The House of Favourite Newspapers

Joto la Mapenzi – 46

0

ILIPOISHIA…

“Mwanao mbishi, kama ataendelea na ubishi huu ataozea gerezani.”

“He! Kwa kosa gani?”

“Kwa lililotokea chanzo ni yeye.”

“Baba huyo mwanangu na mambo hayo wapi na wapi?”

“Kwani muuaji ni nani yake?”

“Mzazi mwenzake.”“Sasa hataki kutupeleka alipo mpenzi wake.”

“Kwani anasemaje?”

“Anasema hajui lolote.”

ENDELEA NAYO…

“Ni kweli hajui lolote, naomba mumuachie kama kosa analo baba yake wala yeye hausiki na lolote.”

“Samahani mama usitufundishe kazi.”

“Haya tutaona mimi na ninyi nani anajua kazi asiporudi nyumbani usiku huu kesho utanitambua,” mama Koleta alikuja juu kusikia mwanaye kashikiliwa na polisi.

“Wewe mama kama nani?”

“Ili kujua mimi ni nani endelea kumng’ang’ania mwanangu na mkimlaza chini kesho na wewe utalala kama yeye mpuuzi mkubwa.”

“Mama askari wetu waliokufa umeona tumepoteza paka?”

“Mngemkamata aliyewaita si mwanangu.”

“Basi fanya lolote.”

“Kesho utaona nafanya nini, sizungumzi na kiroboto kama wewe.”

“Mama usitutukane nitakuja kukukamata.”

“Kabla hujanikamata utakamatwa wewe chawa mkubwa, na tena nakuhakikishia kesho itakuwa chungu maishani mwako.”

“Tutaona,” simu ilikatwa.Baada ya kukatwa simu, mama Koleta alipandwa na hasira na kumtazama mumewe aliyekuwa amelala  kitandani. Hasira zilimpanda  sana na kutamani kumzaba makofi kwa tabia zake za ubishi zilizosababisha  mtoto wake awekwe ndani na kuuliwa askari wawili. Alinyanyua simu na kumpigia rafiki ya mumewe mtu mkubwa serikalini, baada ya siku kuita ilipokelewa.

“Vipi shemeji mbona usiku?’

“Kuna tatizo.”

“Tatizo?”

“Ndiyo shemu.”

“Tatizo gani?”

“Baba Koleta yupo hospitali.”

“Hospitali! Kafanya nini?”

“Amepigwa risasi.”

“Wapi nyumbani au kwenye gari?”

“Nyumbani.”

“Mlivamiwa na majambazi?”

“Shemeji ni hadithi ndefu ila nilikuwa naomba msaada wako mmoja.”

“Upi huo?”

“Naomba mwanangu atoke mahabusu.”

“Mwanao nani?”

“Koleta.”

“Kafanya nini?”

Ilibidi amueleze kisa kwa kifupi, baada ya kumsikiliza alimwambia;

“Kwa nini wamemkamata?”

“Walisema wanakwenda kumuhoji juu ya mpenzi wake ambaye kwa kweli hajui lolote zaidi ya kukutana na kupanga kurudisha uhusiano upya. Lakini kama ujuavyo rafiki yako alivyo mbishi, tulivyokubaliana akaenda kinyume na matokeo yake kaponea tundu la sindano.”

“Nimekuelewa, basi atatoka sasa hivi, yupo kituo gani?”

“Cha kati.”

“Kwa heshima yako nitakwenda mwenyewe, naweza kumtuma mtu wakamtoa asubuhi.”

“Nitashukuru sana shemeji.”

 

Koleta akiwa amejilaza chini kwenye sakafu, moyoni alizidi kumchukia baba yake na kuuapia moyo wake angemfanyia kitu kibaya sana, kama akitoka labda aendelee kufungwa na kunyongwa kabisa japo aliamini hakuna hata ushahidi mmoja anaomtia hatiani. Akiwa amejikunyata na kukosa usinginzi kutokana na baridi kali la sakafuni alisikia akiitwa. Kutokana na hasira hakuitikia mpaka alipoitwa zaidi ya mara mbili.

“Koleta hebu nyanyuka ukalale kwenu.”Koleta alitoka nje na kukutana na rafiki ya baba yake aliyemchukua na kumrudisha nyumbani.

“Eti mama kwa nini unampenda muuaji?”

“Baba, mpenzi wangu si muuaji ni historia ndefu sana, ila Mungu atanilipia nitafurahi nikisikia baba amekufa.”

“Kwa nini unasema hivyo?”

“Yule si baba yangu, hawezi kila siku awe mtu anayeniumiza bila kunionea huruma.”

“Kwani ilikuwaje?”Koleta alimueleza kisa kizima kilichomuacha rafiki ya baba yake mdomo wazi.

“Mmh! Pole sana.”

