The House of Favourite Newspapers

Joto la Mapenzi – 47

0

ILIPOISHIA…

Alijikuta akilia huku presha ikimpanda na kupoteza fahamu ilibidi ifanyike kazi nyingine ya kumkimbiza hospitali. Taarifa za kutolewa Koleta polisi zilirudisha furaha kidogo kwa mama yake. Lakini baada ya nusu saa aliletewa taarifa za Koleta kupoteza fahamu  na kukimbizwa pale hospitali zilimchanganya sana.

ENDELEA NAYO…

Mama mtu alijikuta akichanganyikiwa na kuamini lazima mwanaye amekunywa sumu kutokana na karaha za baba yake. Alianza kulia na kuelekea wodi aliyopelekwa, madaktari walimtoa hofu kuwa ule ulikuwa mshtuko kutokana na kuwa na hasira kali.

Walimhakikishia hali yake baada ya muda mfupi itakuwa sawa, kauli hiyo kidogo ilipunguza presha iliyoanza kupanda taratibu. Koleta baada ya huduma ya kwanza alirudiwa na hali yake pia alipewa taarifa za hali ya mama yake kuendelea vizuri baada ya kuelezwa sababu ya kuwa vile kulitokana na taarifa za kuzidiwa ghafla kwa mama yake.Baada ya muda mfupi aliweza kutembea mwenyewe na kwenda wodi aliyokuwa amelazwa mama yake. Koleta alizidi kumchukia baba yake kwa kitendo cha kikatili alichokifanya cha kutaka kuutoa na uhai wa mama yake kipenzi moyoni aliapa lazima amuue baba yake kwa mkono wake mwenyewe.“Mamaa,” Koleta alimkumbatia mama yake aliyekuwa bado kitandani.

“Koleta mwanangu umepona?”

“Ndiyo mama.”

“Polisi umetoka salama?”“Ndiyo mama, rafiki wa baba kanitoa.”

“Nilimtuma, nashukuru umetoka salama pia hali yako kuwa salama.”

“Asante mama kwa kuonesha upendo wa dhati juu yangu.”

“Vipi mwanangu polisi hawakukupiga?”

“Hawakunipiga nipo salama, vipi mama yangu unaendeleaje?”

“Kama umetoka salama nina imani nimepona.”

“Baba yupo wapi?”

“Yupo wodi ya peke yake chini ya uangalizi maalumu.”

“Lakini anaendeleaje?”

“Hajambo kidogo si kama alivyoletwa.”

“Basi mama pumzika nakwenda kumuona baba.”

“Haya mwanangu, vipi mjukuu wangu Junior hajambo?”

“Nina imani hajambo nimekuta amelala.”Koleta alikwenda chumba alichokuwepo baba yake, alipoingia alimkuta amelala usingizi mzito. Alimuangalia kwa uchungu mpaka machozi yakamtoka, alitamani ammalize lakini alihofia hali ya mama yake kwani angepata taarifa za kifo cha mumewe angeweza kufa kabisa.Koleta aliamini baba yake kuwa katika hali ile ya kulala fofofo bila kujitambua ilikuwa nafasi nzuri ya kumuua bila mtu yeyote kujua kwa kuamini amelala. Hali ya mama yake ilimtibua sana na kujikuta akilaumu polisi kumkamata na kusababisha mama yake kupandwa na presha lakini bila hivyo angeitumia nafasi ile kummaliza.Hakutaka kufanya haraka alipanga njia nyingine ya kumuua baba yake bila mama yake kujua kwa kumuwekea sumu kwenye chakula au kinywaji. Alipanga kufanya mpango ule kabla baba yake hajapona vizuri.

***

Mabina baada ya kumuokoa Ambe mikononi mwa kinywa cha mauti kwa kuamini kama angefikishwa polisi basi lazima angenyongwa kutokana na kesi isiyomuhusu. Ambe hakuzungumza lolote mpaka wanafika kijijini kwao, alipofika kwa uchungu wa kugeukwa na familia ya mpenzi wake aliinama na kuangua kilio kitu kilichomshtua Mabina na kumuuliza.

“Best unalia nini?”

“Siamini bila wewe ningekuwa wapi sasa hivi?”

“Yaone hayo yamepita tujipange kwa ajili ya kuwatia adabu.”

“Kina nani?”

“Mpenzi wako na familia yake japo sina uhakika kama mzee yule kapona.”

“Kwani umempiga sehemu gani?”

“Sijajua lakini nilimpiga sehemu ya kifua.”

“Inawezekana hajafa kwani alikuwa akipiga kelele ila nina wasiwasi na askari waliokuwa wamenishika kama wamepona.”

“Wale hawakupona niliwatageti vizuri.”

“Mzee haya umejifunzia wapi?”

“Nilishafanya kazi ya hatari ya kuvamia sehemu na kuiba mamilioni ya shilingi bila issue ya mzee ningekwishatoka.”

“Sasa tutafanya nini?”

