Joto la Mapenzi – 45
ILIPOISHIA…
“Hapana lazima akaisaidie polisi, lazima tumjue huyu jamaa ni mtu wa aina gani hawezi kutoroka pamoja na kuua vijana wetu.” Kabla ya kuondoka ulifanyika upekuzi wa hali ya juu kila kona kumtafuta Ambe bila mafanikio.
ENDELEA NAYO…
Walichukua maiti za askari wawili na kumuwahisha mzee Mtoe na mkuu wa polisi hospitali kutokana na hali zao kuwa mbaya.
***
Baada ya Ambe kutangulia Mabina alitembea kwa miguu umbali mrefu mpaka kufika nyumba ya mzee Mtoe ambayo alishaifanyia uchunguzi tangu alipoelezwa na Ambe kuwa wanatakiwa kwa baba mkwe bila rafiki yake kujua.Siku moja kabla ya kwenda pale alikwenda hadi nje ya nyumba ya mzee Mtoe na kupokewa na mlinzi.
“Habari ndugu?”
“Nzuri.”
“Sijui wenyeji nimewakuta?”
“Mmh! Wazee hawapo wapo wasichana wa kazi.”
“Sasa nitaweza kuifanya kazi yangu?”
“Kazi gani?”
“Kuangalia vifaa vya umeme kwani sasa hivi kuna mabadiliko makubwa ya mfumo wa umeme ambao umekuwa na nguvu sana inayosababisha nyumba nyingi kuungua. Shida yangu ni kuangalia sehemu ya main swich kama iliyofungwa ni imara kama si imara mje muwaambie wabadili kabla hamjapata hasara kubwa.”
“Sasa sisi tutakuamini vipi pia mzee ametukataza kuingiza mtu ndani tusiyemjua.”
“Sina shida ya kuingia ndani bali kuona vifaa muhimu vya umeme, kwa sababu juzi tu kuna jumba kubwa zaidi ya hili mfumo mpya wa umeme wakati unafanya kazi bahati mbaya walifunga vifaa si imara. Jumba lote limeungua, sasa wewe jumba hili likiungua utafanya wapi kazi. Hivi ninavyokueleza nimemaliza nyumba zaidi ya ishirini na tano. Katika nyumba zote hizo ni nyumba tisa zenye vifaa imara na kuwaomba wote wabadili unafikiri kazi yenyewe ni kubwa ya dakika hata kumi hazifiki.”Maneno ya Mabina yalilainisha mlinzi aliyemsindikiza kuona mfumo wa umeme, baada ya kuuona alimwambia:
“Asante vifaa vyenu ni vizuri hamuwezi kupatwa na tatizo lolote.”
“Lo! Asante.”Mabina baada ya kuondoka aliamini kabisa hata siku wakija lazima waje usiku pia mafungu kwa Ambe kutangulia na yeye kumfanyia surprise ya kutokea katikati ya sherehe.Baada ya Ambe kufika pale Mabina alitembea kwa miguu baada ya kuteremkia sehemu ya mbali ambako aliacha pikipiki. Alitembea taratibu hadi eneo la karibu aliloshuhudia polisi waliokuwa na magari matatu yenye askari pia kulikuwa na askari mmoja aliyekuwa na simu mkononi kuonesha anawasiliana na mtu kuhusiana na wao.Hakwenda mbali sana alikwenda sehemu moja na kutulia kuangalie mwenendo wa askari waliokuwepo. Alijilaumu kutotumia simu kwani angeweza hata kumbumburusha rafiki yake. Baada ya muda polisi walikimbilia ndani na kuamini rafiki yake lazima atakuwa msambweni.Kwa haraka alitembea mwendo wa haraka hadi nyuma ya nyumba kisha alipanda ukuta na kutua ndani. Alinyata hadi sehemu ya dirishani na kuangalia ndani na kuweza kumuona rafiki yake akiwa amelazwa chini huku amefungwa mikono nyuma. Kwa vile main swichi haikuwa mbali na sehemu aliyokuwepo, aliwaangalia vizuri walivyokuwa wamekaa kwa shabaha ya ajabu baada ya kuzima taa aliachia risasi zilizowapata walengwa. Kwa haraka ya ajabu alikwenda sehemu aliyokuwa amelala chini Ambe na kumbeba hadi dirishani na kuzifungua pingu kwa risasi kisha waliteremka na kutorokea kwa nyuma kukimbilia alipoacha pikipiki na kutokomea kijijini kwao.
***
Koleta alishikiliwa na polisi kwa ajili ya upelelezi baada ya kufika polisi alihojiwa na mkuu wa upelelezi.
“Unaitwa nani?” mkuu wa upelelezi alimuuliza akiwa amemkazia macho.“Koleta.”
“Mzee Mtoe ni nani yako?”“Baba yangu.”
