JPM Ateua Wakuu wa Taasisi

RAIS John Magufuli leo Januari 21, 2020, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais na Ikulu, amefanya uteuzi wa wakuu katika taasisi za umma na serikali.
Katika uteuzi huo Prof. Maurice C.Y Mbago anakuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) akishika wadhifa huo kwa kipindi cha pili.
Pia amemteua Dkt. Masatu Masinde Leonard Chiguna kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) akichukua nafasi ya Prof. Ninatubu Mbora Lema ambaye uteuzi wake ulitenguliwa na bodi kuvunjwa.
Prof. Zacharia Mabubu Mganilwa Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) anakuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni ya Huduma ya Meli (MSCL).
Bi. Mariam Alu Nkumbi ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya Mkonge Tanzania huku Dkt. Adam Omar Karia akiteuliwa kuwa Mkuu wa Chuo cha Maji.
Wakati huo huo, Dkt. Godwill George Wanga aliyekuwa Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ameteuliwa kuwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Biashara la Taifa (TNBC)


