RAIS John Magufuli amempongeza Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro kwa kushughulikia suala la dhahabu ya magendo iliyokamatwa mkoani Mwanza, Januari 4, mwaka huu, ambapo polisi wanaodaiwa kuindikiza dhahabu hiyo walitiwa mbaroni na wengine kuvuliwa vyeo.
Magufuli amesema hayo leo Jumatano, Januari 9, 2019 baada ya kuwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua jana akiwemo Waziri wa Madini, Dotto Biteko.
“Nakupongeza sana IGP kwa kushughulikia suala la madini kule Mwanza, umefanya vyema kuwakamata wale askari waliokuwa wakizungumza na mtuhumiwa ili wapewe rushwa. Walishapewa Sh. Milioni 700 na nyingine waliambiwa watapewa Sengerema.
“Kwa taarifa nilizonazo, watuhumiwa wale walishikwa Januari 4, wilayani Misungwi, wakarudishwa mjini Mwanza na kikosi cha polisi annane, wakawapeleka Central wala hawakuwaingiza ndani. Watuhumiwa walikuwa kwenye gari, wakawa wanajadili namna ya kuwapa hela, wakawaambia watawapa bilioni moja na usiku wakaondoka.
“Askari polisi waliendelea kuzunguka na watuhumiwa kwa kutumia magari na mafuta ya serikali, wakavuka Kigongo Ferry kuelekea Sengerema. Niliwasiliana na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella na Mkuu wa Wilaya ya Sengerema ili wakamatwe… Iliwekwa road block na wakamatwa. Askari wale wakaanza kupiga king’ora eti walikuwa wanawafukuza kumbe walikuwa wanawasindikiza.
“Nakupongeza tena IGP kwa kuwashughulikia askari hao, tena huyo Superintendent wa Polisi aliyekuwa akisindikiza huo mzigo umemvua cheo, na watapelekwa kwenye mahakama za kijeshi kisha mahakama za kiraia,” alisema Magufuli.
Aidha ameitaka Wizara ya Madini na Tume ya Madini kufanya kazi kwa weledi na kwamba watendaji wabuni kitu kitakachokuwa na maslahi ya Watanzania.
Comments are closed.