“Mzazi?”
“Ndiyo.”
“Na huyo muuaji?”
“Muuaji nani?”
“Huyo aliyetoroka.”
“Si muuaji.”
“Kwa nini unasema hivyo?”
“Hajawahi kuua hata nzi bali hila za watu.”
“Binti sisi si wajinga kumsaka, hujui kama alifungwa?”
“Najua.”
“Kwa kosa gani?”
“La kusingiziwa.”
“Kivipi?”
“Baba anajua.”
“Anajua nini?”
“Jinsi alivyomtengenezea hila ili afungwe kwa ukweli ulio wazi.”
“Ukweli upi huo?”
“Kamuua baba wa mpenzi wangu, alipokuja kuulizwa alimtengenezea mpango ulioonesha anataka kumuua na kusababisha afungwe bila kosa.”
“Gerezani hakutoroka?”
“Alitoroka kwa shinikizo la rafiki yake, mtu kabakiza muda mfupi atoke atoroke ili iweje?”
“Shinikizo hilo ni lipi?”Ilibidi Koleta auseme ukweli kama alivyoelezwa na Ambe sababu ya kutoroka, baada ya kumsikiliza walimuuliza.
“Kwa nini askari waseme yeye ndiye aliyetoroka na silaha?”
“Si nimewaeleza yote, hata kama leo tutakwenda askari aliyenyang’anywa silaha ana ukweli wote, mpenzi wangu hana hatia kwa vile alikuwa kwenye mkumbo lazima ataonekana amefanya kosa.”
“Nani kazima taa?”
“Nitajuaje wakati wote tulikuwa pamoja sebuleni.”
“Unajua haiwezekani taa izimwe kisha risasi wapigwe askari na baba yako tu.”
“Hilo swali siwezi kulijibu, mlitaka nipigwe mimi?”
“Kwa nini usilijibu?”
“Wote tulikuwa pamoja ukiniuliza mimi mtanionea, ungewauliza askari walioharibu sherehe yangu.”
“Mpenzi wako anakaa wapi?”
“Sijui.”
“Usitutanie binti, unajua kesi ya mauaji itakugeukia wewe kama utaficha ukweli.”
“Wala msinitishe, inamuhusu baba aliyejifanya mtakatifu machoni mwa watu kumbe muuaji mkubwa.”
“Sisi hiyo haituhusu tunataka utupeleke anapokaa mpenzi wako.”
“Sipajui.”
“Kwa usalama wako tunaomba utuelekeze alipo mpenzi wako bila hivyo kesi zote zake utazichukua wewe.”
“Wala msinitishe kila mtu atashtakiwa kwa kosa lake, nipelekeni huko mahakamani muone.”
“Sikiliza binti hatutaki kutumia nguvu tunataka utupeleke kwa mpenzi wako kwa hiyari yako.”
“Nilichowaeleza ni ukweli mtupu sijui zaidi ya kuonana naye hata nilipomueleza anipeleke anapoishi alikataa kwa kusema maisha yetu yatakuwa nje ya hapa, lakini zaidi ya hapo sijui lolote.”
“Binti usifanye utani leo utalala ndani ili kesho useme ukweli, kama unaendelea kuwa mbishi tutakufikisha mahakamani na kufungwa maisha.”
“Wala msisumbuke kusubiri kesho nipelekeni leo kwa vile sina jibu zaidi ya ukweli niliosema zaidi ya hapo ni kunilazimisha niseme uongo.”Koleta alipelekwa mahabusu kwa ajili ya siku ya pili ya mahojiano zaidi juu ya mauaji ya kujua Ambe yupo wapi.
***
Mama Koleta alikuwa amechanganyikiwa na hali iliyojitokeza muda mfupi, akiwa pembeni ya mumewe aliyekuwa na jeraha la risasi. Baada ya matibabu ya hali ya juu yaliyofanikiwa kutoa risasi, mzee Mtoe alipitiwa usingizi kutokana na sindano alizochomwa kwa ajili ya kusafisha jeraha.Akiwa amekaa pembeni ya mumewe huku mawazo yote yakiwa kwa mwanaye aliyepelekwa polisi. Ilibidi apige simu polisi kutaka kujua mtoto wake wamemfikisha wapi.
“Haloo baba mmefikia wapi?”
“Mwanao mbishi, kama ataendelea na ubishi huu ataozea gerezani.”
“He! Kwa kosa gani?”
“Kwa lililotokea chanzo ni yeye.”
“Baba huyo mwanangu na mambo hayo wapi na wapi?”
“Kwani muuaji ni nani yake?”
“Mzazi mwenzake.”“Sasa hataki kutupeleka alipo mpenzi wake.”
“Kwani anasemaje?”
“Anasema hajui lolote.”
Je, nini kitaendelea? Fuatilia wiki ijayo.