“Asante, kuna faida gani ya kuwa na baba kama yule?”

“Lakini mwanangu baba ni muhimu kuliko mwanaume.”

“Na bila huyo mwanaume kujitoa muhanga, baba alikuwa tayari amekufa, nani muhimu kati yao?”

“Kumbuka mkubwa hakosei.”

“Sawa hakosei, kama  ningekufa nani angemuheshimu au kumsikiliza, tumekubaliana tumalize tofauti zetu lakini kanigeuka na kuniona sina maana kwake.”

“Lakini msingeweza kuishi kwa amani kwa vile  bado anatafutwa na serikali.”

“Serikali iliisha kata tamaa wasingesumbuka kwa vile walikuwa hawajui yupo hai au amekufa, hata rafiki yake walijua amekufa lakini mzima wa afya.”

“Basi msamehe baba yako.”

“Yote nilimsamehe lakini kwa hili mpaka nakufa sitamsamehe,” Koleta alisema kwa hasira huku akitokwa na machozi. “Lakini kumbuka ni mzazi wako?”

“Sawa ni mzazi wangu lakini narudia sitamsamehe mpaka nakufa aliyonitenda sasa inatosha.”

Baada ya kufikishwa nyumbani Koleta aliingia chumbani kwake na kuangua kilio cha sauti huku akiwa hajui hatima ya mpenzi wake ipo katika hali gani pia alijiuliza Ambe aliyemuhakikishia usalama atamuelewa vipi kutokana na hali ile kutokea.Alijikuta akilia usiku kuchwa mpaka alipopoteza fahamu ilibidi ifanyike kazi nyingine ya kumkimbiza hospitali.

Taarifa za kutolewa Koleta polisi zilirudisha furaha kidogo kwa mama yake. Lakini baada ya nusu saa aliletewa taarifa za Koleta kupoteza fahamu zilimchanganya sana.Alijikuta akichanganyikiwa na kuamini lazima mwanaye amekunywa sumu kutokana na karaha za baba yake.

Alianza kulia na kuelekea wodi aliyopelekwa, madaktari walimtoa hofu kuwa ule ulikuwa mshtuko kutokana na kuwa na hasira kali.

Walimhakikishia hali yake baada ya muda mfupi itakuwa sawa, kauli hiyo kidogo ilipunguza presha iliyoanza kupanda taratibu.Koleta baada ya kutoka polisi alirudi hadi kwao na kukutana na mfanyakazi wao wa kazi Ester.

“Ester Junior yupo wapi?”

“Amelala.”

“Mama?”

“Yupo hospitali na baba.”

“Baba hajafa tu?”

“Koleta maneno gani hayo baada ya kumuombea apone wewe unataka afe?”

“Tena asipokufa kwa hiyo risasi alizipigwa nitamuua mwenyewe.”

“Koletaaa!” Ester alishtushwa na maneno ya Koleta.

“Ester namchukia baba kuliko kifo.”

“Usifanye hivyo.”

“Wewe mwenyewe shahidi kanifanyia mambo mangapi mabaya nimemvumilia, ila leo sitamsamehe mpaka naingia kaburini na kuanzia aliponisaliti si baba yangu tena.”

“Usiseme hivyo Koleta yule ni baba yetu.”

“Labda kwako wewe si kwangu, yule ni adui yangu kuliko shetani.”Mara simu iliingia na kuipokea Ester, ilikuwa ikitoka hospitali.

“Haloo.”

“Haloo ni nyumbani kwa mzee Mtoe?”

“Ndiyo.”

“Ni hivi hali ya mama Koleta ni mbaya sana.”

“Mungu wangu kafanya nini?”

“Inasemekana taarifa za kushikiliwa polisi Koleta zilimemfanya apandwe na presha sasa hivi yupo katika chumba cha wagonjwa mahututi.”

”Mungu wangu.”

“Ester nini?” Koleta alishtuka.

“Mama.”

“Kafanya nini?” alisema huku akikwapua simu nakuzungumza.

“Haloo.”

“Haloo.”

“Eti kuna nini?”

“Kwani hujanielewa.”

“Mimi ni mtoto wake, mama kafanya nini?”

“Alipatwa na presha baada ya kusikia mtoto wake Koleta amebambikiwa kesi ya mauaji.”

“Mimi ninaye zungumza ndiye Koleta nimeisha toka na hakuna kesi yoyote.”

“Basi habari zako zimemchanganya.”

“Kwa sasa yupo wapi?”

“Yupo katika chumba cha wagonjwa mahututi.”

“Mama yangu, nooo.”Koleta alikata simu na kutoka mbio hadi kwenye gari, Ester alimfuata mbio kabla hajaondoka.

Je, nini kiliendelea hapo? Usikose kusoma kwenye Gazeti la Risasi, Jumatano ijayo.

Leave A Reply