa kuingiza vichwa vyao chini ya meza kwa hofu ya kufa lakini Ambe  hawakuwemo mule ndani. Mzee Mtoe aliugulia maumivu ya kifua alichopigwa risasi huku akimlaumu mwanaye.

“Koleta mwanangu umeniponza.”

“Sijakuponza bali ubishi wako.”

“Bila wewe nisingeuawa.”

“Bila mimi vipi? Baba wewe ndiye uliyemfunga Ambe kwa hila na matokeo yake umemuua baba yake bado huna huruma wewe ni mtu gani? Hata ukifa roho hainiumi.”

“Maneno gani hayo mwanangu?” Mama Koleta alimkanya mwanaye ambaye alionekana hana huruma na tukio la baba yake.

“Mama kilanga haliliwi wala hawekewi matanga ameyataka yamempata. Tena ningefurahi taa zingewashwa na kukuta amekufa. Ujinga wako umesababisha askari wa watu kuuawa na  mkuu wao kujeruhiwa. Kwa nini umeshindwa kuwa mkweli waeleze na wewe umedhulumu na kuua watu wangapi?” Koleta alisema kwa sauti ya hasira.

“Binti huyu si baba yako?” mkuu wa operesheni ya pili alimuuliza.“Si baba yangu,” alijibu kwa mkato.

“Wee Koleta kwa nini unamkana baba yako?”

“Siwezi kuwa na baba asiyekuwa na mapenzi na mtoto wake.”

“Koleta mwanangu nimekupa vitu vingapi leo unasema hivyo?” Mzee Mtoe alisema kwa shida.

“Ulichonipa umetoa kwa mapenzi yako lakini nilichokitaka amekuwa akikipiga vita, heri ninyongwe mimi si Ambe kwa sababu hana kosa lolote hajaua labda kutoroka gerezani tena kwa shinikizo na yote kasababisha baba.”

“Sasa binti nina imani wewe unajua mengi juu ya mtuhumiwa kwa hiyo tutaondoka na wewe kwa ajili ya mahojiano.”

“Nipo tayari,” Koleta alisema kwa kujiamini.

“Hapana afande huyo mwacheni msimpeleke popote kama makosa nimefanya mimi,” mzee Mtoe alimtetea mwanaye.

“Hapana lazima akaisaidie polisi lazima tumjue huyu jamaa ni mtu wa aina gani hawezi kutoroka pamoja na kuua vijana wetu.”   Kabla ya kuondoka ulifanyika upekuzi wa hali ya juu kila kona  kumtafuta Ambe bila mafanikio.

Je, nini kitaendelea? Fuatilia wiki ijayo siku ya Jumamosi.

Leave A Reply