“Kesho tunatinga mjini tukimkuta huyo mpenzi wako atatueleza kwa nini wametufanyia mchezo wa kitoto.”

“Mpenzi wangu ahusiki ametoa msaada mkubwa sana kwetu, haya niliposhikwa alijitahidi hata kuapa mbele ya polisi atamuua baba yake.”

“Sasa tufanyeje?”

“Tumtafute atusaidie kwa vile hata yeye hampendi baba yake itakuwa kazi nyepesi.”

“Ambe bado siamini kama yule msichana atamuua baba yake.”

“Mabina yule msichana namfahamu mimi, aliniapia kama tukio lile litatokea basi atamuua mwenyewe kwa mkono wake.”

“Basi kuna umuhimu wa kesho kwenda mjini kufanya upelelezi.”

“Hakuna tatizo ikiwezekana tuondoke naye.”

“Hakuna tatizo.”

***

Siku ya pili Koleta na mama yake waliruhusiwa kutoka hospitali na kurudi nyumbani lakini mama yake alibaki kwa ajili ya kumuuguza mumewe. Baada ya kufika nyumbani alikuwa na mawazo mengi juu ya hatima ya mpenzi wake kwa kujiuliza yupo katika hali gani pia kutaka kujua nani aliyezima taa na kwa nini aliwapiga risasi watu ambao aliamini walikuwa wenye makosa.Muda mwingi alikuwa katika dimbwi la mawazo kuhusu mpenzi wake yupo wapi. Alijiuliza kama mpenzi wake amepona  hatamuamini tena, lakini aliamini kama atamuua baba yake basi atamuamini. Aliwaza kwenda hospitali kufanya mchakato wa kumuua baba yake kabla hajapata nafuu nzuri.Ester aliyekuwa pembeni ya Koleta alimuonea huruma sana na kujikuta akijitahidi kumchangamsha baada ya kumuona akitokwa na machozi huku akijifyonza.

“Dada vipi?”

“Wee acha tu mdogo wangu, baba kajua kunitenda.”

“Sasa tutafanyaje na ndiye baba yetu hatuwezi kumbadilisha.”

“Hivi unajua Ambe yupo wapi?”

“Sijui, kwani baada ya taa kuzimwa si ulisema hukujua kilichoendelea zaidi ya vilio kwa maumivu ya risasi.”

“Ni kweli, sijajua  alipotelea wapi, mzima au amekufa.”

“Kwani nani aliyezima umeme?”

“Kwa kweli sijui.”

“Na kwa nini risasi amepigwa baba na maaskari, labda ni wenzake  waliokuja kumuokoa?”

“Kama ndiyo wenzake wamemuokoa itakuwa vizuri, je,  ataniamini tena baada ya kumuhakikishia kila kitu kipo sawa na mwisho wake kuangukia katika mikono ya polisi?”

“Hapo ndipo penye tatizo.”

“Hebu nisaidie rafiki yangu, baba ataendelea kuniharibia mpaka lini, kwa kitendo alichomtendea baba Junior siku za nyuma hakikuwa na msamaha, lakini nilimbembeleza na kunielewa na kukubali kuwasamehe wazazi wangu. Ambe kabla ya kukubali kuja nyumbani alinitahadharisha kama nitamgeuka basi atatuua wote.”

“Na wewe?”

“Eeh! Si nitakuwa nimemuingiza mkenge.”

“Unataka kuniambia kama Ambe alitoka salama atalipa kisasi?”

“Hakuna kipingamizi juu la hili hata mimi najua maisha yangu yapo mashakani.”

“Ambe anakupenda hawezi kukudhuru labda baba hata mama hana hatia.”

“Yaani baba alichonifanya najua nitamfanya nini,” Koleta alisema kwa uchungu.

“Lakini usimuue.”

“Hiyo haikuhusu.”

Wakati akibishana Ambe na Mabina walikuwa mjini katika mavazi ya watu wazima kwa kujiwekea ndevu nyingi. Walikwenda hadi katika duka la Koleta na kulikuta limefungwa.

“Sasa tutafanya nini?” Ambe alimuuliza Mabina.

“Tumpigie simu Koleta.”

“Mmh! Anaweza kuwa ameshikiliwa na polisi.”

“Tutajua baada ya kumpigia, kwa vile namba yetu haijasajiliwa hata kama kutakuwa na tatizo hawawezi kututambua ni sisi.”

“Nimekumbuka nina namba ya msichana wake wa kazi Ester.”

“Itakuwa vizuri mpigie yeye.”Ambe alimpigia simu Ester, baada ya kuita ilipokelewa upande wa pili.

“Haloo.”

“Haloo.”

“Nani?”

“Nazungumza na Ester?”

“Ndiyo, nani mwenzangu?”

“Ambe.”

“Ha! Shemu?” Ester alishtuka.“Ester taratibu.”

“Upo salama shemu?”

“Ester nani?” Koleta alijikuta amenyanyuka kutaka kujua simu ya nani.

Itaendelea wiki ijayo.

Leave A Reply